Upelelezi kesi anayedaiwa kumuua mumewe bado
Muktasari:
- Kesi ya mauaji inayomkabili mkazi wa Katanini, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Beatrice Elias (36) anayetuhumiwa kumuua mumewe, Evagro Msele (43) imeahirishwa kwa mara ya nne mfululizo, kwa maelezo upelelezi haujakamilika.
Moshi. Kesi ya mauaji inayomkabili mkazi wa Katanini, Manispaa ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro, Beatrice Elias (36), anayetuhumiwa kumuua mumewe, Evagro Msele (43) imeahairishwa kwa mara ya nne mfululizo, kwa maelezo kuwa upelelezi haujakamilika.
Msele, mfanyabiashara maarufu mjini hapa, anadaiwa kuuawa usiku wa Mei 25, 2024 katika Kitongoji cha Pumuani A, baada ya mwanamke huyo kudaiwa kumvizia akiwa nyumbani kwa mzazi mwenzake na kumshambulia kwa kitu kinachodhaniwa kuwa ni kisu.
Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Juni 10 2024 akikabiliwa na kesi ya mauaji namba 15731/ 2024, mbele Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Herieth Mhenga na kusomewa mashtaka yake na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Henry Daudi.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Betrina Tarimo ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi leo Julai 22, 2024 kuwa upelelezi haujakamilika wakati kesi hiyo ilipotajwa mahakamani hapo.
Hakimu huyo ameahirisha kesi hadi Agosti 6, 2024 itakapotajwa tena.
Kwa mara kadhaa mshitakiwa huyo, amekuwa akitinga mahakamani hapo akiwa amevalia vazi la Nikabu ambalo hufunika mwili mzima kuanzia kichwani hadi miguuni huku baadhi ya ndugu wa mwanaume wakitamani kuona sura yake lakini inashindikana.
Tangu shauri hilo lifikishwe mahakamani hapo ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu wamekuwa wakionekana ndani na nje ya viunga vya Mahakama hiyo wakiwa makundi kwa makundi.
Pamoja na ndugu hao, pia baadhi ya watoto wa mshtakiwa huyo wamekuwa wakifika mahakamani hapo kumjulia hali mama yao.