Utafiti marufuku

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imeagiza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (Tari), kusitisha shughuli za utafiti wa mbegu za GMO pamoja na kuteketeza mazao yote yaliyokuwa yakitumika kwa ajili ya tafiti.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeagiza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (Tari), kusitisha mara moja shughuli za utafiti wa mbegu za GMO pamoja na kuteketeza mazao yote yaliyokuwa yakitumika kwa ajili ya tafiti.

Agizo hilo lilitolewa juzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mathew Mtigumwe baada ya wizara hiyo kujiridhisha kuwa taasisi hiyo ilikuwa imeshaanza kutangaza matokeo ya utafiti kabla ya kuthibitishwa na Serikali.

“Hivi karibuni, Tari kupitia kituo chake cha Makutopora imeshuhudiwa wakialika makundi mbalimbali kufuatilia matokeo ya utafiti wa mbegu hizo wakati Serikali ikiwa haijathibitisha matumizi hayo ya GMO hapa nchini.

“Walitakiwa kwanza kutoa ripoti hiyo kwa wizara kusudi ijiridhishe kama mbegu hizo ni salama kwa matumizi ya binadamu, baada ya majadiliano ndiyo Serikali ingefanya uamuzi,” alisema Mtigumwa.

Hata hivyo, baadhi ya watafiti ambao hawakuwa tayari kutajwa majina yao gazetini walielezea mshituko wao kuhusu uamuzi huo wa Serikali.

“Kama agizo limetoka juu tunahitaji kuwa watulivu kusubiri barua rasmi,” alisema mmoja kati ya watafiti hao.

Mwanasayansi mwingine alisema kazi ya sayansi ni kuleta mabadiliko chanya kwa jamii, lakini hawatakuwa na uwezo wa kufanya lolote kama jamii hiyo haitakuwa tayari kupokea mabadiliko hayo.

Alisema katika sayansi hakuna kinachojadiliwa zaidi nje ya matumizi ya takwimu na vielelezo vya kuthibitisha ukweli.

Mtafiti mwingine alisema ni kweli umma haukuwa na taarifa za kutosha kuhusiana na ukweli wa mbegu za GMO katika zao la mahindi, zilikuwa bado ziko chini ya uzio wa eneo la kituo cha kufanyia utafiti cha Tari na haikuwa imefika kwa wananchi,

Hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata), Steven Ruvuga alinukuliwa na vyombo vya habari katika mkutano wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere akisema mbengu za GMO zitawanyima wakulima haki ya kuwa na uchaguzi wa mbengu wanazozitaka.

Mkurugenzi huyo alikuwa akimaanisha mbegu hizo zitaondoa zile zilizokuwa zikitumiwa na wakulima kwa miaka mingi nchini.

Wakizungumza kwa simu na Mwananchi jana, baadhi ya wataalamu wanaofanya majaribio ya GMO walisema wanasubiri maelekezo ya Serikali.

Dk Janeth Kaaya, mtafiti mstaafu alisema wameipokea kauli ya Serikali kwa masikitiko.

Kauli ambayo iliungwa mkono na Dk Nicholas Nyange aliyesema, “Sisi tunasubiri maelekezo baada ya tamko hili.”

Hata hivyo, Mbunge wa Mwanga, Profesa Jumanne Maghembe alisema utafiti na matumizi ya GMO yanaendeshwa na sheria.

“Kuna sheria inayoendesha uhandisi wa jeni, kwa mtu anayezalisha mazao kama atabainika amesababisha madhara kwa zile mbegu kwa njia ya ‘poleni’, atawalipa wakulima wenzake kwa kadiri atakavyokuwa amesababisha hasara,” alisema Profesa Maghembe.

Alisema umuhimu wa GMO wakati mwingine ni kukabiliana na magonjwa ya mimea na ukame.

“Kwa mfano kule Bukoba, kuna ugonjwa wa mnyauko wa migomba, umesababishwa na wenyeji kubadilisha utamaduni wao wa matumizi ya vyakula, maana ndizi ndio chakula chao kikuu. Sasa wanakula ugali,” alisema Maghembe.

Profesa Maghembe ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Kilimo, alisema mbali na mazao ya chakula kuna mazao ya viwanda kama pamba ambayo mbegu zake za GMO huzalisha mara 10 kuliko ilivyo ile ya asili kwa sasa.

Alisema kwa mfano Kenya, imeshapitisha mbegu za GMO kupitia Bunge lao zilizosambazwa Sudan, Mali, na Afrika Kusini.

Alisema mbegu za aina hiyo zipo pia Pakistan, India, Uturuki na China. “Hata nguo tunazovaa zinazotoka nje, pamba yake ni ya GMO.”

Hata hivyo, Mhadhiri wa Sayansi ya siasa wa chuo kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda aliyefanya utafiti wa kijamii, uchumi na mazingira katika usalama wa chakula, alisema anaishukuru Serikali kwa kutoa tamko hilo. “Hii ni hatua muhimu kwa usalama wa chakula,” alisema.

Na aliikosoa Tari akisema awali ilikuja na matumaini makubwa kwa wakulima lakini sasa wamegeuka.

“Kwa mfano pale Bagamoyo kuna kituo cha utafiti chenye teknolojia za asili kwa muhogo. Sasa unaleta teknolojia nyingine mpya ya nini,” alihoji.