Ujenzi wa daraja la JPM wafikia asilimia 78

Barozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian (wa pili kushoto) akionyeshwa jambo na Meneja Mkuu wa Kampuni la China Civil Engeneering Costruction Corporation (CCECC), Zhang Junle wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua Mradi daraja la Magufuli la Kigongo Busisi na kampuni hiyo. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Daraja la JPM maarufu kama daraja la Kigongo - Busisi umefikia asilimia 78.

Mwanza. Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Daraja la JPM maarufu kama daraja la Kigongo - Busisi umefikia asilimia 78.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh700 bilioni wakati wa ziara ya Balozi wa China nchini, Chen Mingjian, Septemba 9, 2023; Meneja Mkuu wa kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) Afrika Mashariki inayojenga daraja hilo, Zhang Junle amesema hadi sasa, ujenzi wa nguzo kuu tatu za daraja, nguzo za msingi 804  na nguzo mlalo 806 tayari umekamilika.

Amesema kwa sasa kazi inayoendelea katika mradi huo ulioanza Februari 25, 2020 na unaotarajiwa kukamilika Februari 24, 2024 ni ujenzi wa eneo la juu ya Daraja lenye urefu wa kilometa 3.2 litakalounganishwa na barabara za njia nne kila upande zenye urefu kilometa 1.66.

Zhang alimweleza Balozi Chen kuwa kukamilika kwa daraja hilo siyo tu itaunganisha mikao ya Mwanza, Geita, Kagera na Kigoma, bali pia itarahisisha shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo kwenda na kutoka nchi jirani za Uganda, Rwanda na Burundi.

"Kukamilika kwa mradi huu kuapunguza muda wa kuvuka eneo la Kigongo - Busisi kutoka dakika 45 kwa kutumia kivuko hadi dakika 5 kwa gari au dakika 15 kwa miguu," amesema Zhang

Kuhusu manufaa kwa umma wa Tanzanzia, Meneja Mkuu huyo amesema utekelezaji wa mradi huo unahusisha makandarasi 17 wa ndani, watoa huduma 20 huku zaidi ya wahandisi 1,200 na wafanyakazi kadhaa wenye ujuzi wa Kitanzania wakiwa wameajiriwa.

“Teknolojia za kisasa na usanifu zinatumika katika ujenzi wa daraja hili, na hivyo kutoa fursa kwa wahandisi,  mafundi na waajiriwa wa ndani kujifunza kwa kupata ujuzi utakaowawezesha kutekeleza miradi mwingine ya aina hii siku zijazo,” amesema Zhang

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo pamoja na ule wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR ambao pia alitembelea, Balozi Chen ameeleza kuridhishwa na kazi inayofanyika huku akiahidi nchini yake kuendeleza, kuboresha na kuimarisha ushirikiano na Tanzania, hasa katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu muhimu. Lengo likiwa ni kuboresha uchumi, maendeleo na maisha ya watu.

Amesema katika utekelezaji wa mpango huo, biashara na uwekezaji kati ya China na Tanzania imeongezeka mara dufu katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Amesema ndani ya kipindi hicho, thamani ya shughuli za kibiashara na uwekezaji nchini kutoka China imeongezeka kutoka Dola za Kimarekani 3.7 bilioni hadi kufikia zaidi ya dola bilioni 8.

Kuhusu SGR, Balozi Chen amewataka wanaotekeleza mradi SGR kipande cha tano kutoka Mwanza hadi Isaka mkoani Shinyanga kutekeleza kazi hiyo kwa weledi, ubora na kwa wakati.

Mradi wa reli hiyo kutoka Mwanza hadi Isaka yenye urefu wa kilomita 342 unaotekelezwa kwa Sh3.06 trilioni, unatarajiwa kukamilika Mei, 2024.

Akizungumza kwa niaba ya kamati ya Bunge ya urafiki kati ya China na Tanzania, Mbunge wa Masasi Mjini, Godfrey Mwambe aliishukuru Serikali ya China kwa kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo huku akiiomba ushirikiano huo wa kihistoria uendelezwe kwa faida na maslahi ya umma.

Ametaja reli ya Tazara inayounganisha Tanzania na Zambia kuwa miongoni mwa alama za kudumu za ushirikiano kati ya Tanzania na China tangu enzi ya awamu ya kwanza chini ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa kiongozi wa China Mao Zedong.