Ujenzi Mahakama haki za binadamu kuanza

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk Samwel Shelukindo akikabithi nyaraka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya CRJE  Africa Ltd, Zhang Cuishan kwa ajili ya kuanza rasmi mradi wa ujenzi wa Mahakama katika eneo la Lakilaki.

Muktasari:

  • Serikali imekabidhi rasmi eneo la hekari 26 kwa mkandarasi wa kampuni ya China ya CRJE    katika eneo la Lakilaki lililopo kata ya Mateves kwa ajili ya kuanza mradi wa ujenzi wa majengo ya Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu.

Arusha. Serikali imekabidhi rasmi eneo la hekari 26 kwa mkandarasi wa kampuni ya China ya CRJE    katika eneo la Lakilaki lililopo kata ya Mateves kwa ajili ya kuanza mradi wa ujenzi wa majengo ya Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu.

 Akizungumza leo Juni 3, 2023 jijini Arusha wakati wa hafla ya kukabithi nyaraka hizo kwa mkandarasi huyo, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk Samwel Shelukindo amesema, katika eneo hilo patajengwa majengo ya kisasa ya Mahakama hiyo.

Dk Shelukindo amesema ujenzi huo utachukua miezi 18 na utagharimu Sh9 bilioni na kwamba kwa makabidhiano hayo, na kwamba awamu ya kwanza ya mradi huo itahusisha ujenzi wa shule na hospitali ili kusogeza huduma hizo karibu.

"Pia kwenye eneo hilo, kumetengwa eneo maalum ajili ya ofisi za taasisi na mashirika ya kimataifa na tunashukuru sana serikali kwa kufanikisha malengo haya kwani ilikuwa ni shauku ya muda mrefu kumiliki jengo letu wenyewe," amesema.

Kwa upande wake Rais wa Mahakama hiyo Jaji Iman Aboud ameshukuru serikali kwa hatua hiyo kwani jambo hilo wamekuwa wakisubiri kwa muda wa miaka 16 sasa kwa ajili ya kuwa na jengo lao la kudumu.

Amesema kuwa mradi huo ambao ni mkubwa watajenga majengo ya kisasa na watahakikisha unakamilika kwa wakati na utatoa fursa za ajira kwa vijana na wananchi wengi mkoani Arusha.

Mkuu wa mkoa wa Arusha John Mongela ameyahakikishia mashirika na taasisi zote za kimataifa kuimarisha ulinzi kutokana na mkoa huo kuwa ndio kitovu cha sheria Afrika.

Mongela amesema kuwa uwepo wa majengo hayo utasaidia sana kuongeza fursa za ajira kwa wananchi wa mkoa wa Arusha sambamba na kuongeza dhamani katika mji wa Arusha.

"Tunamshukuru sana Rais Samia kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa majengo haya kwani kuwepo kwa majengo hayo kunaenda kuongeza thamani ya mkoa wetu wa Arusha sambamba na kuwepo kwa fursa nyingi za ajira," amesema Mongela.

Kwa upande wa Mkurugenzi  wa kampuni hiyo ya CRJE  East Àfrica Ltd Zhang Cuishan amesema kuwa, wamekuwa wakitekeleza miradi mbalimbali kwa muda mrefu nchini Tanzania na kuwa mradi huo wanaahidi kumaliza kwa wakati kwani tayari kazi inaanza  rasmi na vifaa tayari vipo eneo la mradi .