Utafiti wa kichocho kufanyika Kanda ya Ziwa
Muktasari:
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani zinakadiria asiliamia 52 ya Watanzania sawa na watu milioni 22 wanaugua ugonjwa wa Kichocho na minyoo ya tumbo, Kanda ya Ziwa inaongoza kwa kuwa na maambukizi ya asilimia 50 hadi 80 ya magonjwa hayo ambayo hayapewi kipaumbele.
Mwanza. Utafiti kujua ukubwa wa tatizo la ugonjwa wa kichocho kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa unatarajiwa kufanywa kwa kipindi cha wiki 14 hadi 18 kuanzia Novemba, 2023.
Utafiti huo utakaotumia Dola za Kimarekani 428, 000 unatarajia kuanza kufanyika Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu ukihusisha wanawake wenye miaka kuanzia 18 hadi 60.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani zinakadiria asiliamia 52 ya Watanzania sawa na watu milioni 22 wanaugua ugonjwa wa Kichocho na minyoo ya tumbo, Kanda ya Ziwa inaongoza kwa kuwa na maambukizi ya asilimia 50 hadi 80 ya magonjwa hayo ambayo hayapewi kipaumbele.
Ugonjwa huo unaoenezwa na minyoo aina ya Schistosoma unasababishwa na matumizi ya maji yasiyo safi na salama, shughuli za kilimo zinazohusisha maji yaliyotuama kama Mpunga pamoja na matumizi ya maji ya kwenye madimbwi wakati wa kiangazi.
Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za Afya Bugando (Cuhas) kwa kushirikiana na Mfuko wa Magonjwa yasiyopewa Kipaumbele kutoka Marekani (COR-NTD) wamezindua mradi unaohusika na Kichocho katika via vya uzazi wa wanawake ili kubaini chanzo na suluhu yake.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo uliofanyika Septemba 7, 2023 katika ukumbi wa Chuo hicho; Mkuu wa Shule ya Afya ya Jamii Cuhas, Profesa Humphrey Mazigo ametaja mikoa ya Shinyanga, Simiyu na baadhi ya Wilaya za Tabora na Kigoma kuwa zina wanawake wengi wenye ugonjwa huo.
"Tatizo la kichocho kwenye via vya uzazi vya wanawake na mabinti limekuwepo kwa muda mrefu lakini halipewi kipaumbele kwa upande wa chuo na hospitali ya Bugando tumekuwa tukifanya tafiti mbalimbali lakini hatujawahi kujikita katika eneo hilo kwahiyo mradi huu ni maalumu kwa ajili ya akina mama na maeneo makubwa yaliyoathirika ni yale yaliyo kusini mwa ziwa Victoria”amesema
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kizazi na Uzazi kutoka Hospitali ya Rufaa Kanda Bugando, Godfrey Kaizilege amesema mradi huu unaenda kuchunguza ukubwa wa tatizo hilo na kuja na njia na mapendekezo ya namna ya kukabiliana na kulitokomeza.
"Kichocho cha uzazi kisipotibiwa kinaweza kuleta madhara mbalimbali kama ugumba, mimba kutoka, lakini pia kusababisha maumivu makali katika viungo vya uzazi kwahiyo mradi huu unakuja kuwakumbusha wanawake kwamba wanapopata dalili za magojwa kama Saratani ya uzazi basi kukumbuka kupima hata kichocho cha uzazi," amesema Kaizilege
Naibu Makamu Mkuu Cuhas katika Mipango, Fedha na Utawala, Profesa Stephen Mshana amesema utafiti huo ukikamilika utasaidia Serikali kutunga sera nzuri ya kukabiliana na janga hilo.
"Changamoto ya ugonjwa huu ni kubwa kwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa hivyo utafiti huu utaenda kuwasaidia watunga sera, kuja na mkakati mzuri wa kuweza kutokomeza tatizo hili kwasababu njia ambazo zipo ni gharama kubwa na zinapatikana katika hospitali kubwa na hazipo katika jamii kwahiyo tunaweza kuja na njia nzuri zaidi," amesema Profesa Mshana
Kwa upande wake Mganga Mkuu Mkoa wa Simiyu, Boniphace Richard amesema maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo katika Mkoa huo yanaendelea yakienda sambamba na utoaji elimu kwa wananchi.
"Sisi tayari tumeshajipanga kuhakikisha kuwa tunautekeleza kuanzia Halmashauri ya Wilaya ya Maswa na vijiji vyake kwa kuwaandaa wananchi ipasavyo kupokea mradi, kuwaelimisha namna utakavyofanya kazi lakini pia tutawaandaa wataalamu wetu waliopo katika Mkoa wetu kaunzia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa hadi ngazi ya chini," amesema Dk Richard