Umuhimu wa vikao vya familia

Ni kawaida kila ifikapo mwisho wa mwaka kwa baadhi ya familia za Wachaga kufunga safari kutoka pande zote za nchi na kurejea kwao mkoani Kilimanjaro, pamoja na kusherehekea sikuu za mwisho wa mwaka hupata pia fursa ya kukaa pamoja na kuzungumza mambo yanayowahusu wanafamilia.

Licha ya kuwa utaratibu huu hufanywa pia na baadhi ya watu wa makabila mengine lakini sio kwa ukubwa kama ilivyo kwa wachaga ila nao pia hupata fursa ya wanafamilia kuzungumza masuala mbalimbali.

Maendeleo ya teknolojia na utandawazi yamechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa utaratibu huu kuanzia ngazi za familia hadi ukoo na kutajwa kuwa hali hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa mmomonyoko wa maadili kwa kuwa watoto na vijana wanakosa busara za wazee.

Changamoto hii haipo tu kwenye ngazi za ukoo, hata upande wa familia inayohusisha baba, mama na watoto ni nadra kukuta wana utaratibu wa vikao hivyo wakati mwingine inawawia vigumu kutafuta suluhu ya migogoro.

Mfano wa hili unathibitishwa na Masanja Mabula (si jina halisi) yeye anasema kuna wakati anakaa mwezi mzima hazungumzi na mkewe hivyo analazimika kutumia muda mwingi akiwa nje kuliko anavyotakiwa kuwa nyumbani.

“Kuna wakati mke wangu ananinyamazia, hata umuongeleshe atakujibu hicho ulichomuuliza kisha anaendelea kunyamaza. Kwa kuwa yeye ni mama wa nyumbani na ananitegemea kwa kila kitu utaona ujumbe wake wa simu pale anapoishiwa mahitaji na atakachoandika ni mchele umeisha, gesi imeisha hapo anakuwa amemaliza.

“Nimejaribu mara kadhaa kutafuta suluhu kwa kukaa chini kuzungumza lakini anaonekana hayuko tayari kwa hilo, hivyo basi tunaendelea kuongeza siku na kwa sababu hiyo siwezi kuwa nawahi kurudi nyumbani ni heri nikae bar na washkaji nikifika nikute amelala,”anasema Mabula.

Kilio cha Mabula kinashabiana na yale yaliyondikwa na Johness Clinton kwenye jarida la Familymatters kuhusu umuhimu wa wanafamilia kuzungumza na hasa wanandoa kwani kinyume chake huhatarisha uimara wa ndoa na familia kwa ujumla.

“Mawasiliano baina ya wanafamilia ni muhimu katika kuhakikisha kila mmoja anamuelewa mwenzake.Ukiwa na uwezo wa kuzungumza na wanafamilia wenzio utaweza kushirikisha mawazo yako kwa maana ya kile unachokiamini na kukiona kipo sawa. Ikitokea mmeshindwa kukubaliana katika jambo fulani, kupitia mazungumzo utajua sababu za kupingana na wewe na mwisho mtafikia makubaliano.

“Mazungumzo husaidia familia kutatua changamoto zinazowakabili. Pale tatizo linapojitokeza ndani ya familia ni vyema likapatiwa ufumbuzi na hilo litawezekana endapo wanafamilia watakuwa tayari kukaa chini na kuzungumza. Mazungumzo yanapofanyika inafungua milango kwa wanafamilia kuwa karibu zaidi na kutafuta suluhu ya pamoja itakayowaunganisha,”.

Hilo linawekewa msisitizo na Mwanasaikolojia Christian Bwaya ambaye anasema familia ni taasisi kama taasisi nyingine na hakuna taasisi inaweza kuendeshwa bila vikao kinyume na hapo kuna mtu akuwa anafikiri mawazo yake ndio maamuzi ya familia na hapo ndipo migogoro mingi inapoanzia.

“Tuanze na vikao vya wazazi (wenzi). Mnapokutana kuzungumza mnajenga mshikamano. Unapokuwa na mazingira ambayo kila mmoja anajua hatutafanya jambo bila kuzungumza kwanza inajenga dhana kuwa mnaaminiana. Mnapoaminiana mnaongeza ukaribu unaowawezesha kufahamiana zaidi.

“Ndio maana wataalam wengi wa mahusiano ya familia wanashauri kuweka mazingira wezeshi kuwa na vikao vya mara kwa mara kati ya baba na mama. Vikao vinawasaidia kuweka mipango ya pamoja, kujitathmini, kushirikishana mambo kadri yanavyojitokeza na kusuluhisha tofauti kabla hazijaleta matatizo makubwa. Mkikosa vikao mnaongeza umbali kati yenu hali inayoweza kuzalisha na kukuza matatizo mengi.

Bwaya anasema tabia ya vikao vya wazazi inajenga pia utaratibu wa vikao na watoto hatua inayowafunza ushirikiano baina yao.

“Mnapokutana na watoto mara kwa mara kwanza mnawafundisha kushirikiana. Watoto wanajifunza namna taasisi ya familia inavyoendeshwa pasipo hata kuwaambia moja kwa moja. Wanaona kila wiki mnakaa na kuzungumza. Kuna kitu wanajifunza.

