Prime
Upungufu wa ardhi unavyokuwa tishio
Dar es Salaam. Kasi ya mahitaji ya ardhi isiyoendana na uandaaji na utekelezaji wa mipango ya matumizi yake ya muda mrefu imeelezwa tishio jipya litakalochochea migogoro ya ardhi kwa miaka ijayo, endapo hakutakuwa na sera za kupunguza tatizo hilo.
Kwa mujibu wa wizara yenye dhamana na ardhi, asilimia 25 tu ya ardhi nchini (kilometa 945,087 za mraba) ndizo zilizogawanywa katika makundi sita ya mipango ya matumizi ama ngazi ya vijiji, wilaya, hifadhi na misitu. Vijiji 2,680 kati ya vijiji 12,318 ndivyo vyenye mpango huo wa matumizi ya ardhi.
Mgawanyo huo wa mwaka 2012 kwa ardhi ya Tanzania bara, unaonyesha eneo la misitu, vyanzo vya maji na hifadhi lilitengewa asilimia 51.7 ya ardhi nzima na asilimia 48.3 iliyobaki ni kwa ajiri ya shughuli za binadamu kama makazi, kilimo na madini, malisho na uwindaji.
Hata hivyo, ushahidi unaonyesha huenda eneo linalochukua asilimia 51.7 likaendelea kuongezewa kutoka kwenye eneo la la shughuli za binadamu kutokana na ongezeko la hifadhi, kama zilivyoongezeka sita mwaka 2019, bila kujali kasi ya ukuaji wa miji (asilimia 4.8 kila mwaka), unaoathiriwa pia na mahitaji ya ardhi.
Wakati hali ikiwa hivyo, idadi ya watu inakadiriwa itafikia milioni 129.4 mwaka 2050, wakati huo Serikali ikipunguza uwiano wa gawio la ardhi kwa kila Mtanzania kutoka ekari 2.5 mwaka 2012 hadi ekari 1.5 mwaka jana, huku ikihamisha ujenzi wa magorofa yanayohusisha ardhi kidogo kwa makazi mengi.
“Ni kweli kuna changamoto, ndiyo maana sera yetu ya ardhi ya mwaka 1995 na Sera ya Maendeleo ya Makazi ya 2000 zote tumezifanyia marekebisho kwa mwa mwaka huu,” anasema Deogratius Kalimenze, mkurugenzi wa idara ya maendeleo ya makazi katika Wizara ya Ardhi.
“Hizo sera zinashawishi uwekezaji wa sekta binafsi kujenga apartments (makazi ya kaya nyingi) ili kupunguza gharama za Serikali kutoa huduma na kupunguza kasi ya mahitaji ya ardhi. Changamoto ni kwamba kila mtu anataka kumiliki ardhi kwa sasa. Tunatoa elimu kwa umma kubadili mtazamo huo,” alisema.
Changamoto hiyo inaakisi takwimu za matokeo ya sensa ya watu na makazi mwaka 2022, zinazoonyesha kati ya majengo 13,907,951 ya Tanzania bara, magorofa ni 61,258, sawa na asilimia 0.4, huku asilimia zaidi ya 99 yakiwa majengo ya kawaida yanayotumia ardhi kubwa.
Ili kupunguza athari za upungufu wa ardhi, Kalimenze anatoa wito kwa mamlaka za upangaji miji katika kila halmashauri kutafuta na kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya upangaji na upimaji wa ardhi na kudhibiti ujenzi wa makazi holela.
“Changamoto ni bajeti. Halmashauri za miji zenye master plan (mpango mkuu wa mji) ni 27 kati ya 47 na tunatumia kati ya Sh250 milioni hadi Sh700 milioni kuandaa kila mji, pia halmashauri za wilaya chini ya 20 kati ya 137 ndiyo zina mipango ya uendelezaji wa matumizi ya ardhi na bajeti yake ni Sh150 milioni hadi Sh300 milioni,” anasema Kalimenze.
Hii inamaanisha kwamba, halmashauri hizo zinataji takriban Sh40 bilioni kuhakikisha ardhi yote nchini inapangwa, kupimwa na kugawanywa kwa ajili ya matumizi bora na hivyo kuondoa migogoro, kwa mujibu wa Kalimenze.
Watalaamu wa masuala ya sera na mipango wanashauri Serikali iiwezeshe wizara hiyo kibajeti ili iweze kutekeleza mipango hiyo ambayo ni kipaumbele kwenye mipango ya maendeleo inayohitaji ardhi iliyopangwa.
“Hizo fedha ni kidogo sana, kama Serikali iko makini na ikiamua inaweza kukopa au kupata msaada ili kuondoa tatizo hilo kwa kuwa gharama za migogoro ni kubwa kuliko hizo pesa. Tatizo ni kukosa nia, si uwezo,” anasema Onesmo Olengurumwa, mratibu kitaifa wa mtandao wa watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC).
