Ushahidi dhaifu wamnusuru kitanzi aliyeshtakiwa kwa mauaji
Muktasari:
- Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Simiyu, imemuachia huru Majebele Robert Sang’udi aliyekuwa ameshtakiwa kwa kosa la mauaji ya Kugi Mwinula baada ya kubaini kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kosa hilo bila kuacha shaka.
Arumeru. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Simiyu, imemuachia huru Majebele Sang’udi aliyekuwa akikabiliwa na shtaka la mauaji ya Kugi Mwinula baada ya kuridhika kuwa upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha kosa hilo bila kuacha shaka yoyote ya msingi.
Mahakama imeeleza kuwa ushahidi wa kisayansi na wa mazingira uliowasilishwa ulikuwa na mapungufu makubwa yaliyofanya kesi hiyo kutokidhi viwango vinavyohitajika katika mashauri ya jinai.
Hukumu hiyo iliyomwachia huru mshtakiwa huyo ilitolewa Juni 2, 2026 na Jaji Hussein Mtembwa aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, ambaye baada ya kupitia ushahidi wa pande zote alibaini kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kuwa mshtakiwa ndiye alimuua Kugi.
Tukio hilo lilidaiwa kutokea Agosti 28, 2025 katika Kijiji cha Nkololo, Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu saa mbili usiku.
Ushahidi ulivyokuwa
Ili kuthibitisha kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi sita huku upande wa utetezi ukiwasilisha mashahidi watatu.
Shahidi wa kwanza wa mashtaka (PW1), ambaye ni shangazi wa marehemu, aliiambia Mahakama kuwa usiku wa Agosti 28, 2025 alirejea nyumbani kutoka eneo alilokwenda kuchaji simu na kumkuta Kugi akiwa amefariki dunia katika dimbwi la damu huku dada yake akiwa amejeruhiwa vibaya lakini akiwa hai.
Alidai baada ya kuona tukio hilo alimtuma mjukuu wake kwenda kumwita mwanawe, John Kefa, ambaye alipofika alipiga kelele ya tahadhari iliyowafanya wananchi wengi kufika eneo la tukio. Baadaye polisi walifika na kuanza uchunguzi ambapo walipata jiwe na jembe lenye madoa ya damu.
PW1 pia alieleza wajukuu waligawiwa shamba la familia kwa ajili ya kulima kwa muda wakati wa msimu, ila kukatokea mgogoro wa kifamilia uliotokana na mgawanyo wa fedha za fidia za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) baada ya mradi wa umeme kupita kwenye ardhi hiyo, ambapo kutokana na mradi huo marehemu alipewa Sh2 milioni, malipo yaliyofanywa kupitia akaunti ya benki.
Ilidaiwa Kugi (marehemu kwa sasa) alitoa mgao ambapo alimpa mshtakiwa Sh10,000, kisha akampa yeye (PW1) Sh10,000 na siku iliyofuata mshtakiwa alichukua fedha hizo na fedha nyingine Sh30,000 na kurudisha kwa Kugi kutokana na kutokukubaliana na mgao huo.
Alidai mshtakiwa hakuridhishwa na kiasi cha fedha alichopewa na hata alizirejesha. Hata hivyo, alipoulizwa na wakili wa utetezi, alikiri kuwa hakuwahi kushuhudia mshtakiwa akimuua marehemu na kwamba hakujua ni nani aliyefanya mauaji hayo.
Zaidi, alieleza kuwa kulikuwa na migogoro mingine ya kifamilia ikiwemo ya ardhi iliyowahusisha watu wengine.
PW2 ambaye ni daktari aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu, aliiambia Mahakama kuwa marehemu alifariki kutokana na kutokwa damu nyingi kulikosababishwa na majeraha makubwa yaliyotokana na vitu butu na vyenye ncha kali.
Alidai marehemu alikuwa na majeraha makubwa kichwani, miguuni na sehemu nyingine za mwili, huku baadhi ya mifupa ikiwa imevunjika.
PW3 ambaye ni mtaalamu wa uchunguzi wa vinasaba (DNA), aliwasilisha ripoti ya uchunguzi wa vinasaba, akidai kuwa uchunguzi uliofanyika kwenye vielelezo mbalimbali ulionyesha kuwa mpini wa jembe ulikuwa na DNA za zaidi ya mtu mmoja.
Hata hivyo, alisema DNA ya mshtakiwa haikuweza kulinganishwa moja kwa moja na DNA iliyopatikana kwenye mpini huo kutokana na kutopatikana kwa wasifu kamili wa vinasaba.
