Ushahidi wafungwa kesi ya Halima Mdee kutoa lugha chafu kwa Magufuli

Muktasari:

Katika kesi hiyo mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee anadaiwa kutoa maneno dhidi ya Rais Magufuli ambayo upande wa mashtaka umedai ni kumdhalilisha Rais na uvunjifu wa amani

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais John Magufuli inayomkabili mbunge wa Kawe, Halima Mdee umefunga ushahidi baada kujiridhisha na mashahidi watatu waliotoa ushahidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili wa Serikali, Wankyo Simon alidai hayo leo Alhamisi  mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa shauri lilikuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi lakini kwa upande wao wameridhika na mashahidi watatu waliotoa ushahidi mahakamani hapo.

"Shauri lilikuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi lakini upande wetu wa Serikali tumeridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi wetu watatu hivyo  tunafunga ushahidi,"alidai Simon.

Baada ya maelezo hayo wakili wa utetezi, Hekima Mwasipu aliiomba mahakama hiyo ndani ya siku 14 kuwasilisha hoja kwa njia ya maandishi kama mteja wao ana kesi ya kujibu au la.

Upande wa mashtaka utawasilisha hoja zao siku 14 baada ya kupokea hoja zao za upande wa utetezi .

Hakimu Simba alisema Machi 6, 2020 upande wa utetezi utawasilisha hoja zao na Machi 20, 2020 upande wa mashtaka utawasilisha majibu ya hoja za upande wa utetezi.

Shauri hilo litarudi tena Aprili Mosi, 2020 kwa ajili ya kutolewa uamuzi.

Mdee anakabiliwa na shtaka la kutoa lugha chafu dhidi ya Rais  John Magufuli ambapo alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Julai 10, 2017.

Katika kesi ya msingi inadaiwa kuwa Julai 3, 2017 katika ofisi za makao makuu ya Chadema zilizopo mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni, Mdee alitamka maneno dhidi ya Rais John Magufuli kuwa, ‘anaongea hovyo, anatakiwa afungwe breki,’ kitendo kinachodaiwa kuwa ni kumdhalilisha Rais na kusababisha uvunjifu wa amani.