Ujerumani kutoa Sh68 bilioni kwa Tanzania

Ujerumani kutoa Sh68 bilioni kwa Tanzania

Muktasari:

  • Serikali ya Ujerumani na Tanzania wametia saini mkataba wa Sh68 bilioni kwa ajili ya kuimarisha miradi ya uhifadhi katika Hifadhi za Taifa nchini.

Serengeti. Serikali ya Ujerumani na Tanzania wametia saini mkataba wa Sh68 bilioni kwa ajili ya kuimarisha miradi ya uhifadhi katika Hifadhi za Taifa nchini.

Mkataba huo umelenga miradi mikubwa miwili ambayo ni mfumo wa ikolojia wa Katavi na Mahale wenye thamani ya Sh46 bilioni na mradi wenye thamani ya Sh22 bilioni wa maendeleo ya uhifadhi katika mfumo wa Ikolojia ya Serengeti.

Msaada huo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba wa msaada huo leo Jumanne Septemba 14, 2021 mkurugenzi wa Serikali ya Ujerumani anayeshughulikia masuala ya Bara la Afrika,   Dk Stefan Oswald amesema kuwa msaada huo pia unalenga kusaidia kupunguza madhara yaliyotokana na ugonjwa wa Uviko 19 katika sekta ya utalii.

Amesema kuwa miongoni mwa sekta zilizoathirika na ugonjwa huo ni pamoja na sekta ya utalii baada ya watalii wengi kusitisha safari zao hivyo kupelekea mapato yatokanayo na utalii kushuka hatua ambayo kwa namna moja ama nyingine ilisababisha  kushindwa kutekelezwa kwa shughuli nyingine ikiwemo utunzaji wa ikolojia ya Hifadhi za Taifa.

Katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na  Utalii, Dk Allan Kijazi amesema  msaada huo umekuja kwa muda muafaka kwani mapato ya  Hifadhi za Taifa yameshuka kwa kiwango kikubwa kutokana na kuwepo kwa ugonjwa wa Uviko- 19 duniani.

Amefafanua kuwa hifadhi za taifa zinategemea mapato yake kutokana na ada za utalii ili kuweza kujiendesha na kwamba kutokana na mapato hayo kushuka zipo shughuli nyingi hazijatekelezwa  kutokana na upungufu wa fedha.

Naibu waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema msaada huo utasaidia  kutekeleza na kuimarisha zaidi shughuli na jitihada za uhifadhi nchini.