Prime
Ujenzi usiozingatia taaluma wahatarisha usalama wa shule
Muktasari:
- Uchunguzi unaonesha baadhi ya shule zimejengwa bila kufanyika kwa utafiti wa kina wa mazingira na bila kuhusisha wataalamu, hali inayosababisha majengo kuwa dhaifu, kuharibika kwa haraka na kuhatarisha usalama wa wanafunzi na walimu
Dar es Salaam. Licha ya mvua zinazoendelea kuonekana kama chanzo kikuu cha uharibifu wa miundombinu ya shule, wadau wa ujenzi na mazingira wanasema tatizo kubwa linaanzia kwenye hatua za awali za upangaji na ujenzi wa shule hizo.
Uchunguzi unaonesha baadhi ya shule zimejengwa bila kufanyika kwa utafiti wa kina wa mazingira na bila kuhusisha wataalamu, hali inayosababisha majengo kuwa dhaifu, kuharibika kwa haraka na kuhatarisha usalama wa wanafunzi na walimu.
Mhandisi wa ujenzi, Hamis Mshana anasema kuongezeka kwa makorongo katika maeneo ya shule ni ishara ya moja kwa moja ya udhaifu katika upangaji na utekelezaji wa miundombinu ya kudhibiti maji.
“Unapoona makorongo yanaanza kujitokeza ndani au pembezoni mwa shule, ujue maji hayakudhibitiwa ipasavyo tangu mwanzo. Haya maji yanapopita kwa kasi, yanaondoa udongo hatua kwa hatua na kuacha mashimo makubwa yanayoendelea kupanuka kila mvua inaponyesha,” anasema Mshana.
Makorongo yaliyopo Shule ya Msingi Bwawani iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo ambayo yametokana na mvua.
Anasema hali hiyo ndiyo inayosababisha baadhi ya madarasa kuanza kupata nyufa au hata msingi kudhoofika.
“Makorongo haya yanapokaribia majengo, huanza kuathiri msingi wa darasa, udongo unaoshikilia jengo unapungua na matokeo yake unaona nyufa kwenye kuta, sakafu kupasuka, au hata jengo kuanza kuinama kidogo.”
Anasema kama hatua za haraka hazitachukuliwa, baadhi ya madarasa yako kwenye hatari ya kuendelea kuharibika au kutokuwa salama kabisa kwa matumizi.
“Ni muhimu sana kuchukua hatua mapema kwa kujenga mifereji ya maji, kurekebisha maeneo yaliyochimbika na kuimarisha msingi wa majengo yaliyoathirika. Vinginevyo, uharibifu utaongezeka na gharama ya marekebisho itakuwa kubwa zaidi,” anasema.
Profesa Geraldine Kikwasi kutoka Chuo Kikuu Ardhi anasema matumizi ya watu wasio wataalamu katika kubuni na kujenga miundombinu ya shule yanachangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa ubora wa mazingira ya kujifunzia na kuhatarisha usalama wa wanafunzi.
Profesa Kikwasi anasema pamoja na kuwepo kwa maeneo yaliyotengwa rasmi kwa ajili ya ujenzi, bado kuna kasoro kubwa katika utekelezaji, hasa pale ambapo wataalamu husika hawahusishwi ipasavyo.
Wanafunzi wakipita jirani na darasa ambalo kingo moja ya ukuta imeanguka kutokana na mvua katika shule ya Msingi Malamba Mawili iliyopo Wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam
“Kwa kawaida kuna maeneo ambayo tayari yametengwa na hayaruhusiwi kujengwa kiholela, ukiona shule imejengwa, maana yake ilipata kibali. Lakini tatizo linakuja kwa wanaobuni na kusimamia ujenzi huo,” anasema.
Anasema ujenzi wowote unatakiwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa hata kama unasimamiwa na Serikali kwani kila kitu kinafanyika kwa mujibu wa sheria pindi yatakapotokea madhara.
Profesa Kikwasi anasema licha ya uwepo wa sheria mbalimbali zinazosimamia ujenzi na mazingira nchini, bado utekelezaji wake unaonekana kuwa changamoto.
Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, miradi yote ya maendeleo inapaswa kufanyiwa tathmini ya athari za mazingira kabla ya kuanza, huku Sheria ya Mipango Miji ya mwaka 2007 ikisisitiza ujenzi kufanyika katika maeneo salama na yaliyopangwa kitaalamu.
Anasema baadhi ya miradi ya ujenzi wa shule hutumia watu wasiokuwa wabunifu majengo (architects) au wahandisi wenye sifa stahiki, hali inayosababisha majengo kujengwa chini ya viwango na hata kuhatarisha maisha.
“Unakuta mtu anajenga bila kutumia mtaalamu sahihi matokeo yake ni majengo yasiyo imara, mengine yanaanza kupasuka, au hata miundombinu kama barabara za ndani ya shule inaharibika mapema kwa sababu haikuzingatia mifumo sahihi ya maji na kingo.”