Hata hivyo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula anasema kuna matumaini ya kupunguza migogoro nchini kupitia mradi wa miaka mitano wa Sh345 bilioni utakawezesha kupima na kumilisha ardhi katika vijiji vyote vya halmashauri 44 nchini.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti na Utetezi wa Haki za Ardhi (LARRRI/HakiArdhi), migogoro ya ardhi husababishwa na kutofahamika kwa sheria, upungufu katika sera na sheria, kupanuka kwa miji, ongezeko la watu na mifugo na kugunduliwa kwa maliasili mpya kama vile madini na vito.
“Tusipochukua hatua mapema, hali itakuwa mbaya huko tuendako. Wanyamapori wanaendelea kuingia kwenye makazi na wananchi wanazidi kupanua shughuli za kiuchumi mpakani kabisa mwa hifadhi na kwenye shoroba za wanyamapori,” anasema John Noronha, mshauri mwandamizi wa masuala ya maliasili na mazingira.
Takwimu zinaonyesha wastani wa raia mmoja hufariki dunia kila baada ya saa 52 kwa kujeruhiwa na wanyamapori huku ekari 16 za mazao ya chakula zikiharibiwa.
Kiini cha tatizo
Mchambuzi wa taarifa za mifumo ya kijiografia kutoka Chuo cha Ardhi Morogoro, Colman Charles anasema kiini cha tatizo ni kukosekana mipango ya muda mrefu katika ardhi iliyopimwa kwa makadirio yanayoakisi kasi ya ukuaji wa mahitaji ya miaka ijayo, hatua anayosema itachochea migogoro zaidi.
“Tatizo si ukosefu wa mipango ya muda mrefu tu ila lazima uwe na makadirio ya ukuaji wa mahitaji ya ardhi, kwamba eneo hili kwa idadi ya wafugaji miaka kadhaa ijayo wataingia wangapi na eneo nyeti lenye migogoro ni dogo kuliko eneo lililobakia wazi,” anasema Charles.
Kuhusu miji, Charles anashauri kutekeleza kwa vitendo mpango wa kitaifa unaohusisha mfumo wa ujenzi wa eneo dogo la ardhi na endelevu pamoja na kupanua huduma za msingi maeneo ya pembezoni mwa miji.
“Uingereza iliamua kuijenga London kwa mfumo huo na imefanikiwa sana.”
Tunapoza vidonda
Athari za kukosekana mipango ya muda mrefu zimeanza kubadili uamuzi wa Serikali baada ya wiki chache zilizopita Bunge kuridhia Azimio la kufuta Hifadhi ya Taifa Kigosi, hatua itakayonufaisha kaya 113,547 katika vijiji 126 vya mikoa mitano ya Geita, Kagera, Kigoma, Shinyanga na Tabora.
Pamoja na hilo, jamii inalipia gharama za matukio ya uvamizi wa wayama. Kwa mfano, mwaka 2016/17 wanyamapori 833 walivamia makazi, mwaka 2017/18 idadi hiyo ilipanda hadi 997 na mwaka 2018/19 wakawa 1,510.
Ripoti mpya ya tathmini ya shoroba za wanyamapori ya mwaka 2022, inaonyesha kwamba eneo lilizotengwa kwa ajili ya mtandao wa wanyamapori, hadi kufikia mwaka jana asilimia nane zilikuwa zimegeuzwa kwa ajili ya shughuli za kilimo na asilimia moja makazi katika kujaribu kupunguza migogoro.
Hata hivyo, Dk Elikana Ngallaba, meneja ushirikishwaji wa Sekta binafsi katika Mradi wa USAID, Tuhifadhi Maliasili, anasema miongoni mwa maeneo yaliyofanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa migogoro ni pamoja na Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (WMAs), hususani kwa wananchi walioona faida yake.
Mwongozo wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) wa ushirikishwaji katika kupanga matumizi ya ardhi ili kudumisha uhusiano kati ya jamii, ufugaji na wanyamapori unashauri Serikali kusaidia bajeti ya uandaaji wa WMAs zinazogharimukati ya dola 100,000 hadi 250,000.
Tishio la kimahitaji
Tishio hilo linachagizwa na ongezeko la idadi ya watu kutoka milioni 12.3 mwaka 1967 hadi milioni 61.7 mwaka jana, sawa na ongezeko la watu milioni 49.4 ndani ya miaka 55.
Ushahidi mwingine wa kitakwimu wa Wizara ya Mifugo kati ya mwaka 2006/07 na 2020/21 ni idadi ya mifugo iliongezeka kutoka ng’ombe milioni 18.5 hadi milioni 33.9, mbuzi kutoka milioni 13.1 hadi milioni 24.5, kondoo kutoka milioni 3.5 hadi milioni 8.5, huku kuku wakitoka milioni 30 hadi milioni 87.7.
Kutokana na hali hiyo, Dk Onesmo Kyauke, mwanasheria na wakili wa kujitegemea anasema Serikali inalazimika kutumia mbinu mpya, akisema licha ya kuwepo sheria changamoto ni utekelezaji.