Kuwa familia inaongozwa kwa ushirikiano wa wazazi na watoto. Siku wakiwa watu wazima watapeleka uelewa huo kwenye familia zao. Vile vile, vikao vinasaidia kupanga mipango ya pamoja kama familia.

Mwanasaikolojia huyu anashauri kuwa ni vyema mwaka unapoanza kwa familia kukaa na pamoja kuchora ramani ya wapi inataka kwenda na ni fursa inayopaswa kutumiwa na wazazi kuwasikiliza watoto na kuwasaidia kuweka mikakati ya kufikia malengo yao.

“Tabia kama hii inajenga kuaminiana. Mtoto anajua hata nikiwa na shida mahali, familia ndio kimbilio langu la kwanza. Vikao na watoto vinasaidia kubaini viashiria vya tatizo mapema. Msipokuwa na tabia ya kukutana mnaweza kuishi na mtu mwenye sonona na hamjui. Vikao vinasaidia kujua nani hajisikii vizuri, nani ana tabia zipi, nani anafikiri nini, nani ana shida na nani na mnamsaidia mapema,”anasema.
Bethy Buchumi (35) anasema hakumbuki kama hata mara moja familia yake imewahi kuwa na kikao cha kujadili kitu chochote kwa kuwa maamuzi yote yamekuwa yakifanywa na wazazi wake hususani baba.

“Kiukweli sijawahi kuona kikao na kama kiliwahi kuwepo basi sikushirikishwa, kwetu baba ndiye kila kitu na msaidizi wake mama, wao wanafanya maamuzi nyie mnakuja kupewa taarifa au maelekezo lakini kusema kwamba tukae chini kwa pamoja kujadili kitu haikuwahi kutokea.

Mtaalam wa malezi ambaye pia ni mkurugenzi wa taasisi ya Maadili Centre Florentine Senya anasema ni familia chache zenye utaratibu wa kukutana na kuzungumza jambo ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa mmomonyoko wa maadili.

Anasema kutokana na maendeleo ya teknolojia kinachofanyika kwa sasa kwenye familia nyingi ni kupeana taarifa lakini sio muda wa kukaa kwa pamoja na kujadili mambo yanayohusu wanafamilia.

“Siku hizi watu wa familia moja wanafungua makundi zogozi ya whatsapp na kupeana taarifa hivyo inaweza kutokea hata mwaka mzima hawajakaa pamoja na kuzungumza. Wasichojua wengi ni kwamba vikao vinasaidia kuongeza mshikamano baina ya wanafamilia, mnapoonana ni rahisi kujua mwingine ana changamoto gani mkasaidiana.

“Mambo ya kuzungumza kwenye simu upo uwezekano hujui unayezungumza naye yupo katika hali gani anapitia yapi au huenda ameshaharibikiwa kimaisha, mnapokutana inatoa nafasi ya kushauriana, kuonyana inapobidi na kusaidia pale inapohitajika kufanyika hivyo. Kingine pamoja na maendeleo ya teknolojia nafasi ya wazazi kukutana na watoto wao bado inahitajika na ni msingi imara wa familia,” anasema Senya.

“Mbali na hilo anasema kuna watu kwao ni rahisi kutafuta msaada kwa marafiki au watu wengine wa mbali kuliko ndugu au mwanafamilia mwenzie. Hili linaweza kusababishwa na mfumo wa maisha wa sasa ambao kila mtu anapambana na hali yake au hata tabia ambayo imejijenga kwa mtu husika hataki kuzungumza na wanafamilia wake.

Rehema Nkwanga ambaye ni mwalimu wa malezi na maadili anasema kuna umuhimu mkubwa wa familia kuwa na utaratibu wa kukutana na kuzungumza kwani hilo husaidia kuiweka mbali mambo yanayoweza kuwagombanisha.

“Familia inapokuwa na mawasiliano mazuri haitayumbishwa na mambo yasiyo na tija. Kuna baadhi ya familia umbea inaweza kuwa tatizo kubwa. Tafiti zinaonesha kuwa umbea na majungu huchangia kuwavuruga wanafamilia na kuwafanya washindwe kuwa na mawasiliano mazuri.

“Njia nzuri ya kukabiliana na hilo kwa ngazi ya familia ni kuwa na mazungumzo na kutoruhusu kuvurugwa na maneno yasiyo na tija. Kutokana na hilo badala ya kupoteza muda kushughulikia majungu ni bora kuwekeza nguvu kwenye mazungumzo na mawasiliano thabiti na kuifanya familia yenu iendelee kuwa imara,”anasema Rehema.

Mbali na hilo Rehema anabainisha kuwa familia inayozungumza na yenye mawasiliano imara ni rahisi kuzivuka nyakati ngumu pamoja.

“Mambo hayawezi kuwa mteremko wakati wote kuna nyakati changamoto zinaweza kutokea, kama familia iko imara na yenye mshikamano itakuwa rahisi kuzipita nyakati hizo na kuendelea kuwa imara. Hilo linaweza kuonekana pia kwenye nyakati za changamoto kwa mwanafamilia ikiwemo kupoteza kazi, kuugua kwa muda mrefu au hata msongo wa mawazo unaotokana na hali ngumu ya kiuchumi,”.