Polisi yakana kumshikilia ‘mchepuko’ wa Msele, kuzikwa Jumamosi
Muktasari:
- Beatrice Elias (36), mkazi wa Mtaa wa Katanini Wilaya ya Moshi anatuhumiwa kumuua mumewe, Ephagro Msele (43) kwa madai ya kumkuta kwa mzazi mwenzake.
Moshi. Wakati taarifa zikisambaa maeneo mbalimbali Mjini Moshi za kukamatwa kwa mwanamke aliyezaa na Ephagro Msele anayedaiwa kuuawa na mkewe Beatrice Elias (36) baada ya kumfuma naye, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema taarifa hizo hazina ukweli wowote.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo, Mei 28, 2024, Kamanda Maigwa amesema watu wapuuze taarifa zinazoendelea kuzagaa kwa kuwa Polisi hawawezi kumshikilia mtu ambaye hajatenda kosa.
“Sasa tumshikilie huyu mama kwa kosa gani, mwenye kosa ni yule aliyevamia nyumbani kwa mwenzake a kufanya hicho alichokifanya na huyo ndiye ambaye tunamshikilia,” amesema Kamanda Maigwa.
Akijibu ni lini watamfikisha Beatrice Mahakamani, kamanda huyo amesema bado wanaendelea na uchunguzi, ukikamilika, atafikishwa kortini.
Maziko ya Msele
Mwananchi Digital imefika nyumbani kuliko na msiba wa mfanyabiashara huyo na kukuta ndugu waakiendelea na maandalizi ya maziko ya ndugu yao huyo.
Baba mdogo wa marehemu, Damian Msele amesema ndugu yao atazikwa Jumamosi Juni Mosi, 2024 na ibada ya kumuaga itafanyia katika Kanisa Katoliki la Karanga lililopo Manispaa ya Moshi kuanzia saa sita mchana.
"Ndugu yetu atazikwa hapa nyumbani siku ya Jumamosi na ibada ya misa ya kumuaga ndugu yetu itafanyika katika Kanisa la Karanga jirani kabisa na hapa nyumbani kwetu Katanini," amesema Msele.
Mauaji yalivyotokea
Kwa mujibu wa watu wa karibu na Msele, Mei 25, 2024, Beatrice baada ya kutoka msibani alikokuwa na mumewe, alimfuatilia kila anapokwenda kwa kutumia usafiri wa bodaboda na baada ya mumewe kuegesha gari lake mahali, alidaiwa kwenda nyumbani kwa mwanamke aliyezaa naye.
Inadaiwa kuwa, Beatrice alipofika nyumbani kwa mwanamke huyo, Kitongoji cha Pumuani A, alijificha getini na baadaye aligonga geti na mumewe ndiye aliyetoka kumfungulia.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa baada ya kukutana getini, yaliibuka mabishano kati yao, ndipo Beatrice alipofanikiwa kutekeleza tukio hilo.
Kamanda Maigwa alidai Beatrice alimvizia mumewe akitoka nyumbani kwa mzazi mwenzake na kumchoma na kitu chenye ncha kali.
Alisema polisi waliofika eneo la tukio walikagua mwili na kubaini mwanaume huyo alichomwa na kisu mgongoni.
Alisema wakati polisi wanatafuta kisu kilichotumika kwa mauaji walikukuta ndani ya pochi ya mwanamke huyo kikiwa kimefichwa pamoja na simu na pochi ya mwanaume ambapo polisi waliondoka na mwanamke huyo pamoja na mwili wa mumewe.