Undani wa Tundu Lissu kupigwa risasi

Muktasari:

  • Taarifa zilizopatikana baada ya tukio hilo zilisema kwamba mbunge huyo wa Singida Mashariki alijeruhiwa tumboni na mguuni na alipelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma ambako alifanyiwa upasuaji na hali yake kuelezwa kwamba inaendelea vizuri.

Dodoma. Mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amenusurika kifo baada ya watu wasiojulikana kumshambulia kwa risasi jana mchana akiwa ndani ya gari, nje ya nyumba yake katika eneo la Area D, Site 3 mjini Dodoma.

Taarifa zilizopatikana baada ya tukio hilo zilisema kwamba mbunge huyo wa Singida Mashariki alijeruhiwa tumboni na mguuni na alipelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma ambako alifanyiwa upasuaji na hali yake kuelezwa kwamba inaendelea vizuri.

Picha za gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser VX, zilizopigwa baada ya tukio hilo, zinaonyesha likiwa na matundu zaidi ya 25 ya risasi; kwenye tairi la mbele upande wa abiria, na sehemu mbalimbali za upande huo ambao ndiyo aliokuwa amekaa mbunge huyo.

Dakika chache baada ya kufikishwa hospitalini hapo, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah na viongozi wengine wa ulinzi wa Bunge, Chadema, Ukawa wakiwamo, wabunge Kunti Kajala (Viti Maalumu), Cecil Mwambe (Ndanda), John Heche (Tarime Vijijini) walifika kufuatilia hali yake.

Pia, ndugu na baadhi ya wagonjwa walianza kufurika katika chumba cha upasuaji cha hospitali hiyo huku baadhi wakionekana kulia.

Kadri taarifa za tukio hilo zilivyokuwa zikisambaa, ndivyo watu walivyokuwa wakifurika hospitalini hapo hali iliyomlazimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, James Charles na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kufanya kazi ya kuwatuliza na kuwataka waondoke eneo hilo huku baadhi wakikataa.

Baadaye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Gilles Muroto na Dk Charles waliitisha mkutano wa waandishi wa habari kuzungumzia tukio hilo.

Muroto alisema mara baada ya kupata taarifa hizo walifika eneo la tukio na kuanza uchunguzi, “Tunaomba mwananchi wenye taarifa atusaidie. Jeshi la Polisi tumeanza uchunguzi, tumefika eneo la tukio na tunaendelea.”

Alisema taarifa za awali zimeeleza kuwa kuna gari lililokuwa likimfuatilia Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), aina ya Nissan la rangi nyeupe.

Rugimbana aliwataka wananchi kuwa watulivu na kusubiri taarifa za Polisi na madaktari wanaoendelea na matibabu ya mbunge huyo huku Dk Charles akisema Lissu yu hai na imara na kwamba amepigwa risasi tumboni.

“Tumempokea mchana (jana), kanuni za matibabu haziruhusu mtu mwingine asiye mtumishi kuingia chumba cha matibabu. Tuna uwezo wa kutosha wa kutoa huduma ya dharura,” alisema Dk Charles.

Licha ya kauli hizo, mamia ya watu waliendelea kukusanyika nje ya chumba cha upasuaji katika hospitali hiyo wakisubiri kusikia kinachoendelea.

Miongoni mwao walikuwamo wabunge mbalimbali ambao walikuwa katika makundi wakizungumzia tukio hilo.

Ndani ya mkusanyiko huo, walikuwamo pia askari kanzu na wengine waliokuwa na silaha katika maeneo mbalimbali ya hospitali. Karibu na lango kuu la kuingilia, kulikuwa na gari la polisi lililokuwa limejaa askari wenye silaha.

Ilivyokuwa

Akisimulia tukio hilo, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini alimkariri dereva wa Lissu akieleza kwamba watu wasiojulikana waliokuwa katika gari walianza kuwafuatilia tangu wanatoka bungeni hali iliyomtia shaka dereva.

Alisema licha ya kuwatilia shaka, waliendelea na safari yao na walipofika nyumbani, dereva huyo alimsihi Lissu asishuke katika gari.

“Hao watu walipoona hawashuki walijifanya kuna kitu wanaangalia, walivyoona kuna utulivu walisogeza gari lao ambalo linasemekana ni ‘tinted’ na kuanza kurusha risasi upande wa Lissu,” alisema Selasini.

Mbali ya maelezo ya Selasini, wakazi wa Area D waliokuwa karibu na eneo anakoishi Lissu ambako kunafahamika kama maghorofa ya Site 3, ambayo ni makazi ya viongozi walieleza kupata mshtuko mkubwa baada ya kusikia milio ya risasi.

Wakazi hao ambao hata hivyo hawakutaka kutajwa majina yao gazetini walisema walisikia milio ya risasi katika nyumba hizo na baada ya sekunde chache wakasikia vilio vya watu. Wapo waliokimbilia katika eneo hilo lakini wengine walihofia na kujifungia ndani kwa kuhofia usalama wao. “Mimi niliona gari nyeupe ‘tinted’ ikipita kwa mwendo wa kasi hapa baada ya tukio tu kutokea, nadhani litakuwa ndiyo hiyo lilikuwa linatoka katika tukio,” alisema mkazi mwingine.

