Umesoma vitabu vingapi mwaka 2022?

Muktasari:

  • Pengine ni swali zito kwa walio wengi hasa kutokana na ukweli kuwa Watanzania wengi hawana utamaduni wa kujisomea.


Pengine ni swali zito kwa walio wengi hasa kutokana na ukweli kuwa Watanzania wengi hawana utamaduni wa kujisomea.

Makala haya yanaangazia baadhi ya watu maarufu nchini hususan wanasiasa wakielezea walivyotumia mwaka 2023 kujisomea vitabu mbalimbali.

Ushuhuda wao ni hamasa tosha kwa jamii ya Kitanzania kujihimu katika kusoma vitabu, kama mojawapo ya njia muhimu za kupata maarifa ya aina mbalimbali.



Dk Helen Kijo Bisimba (Mkurugenzi wa zamani wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)

Anasema mwaka huu, amesoma vitabu 18 vyenye maudhui tofauti , ikiwamo Biblia.Alivitaja baadhi ya vitabu hivyo kuwa ni The Magic na Secret.

“Nimevutiwa kusoma vitabu hivi kwa sababu vina ujumbe tofauti na vinaeleza umuhimu wa mtu kuwa na mawazo chanya na hivyo kutoa siri ya namna ya kufanikiwa. Wakati kitabu cha The Magic kinaeleza siri ya kushukuru, yaani ukiwa mtu wa shukrani unafanikiwa sana, kuliko kuwa mtu wa kila siku kunung’unika hata kidogo ukioni.

Vitabu vingine ni katika Biblia nimesoma kuanzia mwanzo hadi Isaya, sasa hivi nipo Isaya ya 17. Kila mwaka nasoma vitabu vya Biblia lakini mwaka huu nimewasoma wanawake katika biblia na nafasi walizoshika, niko katika utafiti nimeanza Mwanzo na nimeshafika Isaya nategemea kufika mwisho.’’


Ismail Jussa Ladhu (Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mfuko wa Maalim Seif Sharrif Hamad)

Mwanasiasa huyu amesoma makumi ya vitabu mwaka huu. Hata hivyo anasema: ‘‘Mwaka huu nimesoma kitabu cha ‘Twilight of Democracy: The Failure of Politics and The Parting of Friends’ cha mwandishi Anne Applebaum.

Hiki ni kitabu muhimu katika kuelewa masaibu yanayoikumba demokrasia duniani katika miongo mitatu iliyopita.

Vitabu vya aina hii vinanisaidia sana kunipa tafakuri ya hali ya mambo inavyokwenda na pia kujihoji katika baadhi ya mambo ninayoyaamini.

Kwa upande mwingine vinaongeza maarifa na kuifahamu kwa mapana zaidi dunia tunayoishi.

Kitabu ambacho kilisisimua hisia zangu ni ‘38 Reflections on Mwalimu Nyerere’ cha Mark Mwandosya na Juma Mwapachu ambacho ni mkusanyiko wa kumbukumbu za watu 38 waliokuwa karibu na waliofanya kazi na Mwalimu Nyerere. Kuna watu wamefunguka sana na kutueleza mengi tuliyokuwa hatuyajui yaliyokuwa yakipitikana kwenye duru za utawala. Watu kama Mzee John Malecela kwa mara ya kwanza ametueleza jinsi alivyong’olewa kugombea urais mwaka 1995 kwa kupitia nguvu kubwa iliyotumiwa na Nyerere kwa sababu tu alithubutu kumwambia yasiyompendeza.

Ukiacha vitabu vya aina hiyo, ninapenda sana historia na hasa historia ya Zanzibar. Ninaamini unapokuwa kiongozi unapaswa kuijua vyema historia ya nchi yako na ulimwengu kwa ujumla. Kwenye historia, vitabu nilivyosoma ni pamoja na ‘Zanzibar Personalities and Events’ cha Nasser Abdallah Al Riyami, ‘Maisha Yangu: Miaka Minane Ndani ya Baraza la Mapinduzi: Khaini au Mhanga wa Mapinduzi?’ cha Khamis Abdulla Ameir,

Vingine ni ‘Biubwa Amour Zahor: Mwanamke Mwanamapinduzi’ kilichoandikwa na Zuhura Yunus, ‘Zanzibar: The Last Years of the Protectorate: A Constitutional and Political Account’ cha Maulid Mshangama, na ‘Sufis and Scholars of the Sea: Family Networks in East Africa 1860 - 1925’ cha Anne K. Bang.


