Ukilima vanila, unapata hadi Sh850,000 kwa kilo
Muktasari:
- Watanzania wanaofikiria kuwa mamilionea kupitia kilimo, wanaweza kujaribu bahati kwa kujihusisha na uzalishaji wa vanila.
Watanzania wanaofikiria kuwa mamilionea kupitia kilimo, wanaweza kujaribu bahati kwa kujihusisha na uzalishaji wa vanila.
Zao la vanila ni sehemu ya mazao ya viungo kama iliki, mdalasini, vitunguu saumu na tangawizi; huuzwa kwa bei ya juu ndani na nje ya nchi.
Japokuwa limeanza kuchangamkiwa na wakulima wachache nchini, lakini lina bei nzuri ikilinganishwa na mazao mengine.
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2018, Mexico, Madagascar, Indonesia, Uganda, Comoro na Papua New Guinea, ndio waagizaji wakuu wa vanila kutoka Tanzania.
Mtaalamu wa uchumi wa kilimo wa Chama cha Wakulima wa Mbogamboga na Maua Tanzania (Taha) kutoka Zanzibar, Ally Kamtande Ally alisema mwaka 2020 vanila safi iliuzwa kwa Sh850,000 kwa kilo.
“Kutokana na athari za Uviko-19, bei zimepungua hadi Sh450,000 kwa kilo ambazo zimesusiwa na wakulima. Sasa wameiomba Taha itafute mnunuzi mwingine,” alisema Ally.
Hata hivyo, alisema zao hilo lina fursa kubwa kwa Watanzania kutengeneza fedha ikilinganishwa na mazao mengine, huku akihimiza ushirikishwaji wa wananchi katika zao hilo.
Uzalishaji wa vanila, uuzaji nje na mapato nchini unaonyesha kuwa kati ya mwaka 2006 na 2015, wakulima walipata karibu Sh2 bilioni kutokana na mauzo ya nje, huku Chama cha Ushirika kinachoshughulika na uzalishaji wa mazao cha Mayawa, kikisafirisha tani 14.3 za vanila iliyotiwa chachu yenye thamani ya Sh39.7 milioni.
Mwaka 2007, tani 32.1 zilisafirishwa nje na kuwapatia wakulima Sh49.5 milioni na pia tani 47.1 zilisafirishwa nje mwaka 2008 na kuzalisha Sh128.8 milioni.
Pia, mwaka 2009 tani 75.6 zilisafirishwa nje na kutengeneza Sh244.6 milioni, wakati mwaka 2010 tani 102 zilisafirishwa na kuwapatia wakulima Sh319 milioni.
Mayawa ilisafirisha tani 70.8 mwaka 2011 na kupata Sh229.4 milioni wakati tani 35.8 ziliuzwa mwaka 2012 zenye thamani ya Sh147.9 milioni.
Mwaka 2013 na 2014; tani 39.2 na tani 27 za vanila zilisafirishwa nje na kuzalisha Sh215.4 milioni.
Mwaka 2015, tani 33.9 za vanilla iliyochachushwa zilisafirishwa nje na kuingiza Sh406.8 milioni. Hata hivyo, uzalishaji wa vanilla nchini umepungua miaka ya hivi karibuni kutokana na ugonjwa wa mnyauko wa migomba ambayo hutoa kivuli, hasa Mkoa wa Kagera.
Ugonjwa huo ulisababisha kung’olewa kwa migomba na kuifanya vanilla isistawi kwa kukosekana kwa vivuli vya kutosha.
Hata hivyo, wakulima wa Tanzania wanaoshiriki katika uzalishaji wa vanilla wanaweza kuongeza vipato vyao kutokana na zao hilo kuwa na bei nzuri.
Daud Mbongo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari-Uyole) anasema ingawa kufanikiwa kwa chochote kunategemea juhudi za mtu binafsi, Watanzania wanapaswa kujaribu uzalishaji wa vanila.