Kwa mujibu wa profesa huyo, madhara ya hali hiyo huonekana moja kwa moja kwa wanafunzi na walimu, baadhi ya shule hukumbwa na mazingira magumu yasiyofaa kwa kujifunzia.
“Unakuta kuna utelezi, mashimo na hata mifereji isiyo salama katika maeneo ya kuchezea watoto hali hii inawanyima wanafunzi nafasi ya kujifunza na kucheza kwa usalama,” anasema Profesa huyo.
Mtaalamu wa masuala ya ramani (Architecter), Selua Barabara anasema hatua ya kwanza kabla ya ujenzi wowote wa shule ni kufanya uchunguzi wa kina wa eneo husika, ikiwamo aina ya udongo, uwepo wa miamba pamoja na hali ya maji ardhini.
“Lazima kwanza ujue eneo ulilolipata lina udongo wa aina gani. Je, ni imara au laini? Kuna miamba au hakuna? Na kama kuna maji, yako katika kiwango gani? Haya yote ni muhimu kabla ya kuanza ujenzi,” anasema Selua.
Sehemu ya kipande cha ardhi kilichoondolewa na mvua katika Shule ya Msingi Msigani ambayo ipo jirani na mto.
Anasema mtaalamu wa sayansi ya maji na uchunguzi wa udongo ni muhimu katika kupanga majengo imara na salama. Bila kufanya hivyo, majengo yanaweza kujengwa katika maeneo yasiyofaa na kusababisha madhara makubwa baadaye.
“Ukijenga bila kujua hali ya maji au miamba iliyopo chini ya ardhi, unaweza kujikuta jengo linaanza kuporomoka au ardhi inazama, hii ni hatari kwa wanafunzi na walimu,” anasema.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, baadhi ya shule zilizojengwa katika maeneo yenye changamoto zimekuwa zikikumbwa na matatizo kama nyufa kwenye majengo, utelezi, au hata maji kutuama katika maeneo ya shule, hali inayohatarisha afya na usalama wa watoto.
Anasema kuwa hali hiyo inatokana na kupuuza hatua muhimu za kitaalamu kabla ya ujenzi kuanza.
“Changamoto hizi zinatokea kwa sababu hatua za awali hazikufanyika. Hakukuwa na uchunguzi wa udongo, hakuna tathmini ya maji, wala mipango ya kitaalamu ya ujenzi,”anasema.
Baadhi ya viroba vyenye mchanga vikiwa vimepangwa ili kuzuia mmomonyoko wa ardhi katika shule ya Msingi Msigani ambayo ipo jirani ma mto
“Shule zinapaswa kupitishwa katika utaratibu ule ule wa tathmini kama miradi mingine. Wataalamu wa mazingira, maji, ujenzi na mipango miji washirikishwe kikamilifu.” Anasema ni lazima kuwe na ushirikiano wa wataalamu mbalimbali ili kuhakikisha usalama na ubora wa maeneo na majengo ya shule.
“Unahitaji kuangalia mambo mengi usalama wa eneo, hali ya maji, ubora wa udongo, hata athari za mazingira kwa ujumla. Haya yote yakizingatiwa, ndipo unaweza kuwa na shule salama,”anasema.
Nini kifanyike
Profesa Kikwasi anasema suluhisho la changamoto hiyo ni kuhakikisha kuwa wataalamu wanaohusika na ujenzi wakiwamo wabunifu majengo na wahandisi wanapewa nafasi ya kufanya kazi zao kikamilifu badala ya kurukwa katika mchakato.
“Tuna wataalamu wanaoitwa washauri ukiwaruka hawa, lazima utapata matatizo, wao ndiyo wanatoa ushauri sahihi wa kitaalamu kuanzia msingi hadi mwisho wa ujenzi,” anasema Profesa Kikwasi.
Pia, anagusia suala la bajeti, akibainisha kuwa shule nyingi za Serikali hukumbwa na changamoto ya fedha, jambo linalochangia baadhi ya hatua muhimu za ujenzi kupuuzwa.
“Serikali ina bajeti yake, wakati mwingine inalazimika kujenga kwa kutumia kile kilichopo. Lakini unakuta kuna mambo muhimu hayajawekwa kwenye bajeti, hivyo yanaachwa na hapo ndipo matatizo yanapoanzia,” anasema.
Pia, anatoa wito kwa Serikali na wadau wa elimu kuhakikisha kuwa kila mradi wa ujenzi wa shule unazingatia viwango vya kitaalamu, ili kulinda usalama wa wanafunzi na kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Viroba vikiwa vimewekwa pembezoni mwa darasa ili kuzuia mmomonyoko wa udongo utakaoathiri msingi.