Zitto Kabwe (Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT- Wazalendo

Ulikuwa mwaka mzuri kwa usomaji vitabu na pia mwaka ambao nilibahatika kupata zawadi nyingi za vitabu kutoka kwa marafiki zangu na ndugu zangu. Nitaanza mwaka 2023, Mungu akijaalia kuvuka salama, nikiwa na karibu dazeni ya vitabu ambavyo sijasoma.

Kama nilivyofanya mwaka jana, kutoka orodha ya mwaka huu nimeshatoa orodha ya vitabu 10 ninavyopendekeza watu kuvisoma mwaka ujao kama hawajavisoma.

Orodha hiyo ipo hapa https://thechanzo.com/2022/12/12/zitto-kabwes-ten-book-recommendations-for-2023/

Zitto anasema mwaka huu amesoma jumla ya vitabu 33 zikiwamo riwaya 10, wasifu na tawasifu 10, vitabu vitano vinavyoelezea nchi na vitabu vingine mchanganyiko saba. Baadhi ya riwaya ni pamoja na Magic of Saida, I am Semba na The Book of Secrets.

Wasifu anataja The Chancellor: The Remarkable Odyssey of Angela Merkel, Reflections on Mwalimu Nyerere na Juhudi na Changamoto cha Sheikh Ponda Issa Ponda. Vitabu mchanganyiko ni pamoja na Time for Socialism, Capturing Hope: The Struggle Continues for a New Malaysia na From Rebel to Ruler: One Hundred Years of the Chinese Communist Party.


Florence Majani (Mwandishi wa habari mwandamizi nchini)

Anasema: ‘‘Nimesoma vitabu 37, vinavyohusu Twitter use and Political campaigns yaani matumizi ya mtandao wa twitter na kampeni za siasa. Na hii ni kwa sababu eneo hilo nalifanyia utafiti.

Hata hivyo, nimesoma kitabu Cha How to deal with difficult people na The Stars are shining down kilichoandikwa na Sydney Sheldon.

Hiki cha Stars are shining down ndicho kitabu bora kwangu mwaka huu, na ni riwaya inayozungumzia biashara ya ujenzi na namna ilivyomwezesha mwanamke mmoja yatima kuwa milionea.

Ama kuhusu How to deal with Difficult people cha Gill Hasson, hiki kitabu ni nyenzo muhimu ya kuweza kuishi na wenzako kazini na zaidi hasa kinakupa mbinu za kukabiliana na wale watu wenye kisirani na wanaoshutumu zaidi.’’


John Mnyika (Katibu Mkuu wa Chadema)

Mwanasiasa huyu kijana anasema: ‘‘Nimesoma vitabu mbalimbali ila nilivyovisoma kwa karibu zaidi ni Biblia Takatifu, Quran Tukufu, Islam in focus cha Hammudah Abdalati , Islam The Misunderstood Religion cha Muhammad Qutb, Maisha ya Watakatifu wa Kila Siku cha Padri Leandry Kimario Ofm Cap , Emma’s Encyclopedia Tanzania of records 1497-1995 na The Art of War.


Magdalena Sakaya (Naibu Kagtibu Mkuu CUF)

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, bara Magdalena Sakaya anasema mwaka huu kutokana na kutingwa na majukumu mbalimbali, amefanikiwa kusoma vitabu takribani vitatu kikiwemo cha Principle za Maisha cha Eric Shigongo.

“Kingine nimekisahau kidogo lakini kinaelezeea kustaafu tajiri au umasikini au uamuzi wako.Nimependa kusoma hasa vya Shigongo kwa sababu mwandishi anaelezea alikotoka na anakoelekea pamoja na changamoto anazokutana nazo.

“ Mwandishi ameeleza pamoja na changamoto lakini hajakata tamaa hadi anafanikiwa.Kitabu hiki kimenisaidia na kuniimarisha namna ya kupambana na maisha.’’


Susan Lyimo (Spika wa Bunge la Wananchi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Anasema mwaka huu amesoma vitabu vitano ikiwemo kwa njia ya mtandao vyenye maudhui ya harakati za wanawake, ukombozi na haki za binadamu.

“ Kilichonivutia kusoma ni kutaka kujua huko wenzetu nyuma walifanyaje, tupo wapi na tunatakiwa kufanya nini ili kuendeleza mapambano,” anasema Lyimo ambaye ni mbunge wa zamani wa viti maalumu kuanzia mwaka 2005 hadi 2020.