Unajua kinachowavutia vijana kufunga ndoa na watu wazima?
Muktasari:
- “Nilikuwa na mke wangu aliyenipenda sana, alikuwa ananitunza vizuri Mungu akamchukua, sasa siwezi kukaa peke yangu, lazima nipate mwenza ambaye atakuwa msaidizi wangu, nahitaji mtu wa karibu wa kunitunza na kunihudumia.
“Nilikuwa na mke wangu aliyenipenda sana, alikuwa ananitunza vizuri Mungu akamchukua, sasa siwezi kukaa peke yangu, lazima nipate mwenza ambaye atakuwa msaidizi wangu, nahitaji mtu wa karibu wa kunitunza na kunihudumia.
“Kwanza kuoa ni takwa la Biblia kwamba mtu atakuwa na mwenzake, kama ulikuwa umeoa halafu mkeo hayupo tena duniani, sheria za kanisa zinaruhusu kama unajisikia kuoa sio dhambi. Nikiangalia afya yangu naona kuna nafasi ya mwanamke.”
Haya ni maneno ya Augustino Mrema (77) ambaye Alhamisi aligonga vichwa vya habari katika mitandao yakijamii baada ya kufunga ndoa na Doreen Kimbi (38)anayemuita dogodogo.
Mengi yamezungumzwa kuhusu ndoa hii, hasa ikiwa imetokea miezi michache baada ya Mrema kufiwa na mkewe kwamba, pamoja na udhaifu wa afya yake wengi wanahoji sababu za kufikia uamuzi huo.
Hata hivyo mwenyewe hakuruhusu ukimya akatoa majibu akisema, “amri za Mungu zinasema usitamani mwanamke wa mwenzio, kwa hali kama yangu kuwa na mwanamke anakusafisha, anakuhudumia anakufulia utamtamani tu, hiyo ni dhambi.
“Kuliko kuzini kwa macho ni bora umchukue kihalali, nimefuata taratibu zote za kanisa, nataka nikifa nizikwe vizuri nisizikwe kama mbwa. Nataka niishi maisha matakatifu ndiyo maanaa nikafikia uamuzi wa kuoa.”
Mrema ni mfano wa wazee wachache wenye uwezo kifedha au mali ambao wamefanya maamuzi kama yake ya kuingia kwenye ndoa na mabinti wadogo pengine wenye umri unaolingana na watoto wao.
Swali linalogonga vichwa vya wengi, nini hasa chanzo cha ndoa za aina hii, je ni fedha, mapenzi au kutafuta heshima.
Saikolojia inasemaje?
Mwanasaikolojia Saldeen Kimangale anasema kwenye ndoa kila mmoja ana sababu zake kwa nini anamuoa au kuolewa na fulani.
Anasema pamoja na kwamba umri huzingatiwa, lakini sio kigezo pekee, bali mapenzi, huruma na utulivu wa akili na moyo ndiyo matarajio ya wengi wanapoingia kwenye taasisi ya ndoa.
Kimangale anasema endapo hayo yatapatikana kwa mwenza mwenye umri mkubwa basi lengo limetimia, hivyo huenda hayo ndiyo yanawasukuma hata watu waliozidiana umri kufikia uamuzi wa kuingia kwa ndoa.
Hilo limethibitishwa na kauli ya Mrema katika mahojiano yake ya hivi karibuni akisema uzee wake sio kigezo cha kukosa mke wakati anahitaji.
“Uzee ni namba ila sio sababu ya mtu kuishi maisha ya upweke, unaweza kuwa na wafanyakazi wakakusaidia kazi zako, lakini mke ana nafasi yake na ni mtu muhimu sana,” anasema Mrema.
Hata hivyo, Kimangale anasema changamoto kubwa kwa wanandoa wa aina hii ni kutofautiana kwa malengo huku kila mmoja akiwa anautazama muunganiko huo kwa jicho la tofauti.
“Wakati mmoja anakusudia kujijenga mwingine yupo kwenye hatua ya kujiimarisha, lugha zao zitatofautiana. Wakati mmoja anataka kufurahia ujana wake na maisha mwingine anaangalia afe vipi. Mawasiliano yenye kuleta maana, malengo yenye kufanana na yenye maana inayokaribiana ndiyo silaha pekee inayowafanya wanandoa wadumu. Sio mali wala umaarufu wala cheo,” anasema Kimangale.