Muda mfupi baada ya polisi kufika katika eneo la tukio hakuna mtu aliyeruhusiwa kuingia isipokuwa kwa watu wanaoishi katika maghorofa hayo.⁠⁠

JPM, CCM, Chadema wazungumza

Rais John Magufuli kupitia ukurasa wake wa twitter alisema, “nimepokea kwa masikitiko tukio la kupigwa risasi kwa Mh. Tundu Lissu, namuombea Mwenyezi Mungu aweze kupona haraka. Aidha vyombo vya dola viwasake wote waliohusika na tukio hilo la kinyama na kuwafikisha katika mikono ya sheria.”

Awali, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kikisema kimepokea kwa mshtuko taarifa ya kupigwa risasi kwa mwanasheria wake mkuu.

“Chadema tunalaani vikali kitendo hicho na tunafuatilia kwa karibu hali yake,” imesema taarifa hiyo iliyotolewa na Kurugenzi ya Uenezi, Mawasiliano na Uhusiano wa Nje ya Chadema makao makuu.

Akiwa hospitalini, Mbowe alisema, “huu si wakati wa kunyosheana vidole, ninaamini vyombo vya dola vitafanya kazi na vikimaliza vitatoa taarifa.”

Pia, Chama cha Mapinduzi (CCM), kilitoa taarifa kikielezea kushtushwa na tukio hilo na kulitaka Jeshi la Polisi, “kuwatafuta, kufanya uchunguzi wa tukio hili na kuchukua hatua kali za kisheria kwa wote waliohusika na kitendo hiki cha kidhalimu.

“Uongozi wa Chama cha Mapinduzi unamuombea ndugu Lissu kupona haraka na afya njema ili aendelee na majukumu yake ya kibunge.”

Kadhalika, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), nao ulitoa taarifa ukisema umepokea kwa mshtuko taarifa za Lissu kupigwa risasi.

“Tunatoa pole kwa familia ya Lissu, wananchi wa Singida Mashariki, wanachama wa TLS na Watanzania kwa jumla,” inasema sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Mratibu wa mtandao huo, Onesmo ole Ngurumwa ikiwataka pia kumuombea apone haraka.

Viongozi wamiminika hospitalini

Hadi kufikia saa 10 jioni jana, zaidi ya viongozi wanne wakiongozwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai walikuwa wamefika hospitalini hapo kufuatilia hali ya Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Ndugai alifika hospitalini hapo muda mfupi baada ya kuwasili akitokea Dar es Salaam ambako alikwenda kukabidhi kwa Rais John Magufuli, ripoti mbili za uchunguzi wa madini ya almasi na Tanzanite uliofanywa na Bunge.

Mbali ya viongozi hao wa Bunge, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba pia alifika hospitalini hapo na baadaye kusema amepokea kwa masikitiko makubwa tukio hilo alilolielezea kuwa ni shambulio baya kutokea nchini tena kwa kiongozi. Alisema iwe limefanyika kwa sababu za kisiasa, hujuma, ujambazi au ugomvi, Serikali itapambana nalo kwa nguvu zake zote na kuhakikisha waliohusika wanapatikana.

Alisema mara baada ya kutokea kwa tukio hilo, aliagiza polisi kuweka vizuizi katika njia zote zinazotoka na kuingia Dodoma ili kuhakikisha waliofanya tukio hilo ambao alisema wanataka kuitia doa Tanzania, hawapati mwanya wa kutoroka.

“Tunalaani, tulio hili. Halikubaliki, tutawasaka kuhakikisha kuwa tunawakamata na sheria inafuata mkondo wake. Kubwa Watanzania tumuombee apate afya njema na aweze kurejea katika shughuli zake za kawaida.”

Akizungumzia hali ya Lissu, Ummy alisema madaktari walichofanya kwanza ni kuhakikisha kuwa mgonjwa anakuwa na utengamano wa afya kwa kudhibiti damu kuendelea kuvuja hatua ambayo alisema imefanikiwa kikamilifu na kwamba madaktari bingwa akiwamo katibu mkuu wa wizara yake, Mpoki Ulisubisya, ambaye ni daktari wa usingizi walikuwa wakiendelea na hatua ya pili ambayo ni upasuaji.

Alisema mara baada ya kukamilika kwa hatua hiyo, madaktari watashauri kupitia ripoti yao kama Lissu apelekwe hospitali ya rufaa ambayo ni ya Taifa ya Muhimbili

Huku akisisitiza kuwa madaktari wanaomtibu wana uwezo na kumhakikishia Spika Ndugai ambaye tukio hilo limemshtua moyo kuwa wamedhamiria kuhakikisha kuwa wanaokoa maisha ya Lissu.

Spika alisema Bunge litatoa kila aina ya msaada kuhakikisha kuwa afya ya Lissu inatengamaa na kuwatoa hofu wapigakura wa Singida Mashariki, ndugu na jamaa kuwa mbunge wao yuko salama huku naye pia akiwataka Watanzania wote kumuombea Lissu ili afya yake itengamae na kurudi katika shughuli zake za kila siku.

Mpaka tunakwenda mitamboni kulikuwa na taarifa kuwa mbunge huyo alikuwa akifanyiwa mpango wa kuhamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).