“Kwa mfano tunajua mifugo inaongezeka. Tulazimishe kila mfugaji awe na mipaka yake ili afuge kisasa kwa sababu athari za kimazingira ni kubwa sana,” anasema.
Kuhusu hoja hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT), Jeremiah Wambura anasema Serikali imeshindwa kutekeleza kifungu cha 147 (ii) cha Ilani ya CCM kinachoelekeza kushajihisha utayarishaji na utumiaji wa malisho na vyakula bora vya kutosha vya mifugo.
“Sisi (wafugaji) tuko tayari kulipia gharama za kupimiwa ardhi lakini ni asilimia isiyozidi 10 tu ya halmashauri nchini ndiyo wametutengea maeneo ya malisho, licha ya kuendelea kutoa elimu ya ufugaji wa kisasa. Serikali itoe wataalamu sisi tutoe pesa kama kikwazo ni bajeti,” anasema Wambura.
Watalaamu wanasema wazo la kuanzisha Jumuiya za Hifadhi za wanyamapori (WMAs) na kijiji kupata mapato ya wanyamapori limepunguza migogoro ya wafugaji lakini eneo kinga (buffer zone) linaendelea kuvamiwa na wanavijiji kutokana na ukuaji wa mahitaji ya ardhi.
Tatu ni ushahidi wa ongezeko la tembo kutoka 43,330 mwaka 2014 hadi 60,000 mwaka huu. Pia faru weusi kutoka 163 mwaka 2019 hadi 238 mwaka jana, idadi ya Simba waliofikia 14,912 kidunia na twiga 24,000 kwa takwimu za Wizara ya Maliasili na Utalii.
Ongezeko la wanyamapori linathibitisha uanzishaji wa hifadhi mpya kutoka moja mwaka 1959 hadi tano ndani ya miaka mitano kabla ya kufikia 11 mwaka 1985, zikiwa na kilometa za mraba 12,818. Idadi hiyo iliongezeka hadi 22 mwaka 2019 zenye eneo la kilometa za mraba 102,891 ndani ya miaka 34.
Mkuu wa sehemu ya utangazaji utalii ikolojia kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Anna Lauwo anasema TFS inamiliki hekta milioni 14 kati ya hekta 48 za mistu zinazolindwa nchini huku zikiongezeka kutokana na upandaji wa miti bila kuingiliwa na shughuli za kibinadamu.
Kijamii, kiuchumi
Watalaamu na wasimamizi wa maliasili nchini wanasema gharama ya kutokuwa na mipango ya matumizi ya ardhi itasababisha mwenendo wa uvamizi wa maeneo ya shoroba za wanyamapori na hifadhi, hivyo kuwa tishio la viumbe kupotea na kupoteza asili ya vivutio vinavyosababisha ongezeko la watalii nchini.
Miongoni mwa ushahidi ni pamoja na tumbili ambao wamekuwa wakivamia mtaa wa Nandope FFU Manispaa ya Mtwara Mikindani na kusababisha uharibifu kwenye bustani za matunda na mbogamboga.
Pili, tangu Mei mwaka 2021 hadi sasa, makundi makubwa ya nyani, ngedere na tumbili kutoka katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro na hifadhi jirani ya nchini Kenya yamekuwa yakivamia mashamba na makazi ya watu wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro na kuharibu mazao na kula wanyama wafugwao.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), miongoni mwa changamoto inayohatarisha uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori na mazingira yao ni uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuli za kibinadamu, hususani mifugo, kilimo, uchimbaji madini na uvuvi haramu.
Mhandisi wa Viwanda, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Julius Enock anasema uharibifu wa mazingira unaosababisha mabadiliko ya tabianchi husababisha hasara ya Taifa.
Anasema wastani wa Sh5 trilioni kwa mwaka hupotea kutokana na uharibifu wa mazingira, ukame, magonjwa ya mazao, mafuriko kuharibu miundombinu.
Mfano mwingine wa gharama kiuchumi ni katika mgogoro wa ekari 6,000 za Kata ya Mabwepande kati ya Shirika la Maendeleo la Jiji la Dar es Salaam (DDC) na wananchi wanaoishi eneo hilo.
“Hao wananchi walinunua na kumilikishwa ardhi, lakini baadaye ikaibuka DDC na nyaraka pia, iliwezekanaje?Kwa hiyo unaweza kuwa na mipango mizuri lakini changamoto ikabakia kwenye uadilifu,” anasema Nicholas Lekule, mchambuzi wa sera kutoka asasi isiyo ya Serikali ya Policy Forum.
“Na hali inaonekana kuwa mbaya tuendako kwa sababu hatuna mipango ya muda mrefu inayoakisi mwenendo wa ukuaji wa mahitaji ya ardhi, inahitajika kazi ya kufanya mapitio upya ya kisera,” alisema.