Ukame ulivyotikisa kilimo, ufugaji nchini

Muktasari:

  • Ni vilio vinavyofanana katika kila sehemu waliyoitembelea waandishi wa habari wa Mwananchi waliokuwa wakifuatilia taarifa za hali ya ukame – mifugo kufa, wananchi kuishi kwa mlo mmoja na mahudhurio duni ya wanafunzi shuleni.
  • Haya yote yametajwa kama matokeo ya ukame uliopitiliza katika maeneo mengi na kusababisha madhila makubwa kwa wananchi.

Ni vilio vinavyofanana katika kila sehemu waliyoitembelea waandishi wa habari wa Mwananchi waliokuwa wakifuatilia taarifa za hali ya ukame – mifugo kufa, wananchi kuishi kwa mlo mmoja na mahudhurio duni ya wanafunzi shuleni.

Haya yote yametajwa kama matokeo ya ukame uliopitiliza katika maeneo mengi na kusababisha madhila makubwa kwa wananchi.

Rombo

Mwandishi wetu aliyetembelea Kata ya Njoro, Wilaya ya Same ambayo ina vijiji vitatu anaeleza kuwa baadhi ya vijana wamezikimbia familia zao na kuwaacha wazee, watoto na wanawake wakitaabika bila msaada na kugeuka kuwa ombaomba kunusuru familia zao.

Kijiji cha Emuguri ambako wanaishi wafugaji kimeathirika zaidi na hali hiyo na mwenyekiti wake, Moses Naimani anasema kwa zaidi ya miaka mitatu hawajapata mvua za kutosha katika eneo hilo.

“Familia nyingi kwa sasa hazina chakula, hali ya mifugo – mbuzi, kondoo na ng’ombe nayo ni ngumu. Watu wanaishi kwa kunywa uji, tena mlo mmoja kwa siku, huku ng’ombe wakianguka na kufa kwa kukosa malisho, tunaomba Serikali itusaidie.

“Katika kijiji changu vijana wengi wamekimbia familia, wamewaacha wake zao, watoto na wazee wakihangaika. Kwa sasa zaidi ya familia 20 zimetelekezwa, hazina msaada,” anasema.

“Ukiacha hao waliotelekeza familia, wengine wamehama na mifugo michache iliyobaki kwenda kutafuta malisho, hivyo ukiangalia wanaotaabika zaidi hapa ni wanawake, wazee na watoto, walioachwa nyumbani.”

Mzee Mbuyuki wa kijiji hicho mbali ya kupoteza mifugo, analia kuelemewa na mzigo wa familia.

“Nimebaki nyumbani na wake zangu wawili, watoto wangu wadogo watano ambao hawajaenda shule na mmoja ameanza shule ya awali. Pamoja na wake wa watoto wangu, nina watoto wao (wajukuu wake) zaidi ya sita, tunapata chakula kwa bahati, watoto wakipata uji asubuhi, jioni wakiupata tena inakuwa ni afadhali wanalala, lakini sisi watu wazima tunakula mlo mmoja tu tena kwa taabu.”

Mzee huyo anasema ng’ombe wake wanakufa kila uchao na sasa wamebaki wanane pekee, wenye hali mbaya kiafya kati ya 40 aliokuwa nao.

Licha ya kwamba anajishughulisha pia na kilimo, mzee huyo anasema kwa zaidi ya miaka mitatu hawajavuna kutokana na ukame na uvamizi wa tembo.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Raheli Lazaro anaeleza kuwa kinamama ambao wengi wao ndio wameachwa kuwa waangalizi wa familia, hawana chakula.

“Mifugo na sisi binadamu tumeathirika sana, hakuna chakula nyumbani, kuna wakati tunaweza kubahatisha kidogo au kupika uji, lakini wakati mwingine tunageuka ombaomba kwa majirani wenye chochote ili tuwape watoto,” anasema na kuongeza:

“Wakati mwingine watoto wanalala bila kula, akiamka usiku kukusumbua unampa maji na kumbembeleza alale, yaani baadhi ya familia watoto wana hali mbaya sana na zisipochukuliwa hatua za makusudi haraka, tunaweza kupata majanga.”

Ester Yohana anasema mifugo mingi imekufa kwa kukosa malisho na wale wenye uwezo kidogo wameinunulia pumba.

