UN: Tuwekeze zaidi kwa vijana

Muktasari:

  • UNFPA na Ubalozi wa Denmark wameandaa majadiliano hayo kuadhimisha wiki ya Nordic wakiangazia ongezeko la watu, fursa na changamoto zake.

Dar es Salaam. Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Mark Schreiner amesema uwekezaji mkubwa unahitajika kwa vijana ili kuwawezesha kuwa na ujuzi wa kufanya kazi.

 Schreiner amebainisha hayo leo Mei 30, 2023 wakati wa majadiliano katika wiki ya Nordic inayoadhimishwa na nchi za Denmark, Finland, Norway na Sweden.

Majadiliano hayo yameandaliwa na Ubalozi wa Denmark kwa kushirikiana na UNFPA na yaliangazia ongezeko la watu duniani sambamba na fursa na changamoto zinazoletwa na ongezeko hilo.

Amesema idadi ya watu duniani sasa ni zaidi ya bilioni nane, huku Tanzania ikiwa na watu karibu milioni 62 na ukuaji wake ni asilimia 3.2.

Amesema asilimia 60 ya watu nchini Tanzania wana umri chini ya miaka 24 na idadi ya vijana inaongezeka. Amesema umri wa kuishi pia umeongezeka hadi kufikia miaka 65 kwa wanaume na miaka 69 kwa wanawake.

"Ukuaji huu maana yake uwekezaji wa haraka unahitajika kwenye ajira, elimu na afya hasa huduma ya afya ya uzazi. Mnakumbuka kwamba kila Dola moja ya Marekani inawekezwa katika uzazi wa mpango, hii unaweza kuokoa fedha za serikali hadi dola sita," amesema Schreiner.

Amesema maendeleo katika sekta ya afya yamechochea ongezeko la watu kwa kuwa wazazi wanazalishwa hospitali, wanawake wanaopata huduma hospitali imeongezeka na vifo vya watoto chini ya miaka mitano imepungua.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umaskini nchini (Repoa), Dk Donald Mmari amesema ongezeko la idadi ya watu linaweza kuwa fursa na changamoto kwa upande mwingine.

Amesema fursa zinazopatikana ni pamoja na soko pamoja na chanzo cha nguvu kazi hasa pale watu hao wanapokuwa na ujuzi wa kuwawezesha kufanya kazi.

Kuhusu changamoto, Dk Mmari amesema unapokuwa na watu wengi lakini hawana ujuzi, wanakuwa mzigo kwa Taifa badala ya kuwa wazalishaji tegemewa kwa Taifa.

"Ongezeko la idadi ya watu na mabadiliko ya tabianchi ni vitu viwili vinavyoshindana. Watu wakiwa wengi, kunakuwa na uharibifu mkubwa wa mazingira, watu watachoma mkaa, watakata kuni, watajenga majumba. Yote haya yanachochea mabadiliko ya tabianchi," amesema mkurugenzi huyo.