Umiliki wa nyumba kwa wageni bado kitendawili

Dar es Salaam. Sekta ya majengo nchini Tanzania ni moja ya sekta zinazokua kwa kasi barani Afrika lakini kwa jinsi ilivyo, umiliki wa majengo kwa raia wa kigeni umepigwa marufuku kisheria kwa sababu ardhi ni mali ya umma.

Na kwa ukuaji huu unaoendelea, inakuja changamoto sokoni, jambo ambalo waendelezaji na wataalamu wa sekta hii wanaamini kuwa linaweza kutatuliwa kwa kuruhusu wageni kununua nyumba kwa sababu hiyo itachochea ukuaji wa sekta hiyo.

Wanaounga mkono hoja hiyo wanasema hiyo ni biashara pekee ambayo uongezaji wa thamani unafanyika ndani ya nchi na hakuna uhamishaji wa mtaji kwa sababu nyumba inabaki hapa nchini.

Haya yanajiri wakati Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linalomilikiwa na Serikali likipendekeza hatua kali zitakazobadili mwelekeo wa sekta ya majengo nchinizichukuliwe.

Miongoni mwa hatua zilizopendekezwa ni Serikali kuondoa vikwazo vyote vinavyokwamisha wanadiaspora wa Tanzania na wageni wengine kununua na kuwekeza katika sekta ya majengo.

Akizungumza na Mwananchi, Ofisa Mtendaji Mkuu wa shirika la Watumishi Housing Investment (WHI), Dk Fred Msemwa alisema faida kuu wanayopata inatokana na mtaji kutoka nje (FDI) kwa sababu wanunuzi wa nje hawakopi fedha kutoka soko la ndani bali huleta mtaji kutoka nje ya nchi.

Hiyo, alisema itaongeza uchangamfu wa sekta ya nyumba isiyohamishika na kuchangia pato la Taifa (GDP) mbali na kodi nyinginezo kama vile Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na kodi ya kampuni itakayokusanywa na Serikali.

“Mipango hii inatakiwa kwenda sambamba na hatua za kisera ambazo zitawawezesha Watanzania wa ndani pia kumiliki nyumba. Hatua ya hivi karibuni ya kibajeti iliyochukuliwa na Serikali kuondoa VAT kwenye nyumba zinazogharimu chini ya Sh50 milioni, ni njia sahihi,” alisisitiza.

Mipango mingine lazima pia ifikie kiwango cha kuongeza uwezo wa waendelezaji wa sekta ya umma na binafsi kupata fedha za ujenzi ili kuwawezesha kusambaza nyumba za bei nafuu sokoni.

Akizungumza katika kikao na wahariri jijini Dar es Salaam mapema wiki iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah alisema Tanzania inakosa mapato mengi kwa kuwanyima wageni haki ya kumiliki majengo nchini.

Anasema kuwa nchi nyingine, kama vile Rwanda, Kenya, Afrika Kusini na nchi zenye uchumi wa juu kama vile Dubai, zinaruhusu wageni kumiliki nyumba.

“Tunakosa kutumia fursa hizo kubwa ambapo watu mashuhuri wanaweza kumiliki nyumba zao kwa ajili ya mapumziko ya likizo nchini Tanzania,” alisema.

Alisema Bill Gates, ambaye anapenda kutembelea Tanzania, anaweza kumiliki nyumba hapa; hata hivyo, kutokana na vikwazo vyetu vya kisheria, hatakiwi kumiliki nyumba yake atakayoitumia wakati wa likizo nchini.

“Bill Gates akija Tanzania tunamuuzia nini zaidi ya picha za kuchora?” alihoji.

“Bill Gates anaweza kumudu kununua nyumba ya likizo ya dola 2 milioni huko Arusha. Hii itatupa fursa ya kumshawishi kuifanya Tanzania kuwa mahali anapopendelea zaidi.”


Mfano wa Zanzibar

Lakini hii ingelazimika kuja na safu ya mabadiliko katika sheria za uhamiaji ili kumpa mnunuzi aina fulani ya makazi ambayo inawaruhusu kupata mali kwa mwaka mzima.

Kwa upande wa Zanzibar, mabadiliko kadhaa yamefanyika ili kukabiliana na umiliki wa nje kwa Sheria ya Mamlaka ya Kukuza na Kulinda Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Na. 14 ya mwaka 2018, ambayo inatoa motisha kwa mnunuzi yeyote anayenunua nyumba yenye thamani isiyopungua dola 100,000.

Manufaa hayo ni pamoja na kibali cha mkazi kwa mmiliki wa awali na mwenza wake na watoto wanne walio na umri chini ya miaka 20, asilimia 100 ya umiliki wa nyumba kwa wageni, asilimia 100 ya msamaha wa mapato ya kimataifa kwa mgeni, asilimia 100 ya posho ya kurejesha faida bila malipo baada ya kodi.


Kiungo kinachokosekana

Hata hivyo, pamoja na kuwepo kwa motisha hizo zote, vikwazo kadhaa bado vipo, kwa mfano inachukua muda mrefu kwa ZIPA kutoa hati ndogo ya kumiliki nyumba.

Vibali vya ukaazi havina uhakika pia kutokana na ukweli kwamba uhamiaji ni suala la Muungano ambalo linapaswa kushughulikiwa na Bunge ili sheria ibadilishwe.

Katika mahojiano, waendelezaji wa majengo katika Mji wa Fumba, CPS na Fumba Uptown Living wanasema kasi ya utekelezaji wa masharti fulani inafanya kuwa vigumu kufikia malengo fulani kwa wakati.

Wanataja masuala ya vibali vya kuishi na hatimiliki kuwa kikwazo kikubwa.

“Inachukua muda mrefu sana kupata hati miliki kutoka kwa mamlaka, kwa sababu tuko chini ya maeneo huru ya kiuchumi hatimiliki zinatakiwa kutolewa na ZIPA, lakini hatimiliki za mali nyingine zinatoka kwenye wizara ya ardhi,” Mhandisi Saeed Bakhressa ambaye alikuwa mkurugenzi wa mradi wa Fumba Uptown Living aliiambia Mwananchi.

Matokeo yake, walichokuwa wakitoa vyeti vya umiliki wa muda wakisubiri hati miliki.

Alisema kutokana na kasoro hizo za udhibiti, baadhi ya wanunuzi wanalazimika kujiondoa katika makubaliano ya ununuzi.

“Sheria tulizo nazo zimeainishwa vyema kwenye karatasi kuhusu masuala kama vile ukaazi, hata hivyo, linapokuja suala la utekelezaji ndipo ucheleweshaji unapoanzia,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Fumba Town, Sebastian Dietzold, pia katika mahojiano, alipongeza uamuzi wa kimkakati wa kubadilisha sheria ili kuruhusu umiliki wa kigeni Zanzibar.

Alisema ni muhimu wamiliki wa mali kupata ukaazi kwa sababu hakuna anayetaka kuwekeza mamia ya maelfu ya dola na kisha kuhitaji visa kufika kwenye nyumba yake.