Unataka kupunguza unene? Hii inakuhusu

Muktasari:

Huduma itaanza kutolewa hospitali ya Bugando hivi karibuni, daktari aeleza faida zake

Musoma. Wakati baadhi ya watu wenye tatizo la uzito mkubwa wakiripotiwa kwenda nje ya nchi kufanyiwa upasuaji, Hospitali ya Rufaa Kanda ya Bugando inatarajia kuanza kufanya upasuaji huo kwa njia ya matundu.

Wimbi la watu kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha miili yao limekuwa likiongezeka, hii ni kutokana tatizo la uzito uliokithiri linalosababishwa na mfumo wa maisha.

Daktari bingwa wa upasuaji kwa njia ya matundu katika hospitali ya Bugando, George Kanani anasema huduma hiyo inatarajiwa kuanza kutolewa mwishoni mwa mwaka huu na kwa sasa hospitali hiyo iko katika maandalizi ya miundombinu na rasilimali watu.

Anasema ili huduma hiyo ya kibingwa iweze kuwa na mafanikio, watafungua idara rasmi kwa ajili ya upasuaji maalumu kwa wenye uzito uliokithiri itakayojulikana kama Bariatric Unit.

“Hospitali imejitahidi kufanya uwekezaji kwenye suala hili kwa maana kwamba miundombinu pamoja na wataalamu. Maandalizi yamefikia pazuri, kwa hiyo mwishoni mwa mwaka huu tutaanza kutoa huduma,” anasema.

Dk Kanani anasema tatizo la uzito uliokithiri ni janga la dunia, hivyo wao kama wadau wameona ipo haja ya kuingilia kati na kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya tatizo hilo ambalo ni miongoni mwa vyanzo vya kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza.

“Sina takwimu, lakini ukweli ni kuwa uzito uliokithiri ni janga na linazidi kukua siku hadi siku, kwa hiyo zinahitajika jitihada za makusudi kukabiliana nalo. Sisi kama wadau tunaamini huduma hii ya upasuaji itakuwa mojawapo ya njia sahihi tena yenye ufanisi katika kukabiliana nalo,” anasema.

Anasema kabla ya kufanyiwa upasuaji huo, mgonjwa atafanyiwa uchunguzi wa kina kuona kama ana sifa za kufanyiwa upasuaji huo, kwani suala la upasuaji ni uamuzi na tiba ya mwisho kabisa kwa mgonjwa mwenye uzito uliokithiri.

Kulingana na mtaalamu huyo, si kila mwenye uzito mkubwa atafanyiwa upasuaji huo, akieleza ili jopo la madaktari liweze kuamua kuwa mgonjwa ana sifa za kufanyiwa upasuaji ni lazima awe ametumia njia nyingine za kitabibu bila kupata matokeo.

Mtaalamu huyo anabainisha yapo mambo mengi ya kuzingatia kabla mtu wa aina hii hajafanyiwa upasuaji, ikiwa ni pamoja na suala la uwiano kati ya uzito wa mwili na urefu (BMI), vitu ambavyo vitawaongoza wataalamu wakati wa kufanya upasuaji huo.

“Zipo njia kadhaa zinatumika kutibu tatizo hili na njia hizi ni pamoja na mazoezi na lishe, kwa hiyo kabla ya kuamua mgonjwa afanyiwe upasuaji atalazimika kwanza kutumia njia hizi kwa muda chini ya ufuatiliaji na usimamizi wa wataalamu na tukiona hakuna mabadiliko ndipo tunashauri mtu kufanyiwa upasuaji,” anasema.

Dk Kanani anaeleza mgonjwa atakayefanyiwa upasuaji huo atatakiwa kufanyiwa ufuatiliaji si chini ya miezi mitatu, ili kujiridhisha kama njia nyingine zimeshindwa kufanya kazi ndipo apangiwe kufanyiwa upasuaji.

Kuhusu gharama za upasuaji, Dk Kanani anaeleza hilo litakuwa ni suala la kiutawala zaidi, huku akisema kuwa miongoni mwa mambo yatakayozingatiwa ni pamoja na kuangalia kama huduma hii itatolewa kwa wagonjwa wenye bima ya afya ama la.


Upasuaji unafanyikaje?

Kuhusu namna upasuaji utakavyofanyika, daktari huyu anasema ni kwa njia ya matundu na kwamba una faida nyingi ikilinganishwa na upasuaji wa kawaida wa kuchana.

Miongoni mwa faida hizo ni kupunguza muda wa kukaa hospitali, kwani mgonjwa anapona haraka zaidi kutokana na kuwa na jeraha dogo ikilinganishwa na mtu aliyefanyiwa upasuaji wa kawaida.

Pia kuepusha mgonjwa kupata maambukizi katika kidonda au jeraha, kwani kunakuwepo na tundu dogo lilitobolewa wakati wa kuingiza vifaa na kwamba wakati wa upasuaji damu inayotoka pia ni kidogo ikilinganishwa na njia ya kawaida.

