Ukabila ulivyomtenganisha Pendo na mwenza wake

Muktasari:

  • Ukabila pekee haukutosha kuwatenganisha Pendo William na mume wake, ila pia unene uliomchukiza mama mkwe wake ulizima ndoto yake ya kuolewa.

Dodoma. Ukabila pekee haukutosha kuwatenganisha Pendo William na mume wake, ila pia unene uliomchukiza mama mkwe wake ulizima ndoto yake ya kuolewa.

Pendo (29) ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto wanne. Alizaliwa mkoani Mwanza. Baada ya kupoteza wazazi wake, hivyo alilelewa na bibi yake. “Baba yangu alifariki mama akiwa na ujauzito wangu wa miezi nane na mama alifariki baadaye nikiwa na miaka mitano,”anasema Pendo.

Tabia za ukali, ulevi na manyanyaso kutoka kwa bibi yake vilimtorosha hadi kwenda kulelewa kusikojulikana na mtu aliyemuita ‘Baba.’ Anasema licha ya kulelewa vizuri na kuanzishwa shule na baba huyo, bado kila wakati ilimjia taswira ya nyumbani kwao (kwa bibi).

Hivyo aliamua kurudi nyumbani, ambapo familia iliamua akaishi kwa mama yake mdogo huko kijijini Nyakalilo.

“Mateso niliyoyaacha kwa bibi yalikuwa mara mbili ya niliyoyakuta kwa mama mdogo, nilikuwa kama mtumwa na sikusoma shule kwa kipindi cha miaka miwili,” anasimulia.

Kutosoma kulimsononesha kiasi cha kupanga njama za kumtishia mama yake mdogo kuwa atachukuliwa hatua na Serikali kwa jambo hilo.

“Baada ya vitisho ndipo akanianzisha shule lakini elimu yangu iligubikwa na kazi nyingi kuliko umri wangu mpaka namaliza darasa la saba,” anasema Pendo. Licha ya kufaulu hakuendelea na elimu ya sekondari, akaanza kazi ya mama lishe akipokea Sh 7,000 kwa mwezi, ndani ya miaka mitatu.

Awekewa dawa za kulevya na kubeba ujauzito

Akiwa mama lishe, alitakwa kimapenzi na kijana wa mtaa aliofanyia kazi.

“Siku moja rafiki yangu alitaka tukatembee licha ya kumkatalia. Tulipofika tuendapo tulikutana na watu aliofahamiana nao. Wao walikunywa pombe, mimi nilikukunywa soda. Walinishawishi kunywa pombe, nilikataa,”anasema Pendo.

Baadaye alimuona kijana aliyewahi kumtongoza na kumkatalia akiingia sehemu walipokuwepo. Aliendelea kulazimishwa kunywa pombe iliyomshinda kwa uchungu huku rafiki yake akimsihi aendelee akitaka uchungu uishe.

Kwa mujibu wa Pendo, rafiki yake alimuomba kumsindikiza chooni na aliporudi alilazimishwa kunywa tena na ndipo akapoteza fahamu.

“Nilikunywa kidogo na kuhisi usingizi mzito, rafiki yangu alinitaka nilale miguuni mwake akimalizia kunywa kabla ya kurudi nyumbani,”anasema. Alishtuka saa 8 usiku katika nyumba ya wageni na kijana aliyemtongoza na kumkatalia muda mrefu.

Pendo anasema kijana huyo alimbaka na kupata ujauzito wa mtoto wake wa kwanza akiwa na miaka 13. Aliporudi kwa bibi, alimfukuza kuhofia kumpoteza Pendo kwa kubeba mimba akiwa na miaka 13.

“Mimba ilipofikisha miezi nane alinifukuza nyumbani akisema anaogopa kesi kwa kuwa nilikuwa mdogo. Nilienda kwa rafiki yangu (Mariamu) aliyenisababishia ujauzito naye aliwasiliana na yule mwanaume ili nikakae nyumbani kwao,”anasema.

Mwanaume yule alikubali kuishi nae na kumuahidi kumsomesha akishajifungua. Baada ya kujifungua, baba mtoto wake alimgeuka na kumuonya atawaacha na yeye ataolewa kwingine.

“Wote walikengeuka, huku baba mtoto akawa mlevi na mama yake mzazi kunisimanga kwa kunipa hifadhi mpaka kujifungua kwangu. Waliniambia niondoke kama sitaki kuishi pale,” anasimulia. Pendo anasema baada ya muda walihamia Geita baada ya mume wake huyo kupata kazi katika duka la dawa.

“Baada ya kuhamia kwao mateso yalizidi, alikuwa si mtu wa kuacha fedha ya matumizi na kuanza kutembea na wanawake wengine,”anasema.

Walivyokutana na mchumba

Baada ya mateso, alianza kuuza viatu, nguo za kike na kiume na kupata kipato kilichomwezesha kupanga chumba. Alianza maisha yake na mwanawe baada ya kutoka kwa mwanaume wake aliyempa ujauzito wa kwanza.

Mwaka 2018, Pendo alikutana na mwanaume mwingine ambaye walipanga kufunga ndoa mara tu akishahitimu katika chuo cha ualimu wa sekondari Butimba.

Alishika ujauzito katika mwaka wa kwanza wa uhusiano huku akidai mwanaume huyo alifurahi kunusurika na mila za kabila la Kibembe za kijana wa kwanza kuoa mwanamke wa kabila lake.

“Baada ya kujifungua, alikuja Geita kuniangalia na kunitaka tufunge ndoa ya Serikali,”anaeleza. Pendo alikataa pendekezo hilo na mwanaume wake alimtaka wale kiapo cha damu wasitenganishwe na chochote badala yake.

“Alikuja na wembe na tulikata vidole vyetu na mimi nikalamba damu yake na yeye akalamba yangu, lengo ni kutoachana milele,” anafafanua.

Nyumbani kwa mwanaume wake, wazazi walimkataa Pendo kuolewa na mtoto wao kutokana na unene, pia hakutoka kabila la Kibembe. Licha ya wazazi kugomea ndoa, mwanaume yule alirudi Geita kuishi naye huku wazazi wakilaani kitendo hiko.

“Miaka miwili baadaye, nilibeba ujauzito wa pili na mwanaume huyo alinitaka niutoe, nami nilikataa, ugomvi ukaanzia hapo,” anasema Pendo.

Anasema, “Wakati huo nilikuwa ninauza genge, alikuja na kusomba fedha zote kwa matumizi yake kwa kuwa alikuwa hana kazi. Tulishindwa kulipa kodi,” anasema.

Pendo alimtafuta baba wa mumewe kumueleza changamoto hizo na kuomba msaada wa kifedha. Baada ya kimya cha wakwe zake juu ya suala hilo, ujauzito ulipofikisha miezi saba mumewe alianza uasherati mbele yake na kumpiga.

Baadaye baba mkwe wake alikwenda Mwanza kumuombea Pendo kwa familia yake kuishi Arusha ili wakalee familia ya mtoto wao (Samweli) aliyekuwa hatunzi familia.

Alipofika Arusha alihojiwa na familia kuhusu mpango wa kuishi na watoto wake na mumewe. Anasema, mzazi mwenzake aliwaambia wazazi wake kuwa ana mpango wa kufunga ndoa na yeye ili walee familia yao baada ya kujifungua.