Upungufu nguvu za kiume tishio kwa vijana chini ya miaka 35

Imeelezwa kuwa matatizo ya kisaikolojia yanayoendana na msongo wa mawazo yanayowakumba zaidi wanaume chini ya umri wa miaka 35, yamekuwa chanzo cha kuwepo kwa upungufu wa nguvu za kiume.

Hata hivyo madaktari wameonya kwamba kila tatizo lina chanzo chake, hivyo si sahihi kwa mwathirika kujitibia kwa dawa yoyote kabla ya kuonana na wataalamu ili kujua kisababishi na kutibu tatizo husika.

Akizungumza na Mwananchi, Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo, Obadia Nyongole anasema upungufu wa nguvu za kiume una sababu tofauti.

“Watu wanachanganya kati ya upungufu wa nguvu za kiume na kukosa hamu ya tendo la ndoa hivyo ni vitu viwili tofauti, mwanaume anaweza akawa na nguvu za kiume lakini anakosa hamu ya tendo la ndoa,” anasema.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Pedro Pallangyo ameeleza kuwa idadi kubwa ya wagonjwa wanasumbuliwa na tatizo kubwa la shinikizo la damu na kisukari, wengi wao wanapungukiwa nguvu za kiume.

”Hali hii inaashiria kuwa magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu yamekuwa yakiongezeka mara kwa mara jambo ambalo linasababisha athari ya nguvu za kiume kuwa kubwa,” anasema Dk Pallangyo.

Dk Nyongole ambaye pia ni Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) anasema kwamba zipo aina mbili za kukosa nguvu za kiume ipo inayotokana na matatizo mbalimbali ya kimwili ambayo husababishwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo homoni ambazo husababisha wengine kuwa na homoni za kike.

Anasema wapo wanaokuwa na ukosefu wa nguvu za kiume kutokana na matatizo ya kiafya yaliyopo kwenye miili yao na wapo ambao wanakuwa na ukosefu wa nguvu za kiume kutokana na matatizo ya kisaikolojia ikiwemo msongo wa mawazo.

“Kwa hili la ukosefu wa nguvu za kiume linalotokana na matatizo ya kisaikolojia au yanayoendana na msongo wa mawazo hili linawakumba zaidi wanaume hasa wale walio chini ya umri wa miaka 35.

“Haimaanishi kwamba linaweza kuwakumba wanaume wenye huo umri pekee, ila waliopo kwenye umri wa kuzaa mwingine anakuwa na msongo wa mawazo labda hana mahusiano mazuri kwenye ndoa yake au kazi inamkosesha hamu ya tendo la ndoa hivyo inapunguza nguvu za kiume.”

Dk Nyongole anasema kwamba tatizo hilo huwakuta zaidi watu ambao bado ni vijana lakini hawana magonjwa mengine ya kimwili zaidi ya yale ya kisaikolojia.

“Mara nyingi utakuta labda mahusiano yaliyopo kwenye ndoa hayamridhishi, kubadilika kwa mfumo wa maisha, walikuwa wanaheshimiana sasa heshima hakuna, mama alikuwa anajiweka vizuri lakini sasa hivi hajiweki vizuri, mfano anaweza akasikia harufu ya ‘perfume’ kwa mwenzake lakini asiipende, basi hamu inamuisha kabisa.”

Anasema kwamba kuna wakati mmoja kati yao akahitaji zaidi lakini kimazingira hawajaandaana vizuri, “Mama akisema siku hizi huniridhishi basi anapata wasiwasi na msongo wa mawazo unaingia baada ya hapo anakuja kumaliza haraka kwa sababu anafanya kwa ajili ya kufanya na si kwamba anafurahia tendo.”

Hata hivyo anaongeza kwamba kuna ukosefu wa nguvu za kiume unaotokana na magonjwa mbalimbali ikiwemo matatizo ya kiafya kama kisukari, presha, magonjwa ya figo au mhusika alishawahi kupata ajali inayohusisha maungo ya uume.

