Umuhimu wa ultrasound kwa wajawazito

Muktasari:

  • Wataalamu wa afya wameshauri mjamzito kufanyiwa uchunguzi wa mtoto aliyetumboni angalau mara tatu kabla ya kujifungua.

Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wameshauri mjamzito kufanyiwa uchunguzi wa mtoto aliyetumboni angalau mara tatu kabla ya kujifungua.

Kipimo ambacho wataalamu hao wanashauri ni cha ultrasound, kinachoonyesha picha ya mtoto akiwa tumboni na maendeleo ya ukuaji wake.

Kipimo hiki hakitumii mionzi, bali hutumia mawimbi ya sauti na mwangwi, ndio maana wataalamu wanasema, ni salama kutumika kwa mjamzito.

Baadhi ya vifo vya wajawazito vimekuwa vikielezwa kuchangiwa na kutokufanywa kwa vipimo hivyo.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi kutoka Hospitali ya Salaaman iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam, anasema gharama za kipimo cha ultrasound huanzia Sh10,000 hadi Sh35,000, “hutegemea na kituo husika, ndiyo maana bei zinatofautiana.”

Akizungumza na gazeti hili, mtaalamu wa tiba ya mionzi kutoka Hospitali ya Mkoa na Rufani ya Temeke, Dk Harieth William anasema kipimo cha ultrasound kinatakiwa kufanyika miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito, miezi mitatu ya pili ya ujauzito na miezi mitatu ya mwisho.

“Kwa miezi mitatu ya mwanzo ambayo ni kati ya wiki tano mpaka nane tunahakikisha kama kweli mama ni mjamzito kwa kuangalia mapigo ya moyo ya mtoto aliye tumboni, hii inaashiria kama kiumbe kipo hai,” anasema.

“Vilevile inatusaidia kutambua umri wa ujauzito na matarajio ya kujifungua kwa mama ambaye hakuwa na uhakika na mzunguko wake wa hedhi na itasaidia kama mtoto aliyetumboni ni zaidi ya mmoja,” anasema Dk Harieth.

Kuhusu kipimo cha pili, Dk Harieth anasema kinatakiwa kufanyika ujauzito unapofikisha wiki 18 hadi 22, sawa na miezi mitano kuelekea miezi sita, lengo kuangalia ukuaji wa mtoto.

“Hapa tunaangalia viungo kama vina ulemavu wowote na mlalo wa mtoto, pia katika hatua hii ya ujauzito jinsia ya mtoto inaweza kugunduliwa na vilevile tunaangalia nini kimetangulia kupita katika mlango wa kizazi ili hatua za kuzalisha salama zichukuliwe,’’ anasema Dk Harieth.

Mtaalamu huyo anaeleza zaidi kuhusu kipimo cha hatua ya mwisho kuwa, mimba inapofikisha wiki 32 hadi wiki za mwisho pia mama anatakiwa kufanyiwa kipimo hicho.

“Hatua hii ya mwisho inatusaidia kujua kiwango cha maji yaliyopo ndani ya mji wa mimba, tunaangalia kondo la nyuma na kiasi cha damu kwenda kwa mtoto, pia hapa ndio tunatambua kama mtoto amekaa mkao unaotakiwa tumboni au amegeuka na njia gani ya kujifungua itumike kwa mama,” anasema Dk Harieth.


Wanachosema wananchi

Ajuna Jackson, mkazi wa Bunju ambaye alishawahi kufanyiwa kipimo hicho akiwa mjamzito anasema, “nilivyojigundua nina ujauzito nilikwenda kufanyiwa kipimo cha ultrasound kwa sababu niliona kwenye mitandao umuhimu wa kufanya uchunguzi huo wakati wa ujauzito.

“Pia, nilivyoanza kuhudhuria kliniki ilikuwa ni lazima tupeleke picha ya ultrasound ya miezi mitatu, sita na tisa.

“Nilipiga ultrasound nyingi kwa sababu kuna muda nilikuwa nasikia maumivu ya tumbo nikaambiwa nifanyiwe kipimo hicho kama kuna shida yoyote itaonekana, hata hivyo nilikuwa nasikia furaha nilivyokuwa namuona mtoto wangu,’’ anasema Ajuna.

Chezalina Mlowe, mkazi wa Kimara anasema alishawahi kufanyiwa kipimo hicho kipindi chake cha ujauzito.

“Mimba yangu ya pili nilihudhuria kliniki muda ukiwa umeenda kidogo, nilivyoanza kufanya vipimo vya kawaida ikiwamo kipimo cha uzito, niligundua uzito wangu unapanda tofauti na ujauzito wa kwanza, ilinibidi nikafanye kipimo cha ultrasound na mtaalamu aliniambia nina mapacha.’’

Dk Lightness Barnabas kutoka Hospitali ya Jeshi Lugalo anasema kipimo cha ultrasound kimekuja kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, kwa kuwa awali wataalamu walitumia njia tofauti ili kujua maendeleo ya mtoto tumboni. “Ili kujua mama ana mtoto zaidi ya mmoja miaka ya nyuma tulikuwa tukigusa tumbo ndipo tunagundua vichwa viko vingapi na miguu inakuwa mingi,” anasema Dk Lightness.

“Kwa upande wa ulalo wa mtoto sisi tunakitafuta kichwa ndo kinachotuongoza kujua mtoto amekaaje.”

Anaeleza uwepo wa kipimo cha ultrasound umesaidia kupunguza idadi ya vifo vya mama na mtoto.

“Ultrasound imesaidia kuokoa maisha, hasa kwa wale ujauzito unaoharibika, lakini unakuwa haujatoka wote mama anakuwa anawahi kusafishwa ili kuzuia kutokwa na damu nyingi,” anasema Dk Lightness.

Faida nyingine za kipimo ni kutambua aina ya kiumbe ndani ya mji wa mimba kama ni mtoto au kitu kingine, kujua kama mimba imetoka au ipo, kujua kama mtoto mzima au mfu, kufahamu maendeleo ya mtoto, ikiwemo kuongezeka uzito.