“Wakati wa upasuaji mgonjwa atakuwa anasimamiwa na madakatari wa aina tatu ili kuhakikisha upasuaji unakuwa na matokeo chanya. Madaktari hao ni wa upasuaji ambaye kazi yake itakuwa ni kuhakikisha kuwa upasuaji unakwenda salama kwa mujibu wa utaalamu.

“Mwingine atakuwa ni mtaalamu au dakatari wa masuala ya lishe ambaye kazi yake itakuwa ni kumsimamia na kumfundisha mgonjwa kabla na baada ya upasuaji aina gani ya vyakula anatakiwa kutumia, ili kupata matokeo mazuri yanayolengwa na wa mwisho ni daktari au mtaalamu wa saikolojia atakayehakikisha baada ya upasuaji mgonjwa anakuwa sawa kisaikolojia kutokana na ukweli kuwa wapo watu wakipata mabadiliko katika miili yao, hasa ya kupungua uzito wanaweza kupata mfadhaiko kisaikolojia,” anasema.

Dk Kanani anaeleza kuwa upasuaji wa kupunguza uzito kitaalamu upo wa aina mbili ambao aina ya kwanza ni ule wa kudumu na aina ya pili ni ule wa muda mfupi kulingana na mahitaji ya mgonjwa mwenyewe.

Upasuaji wa kudumu unahusisha ukataji wa baadhi ya viungo kama vile utumbo na kuondoa kabisa, lengo likiwa ni kupunguza ukubwa wa kiungo hicho wakati upasuaji wa muda unahusu uwekaji wa baadhi ya vifaa mwilini kama vile puto au mpira maalumu kwenye tumbo, ili kubana kwa muda fulani kulingana na mahitaji ya mgonjwa.

“Hapa kwenye kuweka vifaa inategemeana mgonjwa anakuwa amelenga kufikia uzito kiasi gani, kwa hiyo kifaa kinawekwa halafu anaendelea na programu za kupunguza uzito ambazo ni mazoezi na diet, kwa hiyo atakapofikisha uzito ule atarudi tena hospitali kwa ajili ya kuondoa kifaa hicho,” anasema.

Hata hivyo, mtaalamu huyo anaeleza kuwa njia hizi za muda mfupi upo uwezekano wa tatizo la uzito uliokithiri kumrudia mgonjwa endapo hatafuata masharti atakayopewa na wataalamu.

“Ili kufikia malengo hayo ya kupungua uzito mgonjwa atakuwa chini ya uangalizi wa madaktari katika kipindi cha kuanzia miezi mitatu hadi miaka mwili kulingana na hali ya mgonjwa mwenyewe,” anasema.


Ufanisi wa upasuaji

Anafafanua kuwa kitaalamu mtu ana uwezo wa kupungua kilo 17 hadi 30 kwa mwaka na hiyo inategemeana na aina ya upasuaji pamoja na namna mgonjwa anavyofuata ushauri wa wataalamu baada ya kufanyiwa upasuaji.

Hata hivyo, anasema upasuaji wa matundu utafanywa kwa asilimia 90 ya wagonjwa kwa maelezo kuwa wapo wengine kulingana na unene wao hawawezi kufanyiwa upasuaji huo.

“Kuna watu ni wanene sana, hivyo ukisema uingize kifaa ndani kwa njia ya tundu kile kifaa kinaishia kwenye nyama zake badala ya kufika kwenye tatizo, kwa hiyo watu wa aina hii watalazimika kufanyiwa upasuaji wa kawaida,” anasema.

Kuhusu watakaopata huduma hiyo hospitalini hapo, Dk Kanani anasema hakutakuwa na ubaguzi, hasa ikizingatiwa kuwa hiyo itakuwa ni mara ya kwanza kwa huduma hiyo kutolewa nchini, hivyo wagonjwa wote watapokelewa na kupewa huduma sawa.

Baadhi ya wakazi wa Musoma wamesema upasuaji huo utasaidia kupunguza tatizo la unene uliopitiliza, tatizo ambalo wamedai linaongezeka kwa kasi.

“Sio siri sasa hivi watu wengi wanasumbuliwa na tatizo la uzito mkubwa, yaani vitambi vya ajabu ajabu vimekuwa vingi na hii inatokana na aina ya maisha tunayoishi na vyakula tunavyokula, kwa hiyo tiba hii ikija itakuwa mkombozi wa wengi,” anasema Johari Magira, mkazi wa Musoma.

Mkazi mwingine, Anna Masunga anasema, “nadhani kuna haja ya kuwaelimisha wananchi ili wapate tiba sahihi kutoka taasisi sahihi kama Bugando, kwani tumeshuhudia matangazo mengi, hasa kwenye mitandao ya kijamii watu wanasema wana uwezo wa kumaliza vitambi kwa dawa ambazo sina uhakika kama zimethibitishwa na mamlaka husika.”