Ulega ataka taa za barabarani zibadilishwe, Dk Mwigulu na Makonda wasema…
Muktasari:
- Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), ameagizwa kuondoa taa za barabarani zinazotumia umeme badala yake iweke zinazotumia mfumo wa sola, ili kuondokana adha ya barabara kuwa giza baada ya kutokea hitilafu ya umeme.
Arusha. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameaigiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kuondoa taa za barabarani zinazotumia umeme, badala yake ifunge zinazotumia sola ili kuleta unafuu kwa watumiaji wa barabara hizo, hususan katika miji mikubwa.
Amesema taa zinazotumia umeme zimekuwa zikisababisha adha ya giza barabarani pindi nishati hiyo inapopata hililafu au kukatika ghafla, lakini zikitumia sola kuna uhakika zaidi.
Miongoni mwa athari zinazojitokeza kwa taa kutofanya kazi ni pamoja na ajali, wananchi kuporwa mali zao, pia inaathiri shughuli za kiuchumi.
Waziri Ulega ametoa agizo hilo leo Jumatatu, Januari 6, 2025 alipozungumza katika kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Arusha kilichohudhuriwa na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, mkuu wa mkoa huo, Paul Makonda, wenyeviti na wakurugenzi wa halmashauri na wabunge wa mkoa huo.
"Maelekezo yangu leo taa zote zinazotumia umeme wa Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) zibadilishwe haraka na kuwa za taa zinazotumia mfumo wa sola. Tuweke teknolojia nyepesi itakayotusaidia wakati wote.
"Ni aibu kubwa tumenunua taa kwenye miji mikubwa kama Dar es Salaam, unapita unaona nguzo za taa zipo pale lakini hazifanyika kazi, maana fedha za wananchi zimepotea bure ukiuliza unaambiwa hitilafu ya umeme au umekatika badilisheni haraka sana," amesema Ulega.
Waziri Ulega pia amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Balozi Aisha Amour kulifanyia kazi kwa uharaka kwa kubadilisha mfumo wa Tanesco na kuweka sola ili kuwepo na mwanga wakati wote kwenye barabara.
"Nimemsikia mkuu wa mkoa (Makonda) anasema hitilafu kidogo ya umeme basi taa hazifanyi kazi, sasa watalaamu mpo na mna uwezo. Unakuta miji ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya kuna giza," amesema Ulega.
Mbali na hilo, Ulega ameitaka Tanroads kushirikiana na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) kuhakikisha miji inakuwa na taa, akisema taasisi hizo ni kitu kimoja katika kuleta maendeleo kwa Watanzania.
Alichokisema Dk Mwigulu
Katika kikao hicho, Dk Mwigulu amesema barabara ni kiungo muhimu kwa uchumi ndiyo maana kwa Mkoa wa Arusha watatupia jicho kutokana na umuhimu wake, hususan kutokana na utalii.
Kwa mujibu wa Dk Mwigulu, kasi ya ujenzi wa barabara ilipungua ili kupisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo wa mradi wa bwawa la Mwalimu Nyerere na ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR.
"Ni kweli hapa katikati mtiritiko ulipungua kidogo lakini haikuwa bahati mbaya, tuliweka uamuzi wa makusudi ndani wa kuhakikisha aina fulani ya miradi inayoleta kero kwenye Taifa ambayo ilikuwa mbioni kukamilika, tukasema tujifinye tuimalize kisha turejee katika utaratibu wa kawaida.
"Sasa baada ya miradi hii kuanza kazi, kuanzia sasa mtiririko wa fedha tutaongeza kasi kwa sababu tunatambua kazi yenu (miundombinu) ni kiungo muhimu. Tutabadilisha mtiririko wa fedha ili kupeleka kwenye maeneo yenye miradi ikamilike," amesema Dk Mwigulu.
Makonda
Awali, Makonda alimweleza Ulega kuwa Mkoa wa Arusha kwenye suala la barabara imesahaulika, akisema jambo ambalo ni changamoto katika jiji linalosifika kwa utalii na ndiyo makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
"Tunaomba mtuangalie kwa jicho la pili kuhusu miundombinu ya mkoa huu, hasa barabara. Nina orodha ya barabara hapa ambazo zikijengwa kwa kiwango cha lami zitaleta ahueni kuboresha mandhari ya mji wetu.
"Kuna barabara kutoka Longido kwenda hadi Siha (Kilimanjaro) ina kilomita 55 ikijengwa itafungua milango ya utalii kwa kuwezesha watu wanaotoka nchi jirani ambao hawatalazimika kupita katikati ya mji," amesema Makonda.
Hata hivyo, Dk Mwigulu alimuhakikishia Makonda kuwa wataziweka barabara hizo kwenye vipaumbele ili zitekelezwe, huku Waziri Ulega akisema wamechukua maombi ya mkuu huyo wa mkoa na watayafanyia kazi.
Katika hatua nyingine, Makonda amesema wanahitaji taa za barabarani, akisema kuna barabara ya kilomita 14 imejengwa na kuwekewa taa za umeme, lakini ikitokea hitilafu hazifanyi kazi.
"Jambo jingine gharama zake za kuziendesha hizo taa lazima Tanroads walipe ankara, maombi yetu hizo taa ziwekwe za sola ili kuondokana gharama za uendeshaji na hitilafu zinazosababisha taa kuzima," amesema Makonda.