“Familia hazina chakula, watoto wanashinda na kulala na uji, sina mume na watoto wamenikimbia na kuniachia wajukuu ambao ninawalea, kuna wakati wanashindwa kwenda shule kutokana na njaa, hali ni mbaya,” anaeleza Ester.

Kauli za wanakijiji hao zinapewa nguvu na Elitwaza Mbajo, mwenyekiti wa kijiji hicho anayesema hali ya chakula katika eneo lake ni mbaya, “kijiji hiki kina watu zaidi ya 2,800, wote hawana chakula lakini zaidi ya nusu ya wananchi hao wana hali mbaya zaidi na wanahitaji msaada wa haraka.”

Bei ya mahindi vs ng’ombe

Hadi wiki mbili zilizopita, thamani ya baadhi ya mifugo katika eneo la Njoro ilikuwa imeporomoka kwa kiwango kikubwa.

Raheli anasema wananunua gunia moja la mahindi kwa Sh120,000 hadi 130,000, thamani ambayo ni kubwa kulinganisha na bei ya mifugo. Mbuzi wanauzwa kati ya Sh15,000 hadi 20,000 na ng’ombe Sh40,000 hadi Sh60,000.

“Bei ya ng’ombe kwa sasa ni kama ya mchicha, tunauza mpaka Sh30,000 ng’ombe ambaye tulimuuza kwa Sh400,000 na kuendelea, kimsingi hali ni mbaya, tunaiomba Serikali, itusaidie mahindi ya bei nafuu ili watu wapone,” anasema Moses Naimani.

Mwanga

Hali ikiwa hivyo Same, wilaya jirani ya Mwanga kilio ni kilekile. Kidonda katika jeraha hilo kinatiwa chumvi na uvamizi wa wanyamapori katika mashamba ya wakulima, hasa katika kata za Kwakoa, Kigonigoni, Toloha na Mgagao ambazo upungufu wa mvua na uvamizi wa tembo vimewafanya baadhi ya wakulima kutelekeza mashamba yao kwa zaidi ya misimu minne sasa.

Diwani wa Kigonigoni, Jeremiah Aloyce anasema, “tukiachilia mbali mabadiliko ya hali ya hewa, wananchi wameshindwa kulima mazao hata ya muda mfupi au yale yanayohimili ukame kutokana na wanyama wanaovamia mashamba na kuharibu mazao.”

Anasema matokeo yake yamekuwa mabaya si tu kwa binadamu, bali pia wanyama na kuwa wafugaji wamekosa sehemu za kupeleka mifugo yao kwa ajili ya malisho na hivyo baadhi yake kufa.

“Hivi sasa wafugaji hawana chakula kwa ajili ya mifugo, walitegemea majani kipindi wakulima wanavuna lakini hakuna majani, wamebaki kuwatembeza wanyama porini na hakuna chakula, yalipokuwa mashamba pamegeuka kuwa ‘jangwa’ kutokana na mifugo kuswagwa kila siku,” anasema Aloyce.

Mkazi wa Kwakoa, Zumina Rajabu anasema wafugaji wameathirika na kwamba kila siku mifugo yao inakufa na iliyobakia imedhoofu kiasi cha kukosa soko.

“Upande wangu wameshakufa ng’ombe sita, hakuna malisho, mifugo waliobaki hawana thamani. Ng’ombe mkubwa wa Sh800,000 hadi Sh1 milioni sasa hivi ukimpata ananunua kwa Sh100,000 au Sh200,000. Ukipata mteja inabidi umuuze tu. Wengine wanakuwa wachungu kuuza bei hiyo na ng’ombe wao wanaishia kufa,” anasema Rajabu na kuongeza:

“Ukienda kwenye boma la mfugaji asubuhi lazima ukute ng’ombe zaidi ya watano ambao hawawezi kusimama wenyewe, wanasaidiwa kwa kunyanyuliwa. Mfugaji huyu anataka kula, pesa anazitoa wapi wakati mifugo imekonda mingine inakufa kwa njaa na hata mnadani haifai kupeleka?”

Diwani wa Toloha, Palesio Makange anaeleza kuwa kutokana na athari hizo, waliomba kupatiwa chakula cha msaada, lakini upatikanaji wake bado ni mgumu.

“Serikali imesema itatoa chakula kwa gharama nafuu lakini bado. Wapo wananchi ambao wanaishi kwa uji na matunda pori.