“Wale watakaoitumia fursa sasa ndani na ulimwenguni, watakuwa katika nafasi nzuri ya kufaulu, kwa sababu vanila ina soko,” anasema.
Mbongo anasema mti mmoja wa vanila unaweza kutoa kilo tatu hadi tano baada ya miaka minne hadi minane na kwamba wakulima wanaweza kuendelea kuvuna kwa miezi miwili mfululizo. Hata hivyo, anasema ni kiasi kidogo tu cha matunda kitakachovunwa kila siku katika miezi miwili.
Pia, anasema miti ya vanila inaweza kutoa mavuno hata baada ya miaka 17 hadi 18, ingawa wingi unaweza kupungua kadri inavyozeeka.
Hali ya hewa
Mbongo anasema vanila hupandwa katika maeneo yenye joto kati ya sentigredi 20 hadi 30 na urefu chini ya mita 1,500 juu ya usawa wa bahari.
Anasema zao hilo linahitaji wastani wa mvua kati ya milimita 1,200 hadi milimita 2,500 kwa mwaka.
Hapa nchini vanila inaweza kupandwa kaskazini magharibi karibu na Ziwa Victoria mkoani Kagera, Kilimanjaro kaskazini na mashariki mwa Morogoro.
Zao hilo pia linaweza kupandwa wilaya za Muheza mkoani Tanga, Ukerewe (Mwanza) pamoja na Rungwe, Ileje, Kyela na Mbeya Vijijini Mkoa wa Mbeya.
Kilimo cha mazao
Mbongo anasema vanila ni zao la vimelea ambalo hustawi katika ardhi yenye rutuba ambayo haihifadhi maji.
“Zao hilo linahitaji miti ya kuisaidia ambayo baadaye hutumika kusambaza chakula kwenye miti ya vanila. Mbegu au shina linapaswa kupandwa katika nafasi ya sentimita 1.5 hadi sentimita mbili. Nafasi inayopendekezwa kati ya mistari iko kati ya sentimita 2.5 hadi sentimita 3,” alisema.
Wadudu na magonjwa
Mtaalamu huyo anasema jongoo na viwavi ni miongoni mwa wadudu waharibifu katika miti ya vanila ambayo kawaida hudhibitiwa kwa kuuawa.
“Konokono wanaoacha alama juu ya zao husababisha kukwama kwa miti ya vanila. Wakulima wanashauriwa kufanya ukaguzi wa shamba mara kwa mara na kuwaangamiza wadudu,” anasema huku akibainisha kuwa konokono pia wanaweza kudhibitiwa kupitia matumizi ya chumvi.
Mbongo anasema kuoza kwa mizizi, antracnose na ukungu ni magonjwa matatu ya kawaida yanayoathiri vanila, akidokeza kuwa magonjwa mawili ya kwanza yanaweza kudhibitiwa kwa kuzuia kutuama kwa maji shambani.
“Hatua hiyo itazuia mizizi kuoza na kuharibu shina. Mazao yanapaswa pia kunyunyiziwa dawa za ukungu ili kudhibiti maambukizi,” anasema.
Pia, anasema kukata matawi ya miti ili kuongeza mzunguko wa hewa kwenye miti ya vanila na kuzuia msongamano wa shamba kunaweza kudhibiti kwa kasi ukungu.
Anasema dawa za ukungu zinazopatikana sokoni kama vile “ivory” na “victory” zinaweza kupuliziwa ili kudhibiti kabisa magonjwa.
Maua na uchavushaji
Mbongo anasema hapa nchini vanila huchavushwa kwa mikono na wakulima wanatakiwa kutumia zana kali kama sindano.
“Baadhi ya nchi za Amerika ya kusini na kati zimebarikiwa kuwa na nyuki wanaosaidia uchavushaji. Hata hivyo, nyuki hao hawapatikani Tanzania na nchi nyingine nyingi,” anasema Mbongo.