Anasema wakati mwingine mwanaume anaweza kuwa na matatizo ya magonjwa yanayohusisha madhara ya kwenye mishipa midogomidogo ya kwenye damu inayosababisha uume usiweze kusimama vizuri akafanya tendo la ndoa vizuri.

“Wapo wengine ambao wana matatizo ya magonjwa ya moyo yanayofanya mishipa ya damu ijae mafuta zaidi na kuathiri mzunguko wa damu au ana dawa anazotumia za presha kisukari zinazomletea hayo matatizo na mwingine ana matatizo ya ukosefu wa nguvu za kiume kutokana na magonjwa au dawa anazotumia,” anasema.

Utafiti

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile anasema Serikali imeamua kufanya utafiti wa tatizo la ukosefu wa nguvu za kiume kwa wanaume kwa sababu kwa muda mrefu wamekuwa wakitafuta suluhisho kwa kificho na hivyo kukosa taarifa sahihi.

Dk Ndugulile amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Mpoki Ulisubisya kushirikiana na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kufanya utafiti wa afya ya uzazi kwa wanaume ili kubaini sababu ya ongezeko la upungufu wa nguvu za kiume ni kubwa kwa kiasi gani nchini.

Hata hivyo anasema kwa kipindi kirefu Serikali imekuwa ikitilia mkazo afya ya uzazi kwa wanawake na tafiti nyingi zimekuwa zikihusu upande huo mmoja.

Alisema mpaka sasa bado haujafanyika utafiti kuhusu hali ya afya ya uzazi kwa wanaume, japo tatizo hilo linazungumzwa miongoni mwa wanajamii.

“Bado hatujafanya utafiti wa kina kujua tatizo hili ni kubwa kwa kiasi gani, suala hili ni gumu kulisemea kwa maana ukiangalia takwimu ya uzazi Tanzania kwa maana ya ongezeko la watu na idadi ya kinamama kukua unaona kabisa kwamba bado hatuna shida,” anasema na kuongeza:

“Tatizo hili sisi wenyewe tunachangia kwa kula bora chakula na si chakula bora hasa vyakula vyenye mafuta kwa wingi, sukari vinachangia sana katika magonjwa yasiyo ya kuambukiza pamoja na kupungua kwa nguvu za kiume, kutofanya mazoezi, matumizi ya vilevi ikiwemo pombe na sigara navyo ni visababishi vikuu,” anasema Dk Ndugulile.

Kufuatia hilo, Dk Nyongole anasema kwa Serikali kuamua kulifanyia utafiti tatizo hilo, kutaibua tiba maalum kwani nchi itajua hasa nini kiini cha tatizo hilo.

“Ni suala zuri kwa sasa lakini ni namna tu ya kujua kwamba wanatarajia utafiti huu ufanyike kwa njia gani na kwa wakati gani na baada ya muda gani au lini tutarajie majibu,” anasema na kuongeza, “baada ya majibu sisi kama wataalamu tutakuja na kusema kilichoonekana kinamaanisha nini na nini kifanyike.”

Mapema wiki hii Serikali imetangaza rasmi kuzitambua aina tano za dawa za asili baada ya kuzikagua ikiwemo ‘Ujana’ inayodaiwa kutibu nguvu za kiume.

Dawa hizo zilizotangazwa juzi kupitia mkutano wa vyombo vya habari, zimetajwa kuwa ni Ujana, IH Moon, Coloidal Silver, Sudhi na Vatari.

Msemaji wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Gaudensia Simwaza alisema hadi sasa dawa ambazo zimesajiliwa na mamlaka hiyo baada ya kuchunguzwa na kuonekana zinafaa kutumiwa na binadamu ni aina mbili.

“Kuna dawa aina mbalimbali zikiwemo Sildenafil pamoja na tadalafil zinazotoka nchi mbalimbali ambazo zimechunguzwa na TFDA na kuonekana hazina sumu wala madhara kwa watumiaji, hizi zinapatikana katika maduka mbalimbali ya dawa za binadamu,” alisema Simwaza.