Mshauri wa uhusiano na mwandishi wa kitabu cha Usiyoyajua kuhusu mwanamume, Deogratius Sukambi anasema saikolojia ya wanaume inawafanya kuwa tayari kuingia gharama yoyote kutafuta hisia za kupenda na kupendwa na hisia ya kummiliki na kuwajibika kwa mwanamke.
“Hizi hisia mbili wanaume wanazitafuta kwa gharama yoyote kwa sababu hisia hizi huwa zina uhusiano wa moja kwa moja na kiwango cha mafanikio ya mwanamume, hisia hizi huwa zinaibua ari, kujiona hai na kuibua hamasa ndani ya moyo wa mwanamume.
“Kwa ajili ya kuzipigania hizi hisia kuna wanaume wanaweza kufanya kitendo hadi dunia inawashangaa, hivyo hiki wanachokifanya wazee kuingia kwenye uhusiano au ndoa na mabinti wadogo ni mwendelezo wa hayo yanayoweza kujitokeza na kuwashangaza watu. Katika vyote hivi ni namna anavyoutetea uanaume wake,” anasema Sukambi.
Mshauri huyo wa uhusiano anasema tafiti zinaonyesha mwanamume ambaye hana mwanamke karibu yake ambaye anammiliki na kuwajibika kwake upo uwezekano wa kuwa na uwezo mdogo wa kufikiri na hana tumaini la maisha na wengi hufa haraka.
Kuhusu upande wa wanawake ambao ni mabinti wadogo wanaokubali kuingia kwenye ndoa na wazee, anasema sababu ya kwanza ni kutafuta uhusiano unaomfanya ahisi kupendwa, kuthaminiwa na kuheshimiwa.
Pamoja na sababu hiyo pia kuna uwezekano binti akaingia kwenye ndoa na mzee kwa kumuonea huruma kutokana na upweke ambao amekuwa akiushuhudia kwenye maisha yake au labda aliwahi kumsaidia hapo awali na anataka kulipa fadhila.
“Unaweza kukuta mwanamke ana nia njema kabisa ya kuwa na mzee kwa sababu atakuwa wake peke yake, atamjali, kumpenda na kumtunza na anaweza kufikia uamuzi wa kufanya hivyo baada labda ya kuumizwa sana na vijana, basi mapenzi yake yanaweza kuwa ya dhati na akampenda mzee kwa moyo safi,” anasema Sukambi.
Mke wa Mrema anena
Akimzungumzia mumewe (Mrema), Doreen anasema hakufuata mali kwa mwanasiasa huyo kwa kuwa yeye anajiweza kiuchumi na ameingia kwenye ndoa hiyo akiwa na furaha kama mwanamke aliyepata ndoa.
“Umri hauhusiani na upendo, nilichokiangalia ni upendo wake kwangu na kusikiliza moyo wangu, moyo wangu uliponithibitishia kwamba nampenda nikaamua kufanya uamuzi. Nina shughuli zangu za kiuchumi zinazoniingizia kipato, sijafuata fedha kwa huyu mzee, nimefuata upendo na nimesukumwa na moyo wangu lakini fedha zikiwepo nikipewa sitakataa,” anasema Doreen.
Ukiwatoa wachache wanaofanya hivyo kwa dhamira ya dhati ya kuwapenda wazee wanaowaoa, Sukambi ambaye ni mshauri wa uhusiano, anasema wapo wanaoingia kwenye ndoa za aina hiyo kwa kuangalia fursa.
“Sasa hivi tupo katika ulimwengu ambao wanawake wako sensitive mno na fursa, hii inaweza kuwa fursa za kiuchumi, umaarufu, kuhakikishiwa usalama wake wa kihisia kwamba hatakuwa kwenye migogoro au kumgombania mwanamume wake na mwanamke mwingine. Wapo wanaoangalia mali mfano kaona mwanamume ana mali na fedha za kutosha anaona ajibane hapo kwamba likitokea lolote atakuwa na nafasi ya kumiliki.
“Wengine wanaona fursa ya umaarufu, kuwa akifanya kitendo hicho atazungumziwa sana na watu watatamani kumjua yeye ni nani, ukiangalia sasa hivi na utandawazi kila mtu akisikia habari kama hiyo atatamani kumjua yeye ni nani na ikiwa hivyo basi tayari amekuwa maarufu,” anasema Sukambi.
Mbali na Mrema, aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, marehemu Dk Reginald Abraham Mengi alifunga ndoa na Miss Tanzania mwaka 2000, Jacqueline Ntuyabaliwe, maarufu kwa jina la ‘K-Lynn.’