“Tumepewa taarifa kuwa mahindi ya msaada yatakayoletwa yatauzwa Sh885 kwa kilo. Tunaomba kutokana na hali ngumu ya wananchi wetu, bei ishushwe hadi Sh500 ili walau wote waweze kunufaika. Zipo kaya ambazo hata Sh300 hawawezi kuzipata kwa siku, hiyo 800 wataipataje ili waweze kununua kilo ya mahindi.”

Pamoja na hayo, Makange anasema chakula kinapatikana kwa wingi sokoni, lakini wanaomudu kwenda huko ni wachache kutokana na bei, akitolea mfano wa debe la mahindi ambalo anasema linauzwa Sh20,000.

Rombo

Hali si hali pia katika wilaya nyingine ya Mkoa wa Kilimanjaro. Hii ni Rombo na wenyeji wanasema, “haijawahi kutokea.”

Ukame katika wilaya hiyo umeathiri zaidi maneno ya ukanda wa chini (lower road). Kama ilivyo kwa Same na Mwanga, nako mifugo inakufa kwa kukosa malisho na baadhi ya familia zikihaha kusaka mlo.

Mwananchi ilitembelea baadhi ya maeneo ambayo yamekumbwa na ukame katika vijiji vya Usongo, Leto na Kingachi ambavyo vipo katika Kata ya Kingachi na vijiji vya Kiwanda na Kirongo Chini vilivyopo Kata ya Kirongo Samanga na kushuhudia baadhi ya mifugo ikifa kwa kukosa malisho.

Kadhalika, kama ilivyokuwa kwa baadhi ya familia za wilayani Same, mkazi wa Kijiji cha Usongo, Selina Alex anasema baada ya mumewe kuona njaa imezidi na mifugo yote imekufa kwa kukosa malisho, alikimbia nyumbani tangu Juni mwaka huu na hapatikani kwenye simu.

“Ukame kwangu ulianza tangu mwezi wa sita, nilikuwa na mahindi kidogo yakawa yameisha, maana hatujawahi kulima katika hiki kijiji tukavuna chochote kutokana na hali ya ukame. Nilikuwa na ng’ombe na mbuzi wote wamekufa, sasa mume wangu baada ya kuona hakuna chochote kilichobakia akaniambia ngoja niende kibaruani nikatafute, mpaka tunavyoongea leo aliondoka mwezi wa sita sijawahi kumwona na wala hapatikani kwenye simu.

“Mahindi yameisha, ngombe, mbuzi nao wamekufa, watoto nilionao sijui nawapa nini, kuna wakati natoka nyumbani kwenda kutafuta kibarua Kenya, fedha ninayopata ni Sh5,000, ukirudi nyumbani mafuta hakuna, unga hakuna. Hakuna chochote, ukiangalia mahindi kilo moja ni Sh1,200, kwa kweli maisha ni magumu mno na kadiri siku zinavyokwenda mambo yanakuwa mabaya zaidi.

“Kwa zaidi ya miaka miwili nimekuwa nikikodi mashamba na kulima, lakini hata siku moja sikuwahi kuvuna, mahindi yanakaukia shambani kwa kukosa mvua. Sasa hivi nimekata tamaa maana kila mwaka najaribu kulima naambulia patupu.

Sabina Mrema, mkazi wa Kijiji cha Usongo anasema kwa hali ilivyo sasa, imefika mahali hata akimwomba mume wake Sh100 za kununua maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani inakuwa ni ugomvi.

“Sasa hivi tuko kwenye hali mbaya na tunahofia hata watoto wetu, hatuna chochote, hapa tulipo maisha ni magumu, tunateseka sana jamani, hebu Serikali iangalie namna ya kuzinusuru familia zetu, maana huu mwaka ni mbaya haujawahi kutokea.

“Nilikuwa na ng’ombe wanne ambao walikuwa tegemeo kubwa kwetu, wote wamekufa kwa kukosa malisho na maji, sijui tutaishia wapi.”

Marietha Ladslausi, mkazi wa Kijiji cha Usongo anasema, “hapa tulikuwa na ng’ombe 19 na tayari 10 wameshakufa kwa kukosa majani na sasa hivi nimewachoma moto na kuwafukia maana sina jinsi ya kusaidia hawa mifugo na kila siku wanazidi kufa, sina chakula cha kuwalisha, majani hakuna, maji hakuna.”

Mwenyekiti wa kitongoji cha Ndameni Usongo, Venance Mrema anasema zaidi ya wanawake 30 wamefika nyumbani kwake wakilalamikia waume zao kuwakimbia kutokana na ugumu wa maisha.

