Ukawa waanza mapambano nje ya Bunge
Mjumbe wa Bunge la Katiba wa kundi la Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (Ukawa), Ismail Jussa akionyesha moja ya nukuu za kitabu cha Profesa Issa Shivji wakati wa mkutano na waandishi Dodoma jana. Kushoto ni mjumbe mwenzake, Tundu Lissu. Picha na Salima Shao
Muktasari:
Akizungumzia hotuba hiyo, Jussa aliyeweka wazi masilahi yake kuwa ni mwanafunzi wa Profesa Shivji, alisema msomi huyo aliyekuwa tegemeo la wanyonge, alifanya upotoshaji mkubwa ambao umetoa vitisho kwa wananchi.
Dar /Dodoma/Mwanza. Ni dhahiri kwamba mjadala wa msomi wa Sheria, Profesa Issa Shivji umewavuruga wanasiasa waumini wa serikali mbili ambao baadhi yao jana walimshukia wakidai kuwa “mzee huyu ni ndumila kuwili na kigeugeu.”
Shivji juzi alitoa mjadala kuhusu muundo wa Muungano na kuishutumu Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyopendekeza serikali tatu, kuwa ilipotosha maoni ya wananchi. Alipotakiwa kuzungumzia madai dhidi yake, Profesa Shivji alisema: “Nyie ni waandishi wa habari someni, angalieni wapi mimi nilisema Serikali tatu, wanaosema ninatumiwa na CCM hayo ni maoni yao siwakatazi kuzungumza wanachofikiria.”
Jana Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika kampeni yake nje ya Bunge la Katiba, ulimtaka Profesa Shivji kuwaomba radhi wananchi kwa kile wanachodai kwamba amekuwa kigeugeu kwenye maandishi na matamshi yake kuhusu muundo wa Muungano.
Katika mkutano wake wa kuelimisha wananchi kuhusu Katiba Mpya mjini Mwanza uliojaa polisi kila kona, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa alisema wanamshangaa Profesa Shivji kwa mawazo yake yasiyoeleweka kuhusu muundo wa Muungano.
“Kwa kweli tunaamini watu ambao ni wasomi kama Profesa Shivji wanaweza kuwasaidia wananchi kupata katiba nzuri, lakini anachokifanya sasa ni siasa, jambo ambalo siyo jema,” alisema Dk. Slaa na kuongeza:
“Ukawa tunamtaka awaombe radhi wananchi, kwani amewadhalilisha kwa kuwa kigeugeu. Mara ya kwanza tunakumbuka alikuwa muumini wa Serikali tatu leo anageuka na kuanza kuhubiri serikali mbili, huu ni upuuzi kwa msomi kama yeye kufanya hivyo.”
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema CCM wanaogopa Rasimu ya Katiba kwa sababu wamezoea uchakachuaji.
Naye Kaimu Katibu Mkuu wa CUF, Abdulkarim Kambaya alisema Rais Kikwete amewachezea akili wananchi, kwani awali alikuwa anaonyesha yupo upande wao lakini kupitia hotuba yake bungeni amewakana na kuibeba CCM.
Lissu, Jussa nao wanena
Pia baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) jana walimshambulia kwa maneno Profesa Isa Shivji kuwa ni ‘ndumilakuwili’.
Kwa nyakati tofauti, wajumbe Tundu Lissu na Ismail Jussa walisema kuwa Profesa Shivji “alibebwa na CCM na kulishwa maneno kwa masilahi ambayo hayajulikani.”
Akizungumzia hotuba hiyo, Jussa aliyeweka wazi masilahi yake kuwa ni mwanafunzi wa Profesa Shivji, alisema msomi huyo aliyekuwa tegemeo la wanyonge, alifanya upotoshaji mkubwa ambao umetoa vitisho kwa wananchi.
Akitolea mfano wa maandiko mbalimbali ya Shivji, Jussa alisema kila wakati msomi huyo alikuwa ni dira na kioo cha kusema kweli kama msomi.
“Hivi sasa anatumika na upande wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi, ndiyo maana hata katika hotuba yake alitumika moja kwa moja kutukana watu na kudhalilisha watu,” alisema Jussa.
“Kama amechoka basi akapumzike nyumbani kwani kitendo cha kutumika kila mahali na kuwadhalilisha watu wenye heshima, anaonekana hafai tena na hana heshima mbele ya jamii,” alisema Jussa.
Alisema katika maandiko yake Profesa Shivji alisema amekuwa akisifia suala la mfumo wa Muungano wa Serikali tatu ambao ndiyo uliokuwa umependekezwa na wasomi wengi katika tume zilizotangulia.
Alinukuu moja ya vitabu vya Profesa Shivji cha Pan-Africanism or Pragmatism, kwamba kilijaa ukweli na tuhuma za kuwa hata waasisi wa Muungano huo walikufa wakiwa hawaongei, lakini hakuna aliyehoji kwamba amechochea.
Alisema katika kitabu hicho alionyesha kuwa Mwalimu Nyerere alitumikia masilahi ya Waingereza na kusababisha wagombane na Karume na hata walipotaka kuzungumza waliwatumia Bhoke Munanka kwa upande wa Tanganyika na Abdul Jumbe kwa upande wa Zanzibar.
Lissu alisema hakuna mtu ambaye amewaelimisha wananchi kuhusu Muungano kama Profesa Shivji lakini msimamo wake juu ya Tume ya Warioba umekuwa kigeugeu ukikinzana na maandiko yake na tume alizowahi kuzisifia hapo awali.
“Msomi yule ambaye mwanzoni mimi nilikuwa ni mtoto wake nikijifunza zaidi mambo yake, leo ni miaka 30 ameanza kuyakana, huu ni usanii kwa mtu mwenye heshima kama yule,” alisema Lissu.
Lissu alinukuu kitabu kingine cha Shivji cha Tanzania The Legal Foundation of Union, akieleza namna ambavyo Muungano ulikuwa batili na kutuhumu Tanzania Bara iliikandamiza Zanzibar.
Majibu ya Shivji
Akizungumza na gazeti hili jana, Profesa Shivji alisema kwamba uchambuzi alioutoa ni wa kisomi na anauamini na hivyo hawezi kulumbana na watu wanaompinga.
“Kama mnataka uchambuzi ule nitawatumia ili muuchapishe kwa faida ya wananchi lakini siwezi kulumbana na mtu mwenye mawazo tofauti,” alisema Profesa Shivji.
Imeandikwa na Raymond Kaminyoge, Aidan Mhando na Habel Chidawal