Umeme watajwa kumaliza uhaba wa sukari Tanzania

Saturday September 04 2021
sukaripicc
By Sharon Sauwa

Dodoma. Serikali imesema sukari ipo ya kutosha nchini na kukamilika kwa mradi mkubwa wa  umeme wa Mwalimu Julius Nyerere utasaidia bei ya bidhaa hiyo kupungua kuliko ilivyo sasa.

Hayo yamesemwa na msemaji mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa leo Jumamosi Septemba 4, 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema nchi hupata upungufu wa sukari kati ya mwezi Aprili hadi Juni sababu ikiwa ni viwanda kutozalisha kutokana na  miwa inayovunwa kutoa kiwango kidogo cha sukari.

Msigwa amesema uzalishaji wa sukari ni wastani wa tani 367,000  kwa mwaka huku mahitaji yakiwa tani 420,000 kwa mwaka.

Amesema  kuna upungufu wa kati ya tani 40,000 hadi 50,000 na Serikali iliamua kuweka utaratibu wa kutoa vibali vya kuagiza sukari inayopungua kwa viwanda vinavyozalisha sukari nchini.

“Hii imekuwa ikifanyika vizuri, wafanyabiashara wanaendelea kuleta lakini kumekuwa na baadhi ya wafanyabiashara wanataka kulazimisha kuleta sukari nje ya utaratibu huu."

Advertisement

"Kwa nia njema Serikali iliamua hawa  wabebe jukumu,   zoezi hili linakwenda vizuri na  wanaojaribu kwa maslahi yao Serikali iko macho na inafuatilia,” amesema.

Amefafanua Serikali inachukua hatua hizo kwa sababu ya kuhakikisha  Watanzania wanapata sukari kwa bei nzuri.

Hata hivyo, amesema pamoja na kuongeza uzalishaji wa sukari utakaowezesha  baada ya miaka mitatu kuwa na uzalishaji wa sukari zaidi ya tani 670,000, Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha  Watanzania wanapata bidhaa hiyo kwa gharama nafuu.

“Na hii inawezekana kwa sababu moja ya vitu ambavyo vinasababisha kuongezeka kwa bei ya sukari ni gharama kubwa ya umeme."

"Kwa hiyo Serikali katika jitihada zetu tunatarajia megawati 2115 zitakazozalishwa  viwanda vitapata umeme wa gharama nafuu na hivyo  uzalishaji ukawa wa gharama nafuu,” amesema Msigwa.

Advertisement