“Watu wanakuja hapa nyumbani wanalia wanataka msaada wa chakula na mimi mwenyewe sina cha kuwapa watu wote, ukame umetuathiri, sasa nashindwa hata mimi kuwasaidia maana hali yangu nayo ni ngumu,” anasema.

“Kitongoji hiki kina shida kubwa ya njaa, huu ukame upo tangu mwaka 2019,” anaongeza.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Usongo, Dismass Kulwa anasema watu wa ukanda wa chini wameathirika zaidi, kwani kwa zaidi ya miaka mitatu hawajapata mavuno mazuri.

Maria Massawe, mkazi wa Kijiji cha Kiwanda, Kata ya Kirongo Samanga anasema hali ya ukame imewaathiri kiasi cha kushindwa kurejesha mikopo baada ya mifugo waliyoiwekea dhamana kufa kwa kukosa malisho.

“Kinamama ambao tunaishi ukanda wa chini tulikopa fedha tukaanzisha vikundi vitano, tulikuwa tumeshafikisha hisa zetu mpaka Sh1.8 milioni tukawa tunakopeshana wenyewe kwa wenyewe, lakini ukame ulivyoingia tulishindwa kulipa marejesho maana dhamana tulizowekea zile fedha ni ng’ombe na mbuzi, lakini kutokana na ukame baadhi wamekufa.”

Longido

Arusha ni mkoa mwingine ambao umekumbwa na hali ya ukame. Mwandishi wetu aliyetembelea Wilaya ya Longido anasimulia:

“Ni saa nane mchana, nafika kijiji cha Olbomba Wilaya ya Longido mkoani Arusha. Utulivu umetawala katika kijiji hiki, wanaonekana watoto wadogo tu wakicheza na pembezoni wanawake wakiwa chini ya miti wamekaa.

Sioni wanaume na vijana wa kiume, baadaye napewa taarifa kwamba wengi wameondoka kwenda kusaka malisho ya mifugo nje ya wilaya na nchi jirani na wengine wamekwenda kutafuta chakula cha familia.

Sura za wakazi wengi wa kijiji hiki hazina matumaini ya kesho, hii ni kutokana na ukame unaoendelea ambao umeripotiwa kusababisha vifo vya mifugo, pia wao kukosa chakula.

Nafika katika famila ya Ole Mwato, nakuta watoto wadogo sita wakisubiri uji ambao inaelezwa kuwa ndicho chakula cha mchana.

Mama wa familia hii, Senewa Ole Mwato ndiye anayewajibika kuwalea watoto wake sita baada ya mumewe kufariki dunia miaka saba iliyopita.

Anasema kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa familia yake inaishi kwa kula mlo mmoja kwa siku na amekuwa akiishi kwa msaada wa chakula kutoka kwa jamaa na marafiki.

Anasema wanakunywa uji saa nane mchana na usiku wanakula ugali hadi siku ya pili, wanafanya hivyo kwa kuwa hana akiba ya chakula.

“Siku nyingine watoto wanakunywa uji tu na kulala. Hali ni mbaya sana kwani hali ikiendelea kuwa hivi familia inaweza kupata madhara makubwa,” anasema.

Anasema mtoto mmoja anaumwa ugonjwa ambao anauhusisha na kutopata chakula cha kutosha.

Anasema alikuwa na ng’ombe wanne alioachiwa na mumewe lakini wote wamekufa kwa kukosa maji na malisho.

Yayaa Leyo, binti wa miaka 17 ambaye ameolewa na Leyo ole Mwato akiwa na mtoto mchanga, namkuta jikoni akipika uji, anasema hicho ndicho chakula chao siku hizi, anaiomba Serikali kuwasaidia chakula la sivyo watakufa kwa njaa.

“Tuna hali ngumu ya maisha, hatuna chakula, mifugo inakufa tunaomba Serikali itupatie chakula,” anasema.

Safari ya mwandishi wa Mwananchi inamfikisha katika familia nyingine, namkuta mwanamke pekee, Korengera Lekepa, mkazi wa Kijiji cha Olbomba ambaye anasema anaishi na watoto wanne, huku simulizi yake pia ikiwa ni njaa na vifo vya mifugo.

Katika familia hii namkuta mtoto mmoja akinywa uji wakati huo ikiwa majira ya saa 8 mchana.

