Ushahidi kesi ya Mbowe, wenzake kuendelea leo

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiwasili katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi iliyopo Ubungo Mawasiliano jijini Dar es Salaam, jana. Picha na Michael Matemanga


Muktasari:

  • Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu inatarajiwa kuendelea leo, huku shahidi wa tisa wa upande wa mashtaka akianza kutoa ushahidi.

Dar es Salaam. Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu inatarajiwa kuendelea leo, huku shahidi wa tisa wa upande wa mashtaka akianza kutoa ushahidi.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni Halfan Hassan, Adamu Hassan Kasekwa maarufu kama Adamoo na Mohamed Ling’wenya.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita, yakiwamo ya kufadhili vitendo vya ugaidi, kukutwa na silaha aina ya bastola pamoja na sare za jeshi kinyume cha sheria.

Kesi hiyo ambayo iko mbele ya Jaji Joachim Tiganga inasikilizwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumi Uchumi na tayari mashahidi nane kati ya 24 wameshatoa ushahidi, akiwamo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Ramadhan Kingai.

Hata hivyo, juzi Mrakibu wa Polisi Jumanne Malangahe alikamilisha kutoa ushahidi wake baada ya kuhojiwa na kiongozi wa jopo la upande wa utetezi, Peter Kibatala.

Malangahe, ambaye alikuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arumeru, pia alishiriki kuwakamata Adam Kasekwa na Mohamed Ling’wenya, Rau Madukani mkoani Kilimanjaro.

Malangahe alikiri kutofahamu ni wapi mshtakiwa Ling’wenya alishiriki vikao vya ugaidi.

Hii ni sehemu ya mahojiano baina ya wakili wa utetezi, Peter Kibatala na shahidi wa upande wa Jamhuri, Malangahe.

Wakili: Ni wapi Ling’wenya alikiri kushiriki vikao vya kigaidi?

Shahidi: Hakuna.

Wakili: Nitafutie mahali Ling’wenya akieleza bastola itakavyotumika kwenye vitendo vya kigaidi.

Shahidi: Hakuna.

Wakili: Nionyeshe ni wapi Ling’wenya alieleza vilipuzi vitakavyotumika kulipua vituo vya mafuta.

Shahidi: Hakuna.

Wakili: Niambie pale Rau Madukani uwepo wao ulikuwa unahusiana kupanga kutekeleza vitendo vya kigaidi?

Shahidi: Walikuwa kwenye mpango huo.

Wakili: Unafahamu Adamoo hii bastola na risasi alipata wapi?

Shahidi: Sifahamu.

Wakili: Dawa za kulevya alizokutwa nazo Ling’wenya mlichunguza amepata wapi?

Shahidi: Hatukuchunguza.

Wakili: Kwa nini hamjazungumzia kwenye kesi hii?

Shahidi: Hatukuzungumzia.

Wakili: Katika uchunguzi wenu mligundua yanahusika vipi na hii kesi.

Shahidi: Sifahamu.