Unajutia au unajivunia kuwa Mwafrika?

Dar es Salaam. Unajutia au unajivunia kuwa Mwafrika? Takribani watu bilioni 1.4 katika Bara la Afrika leo Mei 25, wanasherehekea siku ya Afrika inayotimiza miaka 60 licha ya kukabiliwa na mitihani mbalimbali ikiwamo hoja ya kujitegemea kiuchumi, vita vya ndani, umaskini na usalama wa afya.

Hata hivyo kuna matumaini ya kujikomboa katika changamoto hizo za kivita kupitia ushirikiano wa kikanda: Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), miaka 42 ya ushirikiano wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Uchumi ya Mataifa ya Magharibi mwa Afrika (ECOWAS).

Pili, mkataba wa uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) uliosainiwa katika Mkutano wa 10 wa dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali Machi 21, 2018 Kigali, Rwanda umebeba fursa ya kujitegemea kimasoko chini ya mataifa hayo yanayoendelea kiuchumi.  

Maadhimisho hayo ya kila mwaka yanafanyika kuakisi juhudi za uanzishwaji wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), sasa ni Umoja wa Afrika (AU) chini ya malengo kadhaa ya kukabiliana na changamoto hizo.

Kwa mujibu wa tovuti ya AU, wanamajumui (PAO), wastaafu na waliopo madarakani wanashiriki maadhimisho hayo katika mataifa 55 ya bara hilo kujadili tulikotoka na tuendako kiuchumi, ajenda ya 2063 kisiasa na kiutamaduni wakati huo Tanzania ikiendelea kujivunia alama yake katika ukombozi.

Tanzania inajivunia mchango wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa miongoni mwa wanamajumui walioshawishi kuanzishwa OAU jijini Addis Ababa, Ethiopia pamoja na katibu mtendaji wa iliyokuwa Kamati ya Ukombozi Kusini mwa Afrika, Hayati Brigedia Jenerali Hashim Mbita (82).

Pia kuna Gertrude Ibengwe Mongella, aliyekuwa rais wa kwanza wa Bunge la Umoja wa Afrika pamoja na ushiriki wa wananchi, vikosi vya kulinda amani Afrika na misaada mbalimbali. 


Hali ya uchumi

Kwa mujibu wa Shirika la Fedha Duniani (IMGF) mwaka 2021, uchumi wa Afrika unakadiriwa kuwa karibu dola trilioni 2.7 ikichangia asilimia 2.84 ya Pato la Taifa la Dunia.

Kanda ya Kaskazini ina uchumi wa juu zaidi (dola 792 bilioni), ikifuatiwa na Afrika Magharibi (dola 777 bilioni). Kanda hizi mbili kwa pamoja zinashiriki takriban asilimia 58 ya uchumi wa Afrika. Asilimia 16.79 ya GDP hiyo inatoka kusini mwa Afrika, asilimia 16.44 inatoka Afrika Mashariki na asilimia 8.04 Afrika ya Kati.