“Tuna shida kubwa ya chakula, hata watoto wanaanza kushindwa kwenda shule kusoma kutokana na njaa,” anasema.

Anasema mumewe, Lekepa Laizer aliondoka kijiji kwenda eneo la Ngarenanyuki wilaya ya Arumeru, kwa ndugu zake kutafuta chakula. “Ana miezi mitatu sasa hajarudi, aliondoka baada ya kuanza kuona ng’ombe na mbuzi wanakufa na hawana chakula.

“Tunaomba msaada kwa Serikali tupate chakula, kwani hawa watoto wadogo wanapata shida sana pamoja na wanafunzi,” anasema Lekepa.

“Hali ya ukame katika wilaya hiyo ni mbaya na sikumbuki kuwahi kuona ukame kama huu,” anaongeza.

Katika boma la Lekitonyi, namkuta ng’ombe ambaye ameshindwa kusimama kutokana na njaa.

Lekepa amemkatia tamaa ng’ombe huyo, anasema hawezi kuendelea kuwa hai bali atakufa kama wengine. Walikuwa na ng’ombe 20 kati yao 14 wamekufa na mbuzi wote 15 wamekufa pia.

Mtoto wa Lekepa, Ndeye Lekitonyi (13) anasema ameshindwa kwenda shule kwa kuwa ana kazi ya kutafuta chakula cha wadogo zake na mifugo.

Anasema hivi sasa mifugo inategemea pumba wanazonunua kwenye mashine.

Habari ya upungufu wa chakula pia naikuta katika familia ya Amos Lemomo, baba mwenye wake wawili wanaoishi nyumba moja.

Mke mkubwa, Grace Amos anasema hali ni mbaya, hawana chakula na kwamba hata bei ya mifugo imeporomoka.

Anasema wanategemea akiba ndogo ya chakula kilichobaki na hivyo kulazimika kula mlo mmoja ili kisiishe mapema.

Mke mdogo, Leteli Amos anashindwa kujieleza kutokana na hali ngumu wanayokabiliana nayo. Amos Lemomo, mume wa wake hao wawili anasema hawajawahi kuona ukame mkali kama huo, akisema hata ule wa mwaka 2018 haufui dafu.

Anasema hawana elimu nyingine zaidi ya ufugaji hivyo kuiomba Serikali kuwasaidia kupata chakula na malisho ya mifugo.

“Hatuna tunachotegemea zaidi ya mifugo, sasa hivi inakufa na hata tukienda kuuza bei imeshuka sana na hakuna wanunuzi,” anasema.

Mchungaji wa Kanisa na Baptist, Musa Murdoko anasema ukame unaotokana na mabadiliko ya tabianchi umekuwa na athari kubwa na Serikali isipoingilia kati hali itakuwa mbaya zaidi.

“Hivi sasa bei ya mifugo imeshuka sana. Ng’ombe ambaye alikuwa anauzwa kati ya 800,000 hadi 500,000 hivi sasa anauzwa kati ya 200,000 hadi 300,000,” anasema.

“Wananchi hawana chakula, maji wala maziwa, Serikali inapaswa kutusaidia,” anasema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Olbomba, Kashilo Alais anasema ukame umekuwa na athari kubwa na kama hatua za haraka zisipochukuliwa kunaweza kutokea maafa.

“Gunia la mahindi wanauza Sh80,000 lakini wananchi wengi hawana uwezo kununua, kwani bei ya mifugo imeporomoka sana,” anasema.

Gairo

Athari hizo pia zinaonekana katika Kijiji cha Kwipipa wilayani Gairo, ambapo Regina Bisoweto, mmoja wa wakazi anasema ukame huo umekwamisha shughuli zake za kilimo cha mbogamboga kilichokuwa msingi wa mahitaji ya familia yake.

Anasema wanachukua mikopo kwenye vikundi vya kuwawezesha wanawake kulima kilimo hicho, lakini mwaka huu hana uhakika wa kurejesha, kwani bustani inakauka.

“Nilichukua mkopo wa Sh50,000 kwenye Vicoba kwa ajili ya kulima mbogamboga ambazo huwa nauza napata fedha ya kurejesha deni na chakula kwa familia, lakini mwaka huu mboga zimekauka,” anasema.

