Ulega: Serikali imeifungua Kigoma kwa miundombinu, uchumi
Muktasari:
- Ulega ameeleza hayo wakati akizungumza katika mikutano ya hadhara aliyoifanya kwa nyakati tofauti akiwa ziarani mkoani humo.
Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema miaka mitano ya Serikali ya awamu ya sita, imewezesha kuufungua Mkoa wa Kigoma kwa kuhakikisha unapitika kiurahisi na kufungua fursa za kiuchumi.
Kwa mujibu wa Ulega, miongoni mwa mambo yaliyochagiza hatua hiyo ni utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo miundombinu ya mtandao wa barabara wa lami unaounganisha Kigoma na mikoa mingine na nchi za jirani.
Ulega ameeleza hayo jana Julai 21, 2026 alipokuwa akizungumza katika mikutano ya hadhara aliyoifanya kwa nyakati tofauti akiwa ziarani mkoani humo. Amesema Kigoma ya sasa ni tofauti na ile ilivyokuwa wakati Rais Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani mwaka 2021.
Amesema kwa miaka 60 ya Uhuru mtandao wa barabara za lami Kigoma ulikuwa na kilomita 259 za lami, lakini Serikali ya awamu ya sita imejenga kilomita 335.
“Hii maana yake ni kwamba kwa miaka mitano tu, Serikali ya awamu ya sita imejenga kilomita za lami ambazo ni zaidi ya kilomita zilizokuwepo kabla yake kwa miaka 60.
“Matokeo yake leo Kigoma ina mtandao wa barabara za lami wenye urefu wa kilomita 594 ambayo ni ongezeko la zaidi ya asilimia 100 ya kiwango kilichokuwepo zamani,” amesema Ulega.
Katika ziara hiyo, Ulega alifanya ukaguzi wa takribani wilaya nne tofauti za mkoa huo, ambapo wabunge na wananchi wa mkoa huo walitoa maoni yao kuhusu utofauti na mabadiliko hayo.
Akiwa wilayani Kasulu, Ulega amesema Serikali imetumia zaidi ya Sh600 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya kimkakati tisa katika Mkoa wa Kigoma peke yake.
“Kinachoendelea Kigoma ndio taswira pia ya maendeleo makubwa ya ujenzi yanayoendelea katika mikoa tofauti nchini Tanzania kwa sababu Rais Samia anaamini barabara ni mlango wa fursa kwa walio wengi.”
Pia, akiwa Kigoma Vijijini, Ulega alipita katika barabara ya urefu wa kilomita 65 ya Mkongoro – Chankere – Mwamgongo – Kagunga ya Chankere inayopita kwenye njia ya Bonde la Ufa la Afrika Mashariki na iliyohitaji utaalamu na gharama kubwa kuijenga.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chiponda, maarufu Baba Levo amesema zamani nauli ya kutoka Kigoma kwenda Dar es Salaam ilikuwa Sh120,000 lakini baada ya barabara kuimarika, hivi sasa nauli imekuwa Sh70,000.
“Muda wa safari umepungua kwa takribani saa nane, kutoka kuwa safari ya siku nzima sawa na saa 24, na kuwa saa 16.”
“Haya mambo ukiwa mtu unaishi Sinza au Kinondoni ni rahisi kudanganywa kwamba hakuna kitu kinafanyika hapa nchini. Ila watuulize sisi tuwaambie kuhusu makubwa yanayoendelea Kigoma na kwingine,” amesema Baba Levo.
Akizungumza katika ziara hiyo ya Ulega, Mayeye amesema kazi ya kuufungua mkoa wa Kigoma inapaswa kuendelea kwa sababu mkoa huo ni miongoni mwa milango muhimu ya uchumi wa Tanzania.
Mbunge huyo, ambaye anaingia bungeni kwa mara ya pili, pia alizungumzia kuhusu namna usafiri ulivyorejesha utu kwa wananchi.
“Zamani ilikuwa inachukua kati ya siku nne hadi wiki moja kusafiri kutoka Kasulu hadi Manyovu ambako ni mpakani kwenda Burundi.”
“Sasa hivi safari hiyo inachukua saa kadhaa tu. Tumerahisisha maisha ya watu na biashara,” amesema Mayeye.