Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Usafiri Dar-Bagamoyo sasa kwa boti ya kasi

Kivuko kilichopewa jina la MV Dar es Salaam, kimeletwa nchini jana kutoka Bangladesh kikiwa cha kwanza kwa mwendokasi kuliko vingine vyote nchini. Kina uwezo wa kubeba watu 300 waliokaa pamoja na mizigo.PICHA|MAKTABA

Muktasari:

Iliwasili nchini jana na itaanza kazi baada ya kuzinduliwa na Rais Jakaya Kikwete.

Dar es Salaam. Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam sasa wataanza kusafiri kwa kutumia kivuko cha kisasa kutoka katikati ya jiji hadi Bagamoyo na mikoa mingine badala ya kutumia usafiri wa barabara.

Kivuko hicho kilichopewa jina la MV Dar es Salaam, kimeletwa nchini jana kutoka Bangladesh kikiwa cha kwanza kwa mwendokasi kuliko vingine vyote nchini. Kina uwezo wa kubeba watu 300 waliokaa pamoja na mizigo.

Akizungumza katika hafla ya kupokea kivuko hicho kwenye Bandari ya Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuri alisema ujio wa kivuko hicho chenye thamani ya Sh7.9 bilioni ni mwanzo wa utatuzi wa kero ya foleni katika jiji hili.

Dk magufuli alisema kumekuwa na utegemezi mkubwa wa usafirishaji kwa njia ya barabara, jambo ambalo linasababisha foleni bila sababu ya msingi.

“Asilimia 99 ya mizigo husafirishwa kwa njia ya barabara, wakati asilimia moja tu ikisafirishwa kwa ndege, treni na meli. Hakuna haja ya kusafirisha makontena kwa njia ya barabara, tunahitaji usafiri wa treni kusafirisha makontena kutoka bandarini kwenda nje ya mji ili malori yakapakie huko,” alisema.

Alisema kwa kufanya hivyo kutasaidia kupunguza adha ya foleni, ambayo mara nyingi husababishwa na malori yanayobeba mizigo kutoka au kwenda bandarini, hasa katika Barabara za Mandela na Kilwa.

Waziri huyo alibainisha miradi mingine ya kupunguza foleni itakayotekelezwa jijini ni ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara eneo la Ubungo na Tazara. Pia, ujenzi wa Daraja la Kigamboni litakalokamilika Juni, mwakani na kugharimu Sh214 bilioni.

Alisema mradi mwingine wa Mabasi Yaendayo Kasi (BRT) utagharimu Sh288 bilioni na unatarajiwa kukamilika Machi, mwakani. Alibainisha kuwa bado ujenzi wa barabara za mzunguko unaendelea na kumtaka mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kudhibiti wafanyabiashara ndogondogo wanaoingilia hifadhi ya barabara na kusababisha foleni.

“Dar es Salaam inahitaji vivuko vingine vingi zaidi, tuna Sh3.7 bilioni kwa ajili ya kivuko kingine cha Dar es Salaam,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa), Mhandisi Marcellin Magesa alisema mradi wa ujenzi wa kivuko cha Dar es Salaam – Bagamoyo ulianzishwa na Serikali kupitia bajeti yake ya mwaka 2013/14.