“Ili watoto wasome katika mazingira salama na yenye tija, ni lazima tuzingatie utaalamu katika kila hatua ya ujenzi wa shule,” anahitimisha.
Anashauri kuwepo kwa mifumo madhubuti ya ufuatiliaji na tathmini (monitoring and evaluation), pamoja na kuwachukulia hatua kali wale wote wanaotekeleza miradi bila kuzingatia sheria za mazingira.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuhusisha wataalamu wa mazingira katika kila hatua ya upangaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kulinda maisha ya wananchi na mazingira kwa ujumla.
Kwa sasa, wananchi wengi wanaendelea kuathirika na madhara ya moja kwa moja ya kupuuzwa kwa ushauri wa kitaalamu, hali inayohitaji hatua za haraka kutoka kwa mamlaka husika.
Kamanda wa Kikosi ca Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala, Peter Mabusi anasema japokuwa hawajawahi kukutana na kadhia ya watoto kusombwa na maji eneo la shule au ajali, muhimu walimu kuwa kribu na wanafunzi kipindi chote chamvua.
“Kipindi cha mvua walimu, wazazi na walezi wanatakiwa kukaa karibu na wanafunzi huku wakiendelea kutoa elimu ya madhara ya mvua kutokana na maeneo waliopo kuepuka madhara yoyote ikiwepo kukaa kwenye miti na maeneo mengine hatarishi,”anasema Mabusi.
Mpango wa Serikali
Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais–Tamisemi, Dk Festo Dugange anasema Serikali inatambua athari kubwa zilizotokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini, ikiwamo uharibifu wa barabara, madaraja na miundombinu ya shule.
Wananfunzi wakifanya usafi kwenye moja ya korongo lililopo katika shule ya msingi Malamba Mawili iliyopo wilaya ya ubungo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwananchi Aprili 29, 2026 kuhusu hali hiyo, Dk Dugange anasema licha ya mvua kuwa na manufaa kwa sekta mbalimbali, zimeambatana na changamoto zinazohitaji hatua za dharura, hususani katika maeneo yaliyoathirika zaidi.
“Tumeshuhudia uharibifu wa miundombinu mbalimbali ikiwamo barabara zetu kuharibika kutokana na maji mengi, lakini pia baadhi ya shule zimeathirika, hali inayohatarisha usalama wa wanafunzi,” anasema Dk Dudange.
“Tunaendelea na tathmini ya maeneo yote hatarishi, tayari tumetoa maelekezo kwa mamlaka husika katika ngazi za halmashauri kuanza kufanyia kazi suala hili na tunapokea taarifa,” anasema.
Anasema hatua zitakazochukuliwa zitategemea matokeo ya tathmini hiyo, ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho au hatua nyingine za kudhibiti athari za mmomonyoko na kulinda miundombinu ya shule.
“Baada ya tathmini, kila eneo litapatiwa ufumbuzi kulingana na uhitaji wake ili kuhakikisha usalama wa wananchi unaendelea kulindwa,” anasema.
Anasema Serikali itaendelea kuchukua hatua stahiki kuhakikisha athari za mvua hazizuii utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi, hususani katika sekta ya elimu na usafiri.
Pia, anasema Serikali kupitia viongozi wa ngazi za vijiji, vitongoji na kata imeelekeza kuhakikisha wanachukua hatua za haraka kulinda miundombinu ya shule na usalama wa wanafunzi, hasa katika maeneo yenye hatari ya maji kutuama au mafuriko.
“Tumewasisitiza viongozi wetu kuhakikisha wanachukua tahadhari maalumu kwenye maeneo yenye madimbwi au maji yanayotiririka ili kuepusha ajali, ikiwamo watoto kuzama,” anasema.
Aidha, anasema Serikali inaendelea kusimamia matengenezo ya miundombinu iliyoharibika, ikiwamo vivuko na madaraja, ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma na wanafunzi wanafika shuleni kwa usalama.
“Pale ambapo inawezekana kufanya matengenezo ya haraka, tayari kazi zinaendelea kufanyika ili kurejesha huduma katika hali salama,” anasema.
Katika hatua nyingine, Dk Dugange ametoa wito kwa wazazi, walezi, walimu na jamii kwa jumla kushirikiana katika kuhakikisha usalama wa watoto unalindwa wakati huu wa mvua.
“Natoa wito kwa wazazi, walezi, watoto wetu, walimu na viongozi wa ngazi zote kuhakikisha wanakuwa karibu na watoto na kufuatilia maeneo hatarishi ili kuepusha ajali zisizo za lazima, ikiwemo watoto kuzama au kupata madhara mengine,” anasema.
Anasema ushirikiano wa jamii ni muhimu katika kipindi hiki ili kupunguza athari zinazoweza kuepukika, huku akiwataka viongozi wa Serikali za vijiji na mitaa kuendelea kuhamasisha wananchi kuchukua tahadhari.