Usiyoyafahamu kuhusu Mustafa Mkulo

Waziri wa zamani wa Fedha wa Tanzania, Mustafa Mkulo

Muktasari:

  •  Mustafa Mkulo alikuwa mbunge wa Kilosa kwa miaka 10 hadi mwaka 2015 alipoamua kuacha ili angine mwingine

Dar es Salaam. Wakati Mustafa Mkulo kesho Jumapili Mei 5, 2024 akihitimisha safari yake ya mwisho hapa duniani, waziri huyo wa zamani wa fedha ameelezwa jinsi alivyofanya mageuzi makubwa ndani ya Shirika la Hifadhi za Jamii (NSSF).

Mkulo aliyefikwa na mauti jana Ijumaa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu, mwili wake unatarajiwa kuzikwa nyumbani kwake, Kilosa mkoani Morogoro kesho Jumapili. 

Watu wa karibu na mbunge huyo wa zamani wa Kilosa wamemwelezea kwa mitizamo tofauti na alama alizoziacha hapa nchini ambazo zitabaki kukumbukzwa.

Waziri wa zamani wa kilimo, Dk Charles Tizeba aliyefanya kazi na Mkulo katika Baraza la Mawaziri chini ya Rais Jakaya Kikwete amesema alimfahamu tangu akiwa Mkurugenzi Mkuu NSSF huku akieleza ndiye aliyekuja na wazo la kuanza kutumia fedha za mfuko huo kufanya uwekezaji.

“Ndiye mkurugenzi wa kwanza wa mfuko ule, aliyeanzisha uwekezaji katika mfuko, kabla yake fedha zilikuwa zinakaa hazizunguki, alikuja na harakati za kuewekeza,” amesema Dk Tizeba.

Baada ya kutoka kuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF aliingia katika ubunge kabla ya kuwa Waziri wa Fedha kati ya mwaka 2007 hadi 2012 na anatajwa kuleta mageuzi kadhaa ikiwamo kupunguza mfumuko wa bei.

“Wakati wake ndiyo kasi ya mfumuko wa bei wa Taifa ulianza kupungua kutoka namba mbili (two digit) yaani 10 na kuendelea hadi kuwa namba moja tunazozishuhudia sasa (single digit),” amesema Dk Tizeba.

 “Pia alisimamia sana makusanyo ya TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) na kuyafanya kuongezeka, alikuwa kiongozi mzuri alieelewa anachokifanya na kusimamia anachokiamini.”

Naye Aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSFCrescentius Magori amesema chini ya Mkulo ndiyo NSSF ilizaliwa kutoka Mfuko wa akiba (National Provident Fund -NPF) aliyoikuta. 

Amesema mwaka 1987 wakati Mkulo akiingia NPF alilikuta shirika hilo likiwa linachukiwa na wafanyakazi kutokana na kuchelewesha mafao, hakuna takwimu wala kumbukumbu.

“Alikuja kufanya mapinduzi makubwa sana na baadaye ikaonekana ulipaji wa hela kwa mkupuo haiwapendezi wafanyakazi kwa sababu wamezoea kufanya kazi na kulipwa kila mwezi, mwaka 1997 yakafanyika mageuzi makubwa katika sekta ya hifadhi ya jamii na kuzaliwa NSSF,” amesema. 

Amesema kupitia mageuzi hayo shirika liligeuzwa kutoka Mfuko wa akiba wa wafanyakazi na kuwa mfuko wa hifadhi wa jamii huku akieleza, Mkulo aliendelea na utekelezaji wa kile alichokianzisha hadi alipoomba kustaafu mwaka 2000.

“Hifadhi ya jamii imepoteza nguli aliyeleta mapinduzi na magauezi makubwa ambayo tutayaenzi,” amesema Magori.

Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Pofesa Haji Semboja amesema Mkulo alikuwa mtu anayejua nini Serikali inahitaji, kinachotakiwa kufanywa na kinachoweza kutekelezwa na alikuwa mtu wa mfumo.

“Mtu kama huyu kila kitu kilifanyika kwa sera na mipango na mawasiliano ndani ya Serikali, alifanya kazi vizuri sana, alikuwa anaelewa kile anachokifanya, mwenye kusikiliza watu na kuelewa kirahisi,” amesema Semboja.

Anasema katika utendaji wake alikuwa mtu wa kupokea mawazo na hakua mtu wa kujificha.

Kiongozi wa Chama mstaafu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema anamkumbuka wakati Mkulo anakuwa Waziri wa Fedha, ndiyo kilikuwa kipindi kigumu cha sakata la Escrow. 

Katika ripoti ya Uchunguzi Maalumu wa mabilioni ya fedha ya Akaunti ya Tegeta Escrow Mkutano wa Bunge wa 16/17 maazimio yaliyofikiwa Novemba 29 mwaka 2014, ulisababisha mawaziri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge kujiudhuru nyadhifa zao.

Mawaziri waliong’oka kutokana na sakata hilo ni, Profesa Anna Tibaijuka aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Sospeter Muhongo wa Nishati na Madini pamoja na AG Fredrick Werema.

Wabunge waliovuliwa nyadhifa zao ni; Andrew Chenge (Bajeti- Bariadi Magharibi), William Ngeleja (Katika, Sheria na Utawala-Sengerema), Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini-Lupa).

Zitto aliyekuwa mbunge wakati huo amesema: “Tulikwazana na Mkulo kwa hoja sio kwa ubaya kuhusu mgogoro wa Shirika la Consolidated Holdings, lakini pia wakati marehemu ndiyo kulikuwa na kashi kashi ya sakata la Epa (Akaunti ya Madeni ya Nje).”

Zitto alikumbushia namna walivyohakikisha usimamizi ofisi ya deni la Taifa linarejeshwa wizara ya fedha badala ya kubaki katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakati Mkulo akiwa waziri wa sekta hiyo. 

“Mara mwisho nilikutana na mzee Mkulo katika msiba wa Membe (Bernard-aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje) Mungu ailaze pema peponi roho yake,” amesema Zitto.

Kufuatia kile alichokisema Zitto, Mei 2012, Mkulo alikuwa miongoni mwa mawaziri sita waliotemwa katika baraza la mawaziri la Kikwete ambapo kila mmoja aliachwa kwa sababu zake. 

Mawaziri hao waliotemwa walikuwa wakiongoza wizara nyeti zinazosimamia rasilimali za nchi na huduma za afya na uchukuzi. 

Katika waliong'olewa mbali na Mkulo (Fedha) wengine ni William Ngeleja (Nishati na Madini), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Omari Nundu (chukuzi), Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara) Dk Haji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii). 

Pia, panga hilo liliwakumba waliokuwa Naibu Mawaziri, Dk Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii) na Dk Athuman Mfutakamba (Uchukuzi). 

Kuanguka kwa Mkulo, Ngeleja na Maige kulitajwa kutokana na taarifa hiyo ya CAG iliyozihusisha wizara zao na ufisadi. 

Hadi umauti unamkuta, Mkulo amewahi kufanya kazi katika ofisi tofauti ndani ya Serikali ya Tanzania ikiwamo Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Ofisi ya Msajili wa hazina na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF). Alikuwa mbunge wa Kilosa kwa miaka 10 hadi mwaka 2015 alipoamua kuacha ili angine mwingine.