Ukweli kuhusu mradi wa maji Arusha

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mbunge wa Viti Maalum Arusha Mhe. Catherine Magige

Muktasari:

  • Rais John Magufuli leo Jumapili Desemba 2, 2018 amezindua mradi wa maji mjini Arusha ambao pamoja na mambo mengine unatajwa kuwa utapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la maji jijini humo

Arumeru. Rais John Magufuli ameweka jiwe la msingi katika mradi mkubwa wa maji safi na mazingira katika jiji la Arusha ambako vitachimbwa visima 56 vitakavyokuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni mbili kwa siku.

Akizungumza leo Jumapili Desemba 2, 2018 baada ya kuweka jiwe la msingi katika moja ya visima virefu katika kijiji cha Kimnyaki, Rais Magufuli ameeleza kuridhishwa na mradi huo ambao utamaliza tatizo la maji katika Jiji la Arusha na baadhi ya maeneo wilaya ya Arumeru.

“Ninawapongeza sana sana kwa mradi huu Mungu awabariki sana,” amesema.

Awali mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Mazingira  Arusha (AUWSA), Luth Koya amesema katika mradi huo visima 56 vitachimbwa ili kusambaza maji.

Amesema visima hivyo vinaweza kuzalisha lita milioni mbili kwa siku ambavyo vitaweza kumaliza  tatizo ya maji jijini humo ambalo mahitaji yake ni lita 940,000 kwa siku.

Amesema kisima ambacho kimewekewa jiwe la msingi katika  kijiji cha Kimnyaki  kina uwezo wa kutoa  lita 400,000 za maji kwa saa lakini  zitakuwa zikichukuliwa lita 300,000 kwa saa.

Amesema mradi huo wa Sh520 bilioni unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Mandeleo ya Afrika.