Hali imekuwa mbaya zaidi kutokana na kile alichoeleza kuwa, bwawa walilokuwa wanatumia kwa ajili ya kumwagilia limekauka, “tunachofanya hapa kwenye bwawa tunakuja asubuhi sana utakuta maji kidogo ndiyo hayohayo tunamwagilia, lakini hayatoshi, ukimtuma mtoto hawezi kupata maji,” anasema.

Mwenyekiti Kitongoji cha Mkokani, Kata ya Kwipipa, Dickson Mligita anasema ukilinganisha na miaka mingine katika eneo hilo, mwaka huu mvua zilinyesha kuanzia Januari hadi Machi, kipindi ambacho ndio kwanza mazao yalitarajiwa kukomaa, hivyo kuathiri ustawi wake.

“Kwa miaka yote mvua za vuli huwa zinaanza Oktoba, lakini kwa msimu uliopita zilianza Januari zikaisha Machi, mazao hayakuwa yamekomaa, kwa hiyo mahindi na mtama yalikauka, tulipata mavuno kidogo,” anasema.

Mtama, mahindi na alizeti, ndiyo mazao yanayolimwa zaidi katika eneo hilo na kutokana na hali ya hewa sasa uzalishaji umepunguza kutoka magunia 10 ya mahindi kwa ekari hadi mawili au matatu.

Anasema kilimo pekee kinachotegemewa na wengi katika eneo hilo ni alizeti kwa kuwa inastahimili ukame, lakini si ulezi kutokana na hali iliyopo sasa.

Ugumu wa maisha unaosababishwa na hali hiyo, anasema umewahamisha vijana wengi kutoka wilaya hiyo kwenda maeneo yenye afadhali, ikiwamo Kiteto na Kilindi kwa ajili ya kilimo na ufugaji, “angalau huko kuna mapori ya kilimo, malisho ya mifugo, kijana aliyebaki hapa labda wa bodaboda.”

Kutokana na kuporomoja bei ya mifugo, bei ya nyama pia imeshuka kutokana na idadi kubwa ya mifugo kuchinjwa baada ya kukosa malisho na kudhoofu, huku upatikanaji wa maziwa ukiwa mgumu.

Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Jabir Makame anasema licha ya kukosekana kwa mvua za kutosha, hata vyanzo vya maji, zikiwamo chemchemi, vimetoweka.

Hali hiyo, anasema imesababishwa na wananchi kufanya shughuli za kilimo na kupitisha mifugo kwenye vyanzo vya maji na hivyo kuviathiri.

“Kwa sehemu kubwa watu wanalima karibu na vyanzo vya maji na wafugaji wanapitisha mifugo yao humo, hii imefanya vyanzo vingine vya maji visivyotegemea mvua kutoweka,” anasema.

Makame anasema msimu wa mwaka jana haukuwa na mvua za kutosha, hivyo kusababisha mavuno machache na kuathiri biashara ya mazao pekee na vyakula.

Kilosa

Kilichotokea Gairo hakitofautiani sana na Kilosa, ambako kilimo na mifugo vimeathiriwa pakubwa.

Katika mazungumzo yake na Mwananchi, mkulima katika Kata ya Magole wilayani Kilosa, Mwajuma Hamad anasema ukame umeibua magonjwa ya mazao.

“Shamba langu lina ekari tatu, nimelima lote lakini kwa mahindi napata magunia saba kwa shamba lote, zamani nilikuwa napata hadi magunia 30,” anasema.

Anasema akikwama katika mazao ya chakula anahamia kwenye bustani ya mbogamboga, lakini kwa sasa “hazistawi kwa sababu hakuna mvua,” anasema.

Magonjwa ya mifugo, ikiwemo homa ya mapafu ni changamoto nyingine aliyosema wanakabiliana nayo kutokana na hali hiyo.

Akizungumzia athari katika sekta ya kilimo na mifugo, Ofisa Kilimo na Mifugo wilayani Kilosa, Elina Dunstan alisema kukauka kwa vyanzo vya maji ni athari mojawapo, kwani wakulima wanashindwa kufanya kilimo cha umwagiliaji na bustani.

“Hii inawafanya wauze vyakula walivyonavyo ili wapate fedha za kumudu huduma nyingine, lakini kungekuwa na bustani wangekuwa wanauza mboga,” anasema.


Imeandikwa na Florah Temba, Maryasumpta Ausebi, Janet Joseph (Kilimanjaro), Mussa Juma (Arusha), Juma Issihaka (Moro), Raisa Said na Burhani Yakub (Tanga).