Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utafiti: Asilimia 15 madai ya bima duniani yana viashiria vya udanganyifu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Saada Mkuya Salum

Muktasari:

  • Akizungumza leo Alhamisi Mei 15, 2025, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango ya Zanzibar, Dk Saada Mkuya Salum amesema udanganyifu katika sekta ya bima nchini, unatajwa kuathiri kwa kiasi kikubwa uaminifu wa sekta hiyo na kuathiri ustawi wa wananchi wanaotegemea bima kama ngao ya kiuchumi dhidi ya majanga

Arusha. Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi amesema utafiti wa hivi karibuni unaonyesha takribani asilimia 10 hadi 15 ya madai ya bima duniani kote yana viashiria vya udanganyifu.

Udanganyifu wa sekta hiyo hapa nchini unatajwa kuathiri kwa kiasi kikubwa uaminifu wa sekta hiyo, kuongeza gharama za huduma za kampuni za bima, kudhoofisha uwekezaji na kuathiri ustawi wa wananchi wanaotegemea bima kama ngao ya kiuchumi dhidi ya majanga.

Hayo yamesemwa jana  Alhamisi Mei 15, 2025 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Saada Mkuya Salum, kwa niaba ya Rais Mwinyi katika mkutano mkuu wa mwaka wa umoja wa wataalamu wa masuala ya uchunguzi na ubadhirifu wa masuala ya bima (IASIU), mwaka 2025 jijini Arusha.

Dk Saada amesema udanganyifu ni changamoto kubwa siyo tu kwa kampuni za bima bali pia kwa Serikali, kwa sababu fedha hizo zingetumika kutoa huduma bora kwa wananchi na kuongeza uwekezaji katika maeneo mengine ya maendeleo.

Amesema udanganyifu wa bima si tu kosa la jinai bali ni kikwazo cha maendeleo kwani kinaporomosha imani ya wananchi katika mfumo, kuathiri uendelevu wa kampuni za bima ambazo zinafanya kazi kwa uadilifu.

"Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa takribani asilimia 10 hadi 15 ya madai ya bima duniani kote yana viashiria vya udanganyifu.Katika nchi yetu tumeshuhudia ongezeko la visa vya madai hewa, matumizi ya nyaraka bandia na hili haliwezi kuvumiliwa," amesema

"Nimeelezwa udanganyifu unaoripotiwa mara kwa mara ni pamoja na uwasilishaji madai ya uongo au kupangwa,kuficha taarifa muhimu wakati wa kuomba bima, ushirikiano usio sahihi kati ya wateja, watumishi wa kampuni za bima au hospitali.

Kutokana na changamoto hizo Waziri huyo amesema Serikali ina dhamira ya kweli ya kupambana na udanganyifu wa aina yoyote na kuwa inaanzisha mkakati maalum wa kitaifa wa  kudhibiti udanganyifu wa bima kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania ( Tira).

"Kupitia mkakati huo tutashirikiana na vyombo vya usalama, mamlaka zingine zilizokuwa katika mnyororo wa huduma za kibima, kuweka kanuni kali dhidi ya kampuni au watu wanaojihusisha na rushwa na kuanzisha mahakama au kitengo maalum cha kushughulikia kesi za udanganyifu wa bima kwa haraka na weledi," ameongeza.

Waziri huyo amesema huu ni wakati wa kujitathmini, kushirikiana na kuchukua hatua ambapo amezitaka kampuni za bima, hospitali na washauri wa kifedha kuungana na serikali katika kuimarisha maadili na uwajibikaji wa sekta hiyo.

"Tuache kujilinda kwa kisingizio cha ushindani wa kibiashara huku tukiacha mianya ya udanganyifu kuendelea.IASIU inalenga kuweka msisitizo juu ya umuhimu wa kuwepo kwa vitengo imara vya uchunguzi ndani ya taasisi za kifedha na bima na kuweka mipaka ya kuripoti na kushughulikia madai yenye mashaka.

Awali, Kamishna wa Bima nchini, Dk Baghayo Saqware amesema mkutano huo ni fursa adhimu ya kujadili changamoto zinazokabili sekta ya bima hasa suala la udanganyifu ambalo limeendelea kuwa mwiba kwa maendeleo na ufanisi wa sekta hiyo.

Amesema udanganyifu katika bima ni changamoto inayozikumba si kampuni za bima tu bali wateja na jamii kwa ujumla na kuongeza kuwa sekta hiyo inakua kwa asilimia 15 kila mwaka.

"Kama mnavyofahamu udanganyifu katika bima huathiri uaminifu wa wateja na kuathiri utendaji wa kampuni za bima. Unaleta hasara kubwa kiuchumi na kupunguza kasi ya maendeleo ya sekta nzima na kwa upande wetu kama mamlaka tumeweka mkakati madhubuti ili kukabiliana na changamoto hii," amesema.

"Tumeanzisha mifumo ya kisasa ya kudhibiti taarifa na kufuatilia madai ya bima kwa ukaribu zaidi na tunashirikiana kwa karibu na wadau wengine wa sekta ya bima," amesema.

Kamishna huyo amesema ili kupambana na udanganyifu katika bima,pia wameanzisha kitengo cha kupambana na udanganyifu katika bima (Insurance Fraud Unit), ambacho kina jukumu muhimu la kuhakikisha uwazi,uwajibikaji na uadilifu kwenye sekta hiyo unaongezeka ikiwemo kuchambua nyaraka na ushahidi ili kubaini vitendo vyenye nja ya udanganyifu.

Rais wa AISIU  tawi la Tanzania, Mjabwa Hanzuruni amesema tawi hilo ambalo ni la kwanza Barani Afrika, amesema linalenga kukuza ufanisi katika kuibua, kuchunguza na kuzuia udanganyifu wa bima kwa kutumia mbinu bora na za kisasa na kujenga uelewa kwa wanachama wake na kuhamasisha maadili ya juu ya taaluma.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini, amesema kumebainika kuwepo kwa changamoto za kisheria na kushauri sheria zenye ukakasi ambazo ni kikwazo waziainishe zifanyiwe marekebisho.