Utafiti dawa ya kansa kicheko

Muktasari:

  • Madaktari ulimwenguni kote wanaendelea kukuna vichwa vyao kwa matumaini kwamba mafanikio ya hivi karibuni katika majaribio ya dawa za saratani yataidhinishwa.


Dar es Salaam. Madaktari ulimwenguni kote wanaendelea kukuna vichwa vyao kwa matumaini kwamba mafanikio ya hivi karibuni katika majaribio ya dawa za saratani yataidhinishwa.

Katika majaribio ya dawa yaliyofanywa na watafiti katika Kituo cha Saratani cha Memorial Sloan Kettering (MSK) cha New York, wagonjwa wote 12 waliopewa dawa walitibiwa saratani kwa mafanikio.

Walitibiwa kwa dawa iitwayo dostarlimab ambayo inauzwa kwa jina la Jemperli.

Watafiti, kama walivyonukuliwa na gazeti la The New York Times, wamesema dostarlimab ni dawa ya kinga ya mwili inayotumika kutibu saratani ya endometria, ukiwa uchunguzi wa kwanza wa kitabibu dhidi ya saratani ya uvimbe kwenye utumbo mpana.

“Ninaamini hii ni mara ya kwanza kutokea katika historia ya saratani,” daktari wa magonjwa ya saratani, Luis Diaz Jr. kutoka MSK aliliambia gazeti la New York Times.

Habari hizo zimepokewa kwa matumaini, huku Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) ya jijini Dar es Salaam, Dk Julius Mwaiselage akisema ameisoma habari hiyo kwa matumaini huku akitarajia matokeo ya tafiti zaidi.

“Tumepokea habari hizo vizuri. Hata hivyo, kulikuwa na watu wachache tu waliohusika katika utafiti, mengi zaidi bado yatahitajika katika awamu nyingine ya majaribio ili dawa ikubalike na kuruhusiwa kufanya kazi,” alisema.

Dk Mwaiselage alisema majaribio zaidi yatalazimika kufanywa kwa watu wengi tofauti, wakiwemo wanaume, wanawake, vijana, watoto na wazee.

“Watu hawa lazima wapitie hatua ya kwanza, hatua ya pili na ya tatu katika majaribio,” alisema.

Alisema wagonjwa wa saratani kwa sasa wanaongezeka kote ulimwenguni na njia pekee ya uhakika ya kunusurika na ugonjwa huo kwa sasa ni kuwahi kupima na kupata matibabu mapema.

“Kadiri tunavyoendelea kuwa na matumaini, ni muhimu kutambua kwamba inachukua muda kwa dawa kuidhinishwa. Inachukua miaka kadhaa kuanzia mitatu hadi minne kuidhinishwa rasmi baada ya awamu ya majaribio, lakini ikithibitika kuwa na matokeo ya kutia moyo, inaweza kuchukua hata mwaka mmoja tu,” alisema Dk Mwaiselage.

Sambamba na utaratibu wa kuidhinisha, mara itakapopitia majaribio yote husika nchini Marekani na pia Mamlaka ya Dawa na Vifaa vya Tiba Tanzania ndani ya nchi, hospitali zitalazimika kuanza kuitumia.

“Majaribio hayo ya kutia moyo yataruhusu watu mbalimbali kutoa maoni yao na tunasubiri kuona iwapo hatimaye watatangaza kuhusika kwa watu wengi zaidi katika majaribio hayo.

“Hilo likifanyika, tuko tayari kushiriki na kuona jinsi wagonjwa wetu wa saratani wanavyoweza kupata matibabu katika siku zijazo,” alisema Dk Mwaiselage.

Bila kuweka takwimu halisi za wagonjwa wa saratani nchini Tanzania, Dk Johnson Katanga pia kutoka Ocean Road alisema tatizo hilo ni kubwa nchini hadi kufikia hatua ya Serikali kuweka vituo vya matibabu katika baadhi ya mikoa, ikiwemo Mbeya, Kilimanjaro na Dar es Salaam.

“Pia tunapokea wagonjwa kutoka nchi jirani za Msumbiji na Malawi miongoni mwa nyingine,” alisema.

Alisema inatia moyo kuwa dawa hiyo imeonyesha matokeo chanya kwa binadamu, jambo ambalo linaonyesha kuwa imepitia baadhi ya hatua za majaribio.

“Ili dawa zianze kufanya kazi lazima zipitie awamu nne ambapo zinaanzia kwa wanyama na kisha kwa binadamu. Walichokifanya wenzetu ni katika hatua ya tatu ambapo kikundi kidogo cha watu wamepimwa na wataangalia majibu ya dawa hizo kabla na baada,” alisema Dk Katanga.

Dk Katanga aliongeza kuwa baada ya majaribio mengine, wataongeza idadi ya watu ili kujua ufanisi wa dawa hiyo baada ya mamlaka katika nchi husika kutuma dawa iliyothibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kutumika kote.

“Kama WHO itaidhinisha dawa hizi, tutakuwa na wakati mzuri wa kuzitumia nchini kwa idhini ya TMDA, tunaweza kuzinunua kutoka MSD au kuagiza kutoka nje,” alisema Dk Katanga.

Imeandikwa na Naomi Achieng