Utafiti utakaobainisha changamoto za tozo kwenye zabibu waja

Muktasari:

  • Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Kampuni ya Agri Connect inafanya tahimini mnyororo wa thamani katika zao la zabibu unaolenga kubainisha changamoto zitokanazo na tozo za ushuru na ada.

Dodoma. Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Kampuni ya Agri Connect inafanya tahimini mnyororo wa thamani katika zao la zabibu unaolenga kubainisha changamoto zitokanazo na tozo za ushuru na ada.

Tathimini hiyo inalenga katika kushauri sera wezeshi za ufanyaji wa biashara ya zao hilo zitakazowezesha kulinda soko la zabibu hapa nchini.

Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda ameyasema hayo jana Ijumaa Novemba 5, 2021 wakati uzinduzi wa tamasha la mvinyo linalojulikana kama Dodoma Wine Festival.

Aidha, amesema Serikali kwa kushirikiana na moja ya kampuni nchini Israel watatoa elimu ya kanuni bora za kilimo na miundombinu ya umwagiliaji ili kuongeza tija za uzalishaji mazao ya kibiashara.

Profesa Mkenda amesema kuna viwanda vikubwa viwili, vya kati, viwanda vitatu na viwanda vidogo 13 ambavyo vinafanya usindikaji wa zao hilo la zabibu.

Amesema zao la zabibu ni kama kielekezo ama nembo ya mkoa wa Dodoma na hivyo kutokana na hilo Serikali imechukua hatua mbalimbali ili kuimarisha zao la Zabibu.

Amezitaja hatua hizo ni pamoja na kuweka mratibu wa zao la zabibu wizarani kwa ajili ya kusimamia zao hilo na kufanya mafunzo rejea  kwa maofisa ugani huduma.

Profesa Mkenda amesema Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Nchini (TARI), imepatiwa takribani Sh200 milioni kwa ajili ya kufanya utafiti, kuzalisha miche bora ya zabibu na kutoa elimu ambapo Sh80 milioni zimeshatolewa.