Unahitaji ufadhili wa masomo nje ya nchi? Changamkia fursa

Muktasari:

  • Nchi tatu zimetangaza  ufadhili wa shahada ya kwanza, uzamili na uzamivu katika muhula wa mwaka 2024/25.  

Dar es Salaam. Bila shaka unaweza kuwa miongoni mwa Watanzania vijana wenye changamoto za uwezo wa kujiendeleza kielimu kutokana hali ya kipato.

Habari njema kutoka mataifa matatu--- China, Uturuki na Mauritius yanayoweza kutimiza ndoto zako baada ya kutangaza ufadhili wa shahada ya kwanza, uzamili na uzamivu katika muhula wa 2024/25.

Hata hivyo, unaweza kukabiliwa na kikwazo cha kigezo cha umri katika maombi yako endapo hautakuwa na umri kati ya miaka 25  hadi 40 kwa mwombaji kuanzia shahada ya kwanza hadi uzamivu.  

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo katika tovuti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Iddi Seif Bakari ametoa wito kwa Watanzania kutuma maombi kabla Februari 20, 2024 ili kunufaika na fursa hiyo katika vyuo mbalimbali nchini humo.

Katika barua yake aliyoituma Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Bakari amesema ufadhili huo utatolewa na taasisi tatu; Turkiye Baurslari, Diyanet Burslari-Turkiye Diyanet Vakfi na Islamic Development Bank. Taarifa za maombi zinapatikana kwenye tovuti za taasisi hizo.

Pili, ni fursa iliyotangazwa na Serikali ya Mauritius ya kufadhili Watanzania watakaonufaika na fursa ya masomo ngazi ya shahada ya kwanza, uzamili na uzamivu katika vyuo mbalimbali vilivyopo nchini humo.

Mwisho wa kutuma maombi kwa kuzingatia vigezo ni Aprili 5, 2024 kupitia tovuti ya http://ministry-education.govmu.org na http://highereducationmauritius.com

Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, fursa nyingine imehusisha kusoma nchini China chini ya ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China. Ufadhili huo unahusisha shahada ya kwanza, uzamili na uzamivu na mwisho wa kufanya maombi ni Januari 25, 2024. Tembelea tovuti ya www.campuschina.org