PW4 ambaye ni mtaalamu wa alama za vidole, aliiambia Mahakama kuwa baada ya kufanya uchunguzi alibaini kuwa alama za vidole za mshtakiwa zilifanana na alama zilizochukuliwa kutoka kwenye mpini wa jembe lililodaiwa kutumika katika tukio la mauaji.
PW5 ambaye alikuwa mpelelezi wa kesi hiyo, alieleza kuwa alipokea taarifa za siri zilizomtaja mshtakiwa kuwa ndiye aliyemuua marehemu. Baada ya mahojiano na baadhi ya mashahidi, alimkamata mshtakiwa Septemba 1, 2025 na kuendelea na uchunguzi.
Alidai baada ya mshtakiwa kukana kuhusika na mauaji hayo, waliamua kutumia uchunguzi wa kisayansi wa DNA na alama za vidole ili kubaini ukweli.
PW6 alieleza jinsi alivyohusika katika uchukuaji wa alama za vidole kutoka kwenye mpini wa jembe na namna vielelezo vilivyotumwa kwa wataalamu wa uchunguzi. Pia aliwasilisha nyaraka za mnyororo wa utunzaji wa vielelezo.
Utetezi
Kwa upande wa utetezi, mshtakiwa mwenyewe (DW1) alitoa ushahidi na kukanusha shtaka lote la mauaji, akisema marehemu ndiye aliyemlea tangu akiwa mtoto na walikuwa na uhusiano mzuri.
Alidai kuwa alikuwa akimsaidia marehemu kwa shughuli mbalimbali na wakati mwingine kumpatia mazao baada ya mavuno na kusisitiza kuwa hakuwa na mgogoro wowote na marehemu na kwamba hakuwa na sababu ya kumuua.
DW1 alidai kuwa alipofika eneo la tukio na kuuona mwili wa marehemu ukiwa katika dimbwi la damu, alishtuka kiasi cha kupoteza fahamu kutokana na huzuni.
Uamuzi wa Mahakama
Katika uamuzi wake, Mahakama ilisema upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha bila kuacha shaka yoyote kuwa Majebele ndiye aliyemuua Kugi.
Jaji Mtembwa amesema ingawa ilithibitika kuwa marehemu alikufa kifo kisicho cha kawaida kutokana na majeraha makubwa yaliyosababishwa na vitu butu na vyenye ncha kali, ushahidi uliowasilishwa haukuweza kumhusisha moja kwa moja mshtakiwa na tukio hilo.
Mahakama ilibaini kuwa hakuna shahidi aliyeshuhudia mauaji hayo, huku ushahidi wa mazingira uliotegemewa na upande wa mashtaka ukiegemea zaidi kwenye madai ya mgogoro wa kifamilia kuhusu mgawanyo wa fedha za fidia za Tanesco.
Hata hivyo, mahakama ilisema ushahidi huo haukuwa wa kutosha kwa kuwa mashahidi walikiri kuwepo kwa migogoro mingine ya kifamilia na kwamba hawakumwona muuaji.
Kuhusu ushahidi wa kisayansi, mahakama ilieleza kuwa ripoti ya DNA ilionyesha kuwa mpini wa jembe lililodaiwa kutumika katika mauaji ulikuwa na vinasaba vya zaidi ya mwanaume mmoja, huku DNA ya mshtakiwa ikishindwa kuhusishwa moja kwa moja na kielelezo hicho.
Mahakama pia iliona kuwa ushahidi wa alama za vidole uliwasilishwa katika mazingira yenye mashaka kutokana na kutokuwepo kwa mnyororo kamili wa utunzaji wa vielelezo.
Jaji Mtembwa amesema kuwa askari aliyedaiwa kukusanya jembe na jiwe kutoka eneo la tukio hakuitwa mahakamani kutoa ushahidi, jambo lililoacha maswali kuhusu namna vielelezo hivyo vilivyopatikana na kuhifadhiwa kabla ya kufikishwa kwa wataalamu wa uchunguzi.
Mahakama imeeleza kuwa jembe lenyewe halikuwasilishwa mahakamani kama kielelezo licha ya kutajwa kuwa silaha iliyotumika katika mauaji hayo.
Kutokana na mapungufu hayo, mahakama iliamua kutoupa uzito ushahidi wa alama za vidole na kuhitimisha kuwa ushahidi uliobaki haukutosha kuthibitisha shtaka la mauaji dhidi ya mshtakiwa.
“Kwa kuzingatia ushahidi wote uliowasilishwa mbele ya mahakama hii, kosa linalomkabili mshtakiwa halijathibitishwa bila kuacha shaka yoyote ya msingi,” amesema Jaji Mtembwa.
Mahakama ilimuamuru mshtakiwa aachiliwe mara moja kutoka gerezani isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine za kisheria.