UoI: Wanafunzi walioghushi kufukuzwa chuo ikiwa hawatalipa ‘fidia’

Iringa. Chuo Kikuu Iringa (UoI) kimejitenga na taarifa za madai ya kuwa na mfumo dhaifu wa ulipaji wa ada za wanafunzi, huku Mkuu wa chuo hicho Profesa Ndelerio Urio akisema wote waliohusika kupotosha ankara zao, watafukuzwa iwapo watashindwa kulipa fidia.

Hivi karibuni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Maimuna Pathan, akiwa Bungeni; alidai uongozi wa chuo hakuwa makini na hivyo kusababisha upotevu wa fedha, huku kikiwafukuzwa wanafunzi waliobanika kughushi malipo.

Kufuatia kauli hiyo, Mwananchi Digital imefanya mahojiano na Profesa Urio mifumo ya kiuongozi na ile ya malipo chuoni hapo, bado iko imara na kwamba kilichotokea ni kwa baadhi ya wanafunzi kughushi malipo na hivyo kukiibia chuo kupiti mfumo uliokuwepo awali.

“Wanafunzi waliingilia mfumo, waghushi malipo ya ada na hivyo kuonekana hawadaiwi. Hii imekikosesha UoI mamilioni ya shilingi. Pia wanadaiwa kughushi stakabadhi za malipo na mihuri ya benki ili kuridhisha kuwa hawadaiwi ada,” amesema Profesa huyo.

Kwa mujibu wa uchunguzi ulifanywa na gazeti hili na kuthibitishwa na uongozi wa chuo, imebainika wanafunzi waliofanya hujuma hiyo ni wale wanaosomea cheti na shahada ya awali (bachelor) hali ambayo imeleta taharuki kubwa chuoni hapo.

Taarifa zinatanabaisha kuwa ada wanayopaswa kulipa wanafunzi wanaosomea kwa mwaka katika ngazi za cheti (certificate) ni Sh840, 000 huku wale wanaosomea shahada kwanza wakitakiwa kulipa Sh1, 670,400 katika mwaka wao wa kwanza.

Huku Sh.1, 610,400 na Sh1, 760,400 zikitakiwa kulipwa mwaka wa pili na wa tatu wa masomo chuoni hapo.

Mfumo wa SAMIS unaodaiwa kuingiliwa na wanafunzi hao unatumika na chuo hicho katika masuala ya malipo ya ada, kuweka kumbukumbu za wanafunzi na masomo.

Profesa Urio alikiri juu ya tatizo hilo kutokea na kwamba uongozi ulichukua hatua kwa kuunda tume ya watu wanne ambao wanaendelea kuchunguza.

Hata hivyo Mkuu huyo wa UoI ameiambia Mwananchi Digital kuwa uchunguzi wa awali uliofanywa ulibaini wanafunzi 262 ndio walihusika katika kadhaa hiyo ambao baada ya kufanikiwa na ukaonyesha wamelipa ada, waliruhusiwa kufanya mitihani kabla chuo hakijashtukia hujuma hiyo.

"Baada ya kuwabaini wanafunzi waliofanya hujuma hiyo huku wakiwa tayari walishafanya mitihani, tumezuia matokeo yao hadi watakapolipa ada kamili wanayodaiwa," alisema Profesa Urio

“Tumeandaa taarifa itakayo wasilishwa kwa Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema.

Mhasibu na msimamizi wa malipo ya chuoni hapo, Jackson Kapinga ameweka wazi kiasi kinachosadiwa kuibwa kutokana na hujuma hiyo kuwa ni Sh100 milioni na kwamba vikao halali vya chuo hicho vimewataka wanafunzi husika kulipa fidia zote kutokana na makosa yao.

Kapinga meongeza kwa kusema kwamba japo wanafunzi wengine waliohsika kwenye kadhaa hiyo Tayari wameishlipa ada zao, ni 54 ndiyo wanaonekana kukaidi agizo hilo na kwamba uongozi wa chuo unatarajia kuwafukuza iwapo wataendelea kusita kufanya malipo hayo.

Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho wametoa maoni mseto na kusema kuwa uongozi wa chuo hicho ujitathimini kwani mifumo yake ya ulipaji ada ingekuwa imara, ni wazi kusingetokea shida kama hiyo.

Kwa nyakati tofauti, wanafunzi hao wamefafanua kwamba madhaifu hayo yaliyojulikana toka mwaka jana, na kwamba dhahiri hata wanafunzi waliomaliza, huenda walishawahi kufanya hujuma kama hiyo bila uongozi kutambua.

Kwa upande mwingine, wanafunzi hao wameomba uongozi wa chuo kuwa makini hata na wahasibu na wasimamizi wa fedha chuoni hapo ili kuepusha changamoto kama hizo kutokea.

Wanafunzi hao wamemaliza kwa kueleza kwamba Wanafunzi waliogushi malipo ni Bora wafukuzwe na sio kuwatetea kitu ambacho kinaweza kusababisha chuo kuwa na sifa mbaya.

Nao baadhi yao wameeleza kwamba chuo kimejitahidi mpaka kuwapata Wanafunzi waliogushi malipo hayo na kuwalipisha fidia hizo ili kuepuka kuleta hasara kwa chuo hicho.

"Chuo Kikuu cha Iringa kilipatwa na adha hiyo lakini kuna mambo wanafunzi waliosababisha hayo wamelipishwa fidia hata hivyo, uongozi unatakiwa kujitathimini na kama kuna shida yoyote ifanyiwe kazi kwa uharaka," alisema mmoja wa wanafunzi hao ambaye hakupenda jina lake lifahamike. 

Mwisho...