Utafiti wabaini sababu wakazi Arusha kuogopa kula mboga za majani

Saturday November 28 2020
utafitiiiipicmajani
By Filbert Rweyemamu

Arusha. Utafiti uliofanywa jijini Arusha na maeneo jirani umebaini kuwa dhana potofu kuwa wenye kipato cha chini ndio wanakula mboga za majani umesababisha wananchi wengi kukosa lishe bora.

Hayo yameelezwa leo Jumamosi Novemba 28, 2020 na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Profesa John Msuya wakati wa kikao na wadau wa lishe kujadili  namna ya kuhamasisha matumizi ya mbogamboga za asili kwa wingi ili kuboresha lishe kwa watumiaji.

Amesema matokeo ya utafiti huo yametokana na mradi unaolenga kuboresha kuzingatia matumizi ya mbogamboga za asili maeneo yote nchini kutokana na umuhimu wake kwa jamii licha ya watu wengi kudhani matumizi hayo ni kwa ajili ya watu wenye vipato vya chini.

“Utafiti umekuja na mambo mengi ambayo tuliyatarajia na mengine hatukuyatarajia..., jambo kubwa ambalo tumeliona ni kwamba mfumo wetu wa chakula unahitaji kuboreshwa ili uweze kutupatia hali bora ya uhakika wa chakula na lishe huku matumizi ya mbogamboga za asili yakiimarisha uendelevu wake,” amesema Profesa Msuya

Profesa Msuya amesema faida za kilimo cha mbogamboga za asili ni kustahimili hali ya hewa na mabadiliko ya tabia nchi kwa kutoshambuliwa na wadudu wasumbufu na utunzaji wake  hautumii gharama kubwa ukilinganisha na kilimo cha mbogamboga biashara.

Amezitaja mboga za asili kuwa ni mchina, mnavu, mgagani na matembele ambazo zinapaswa kuongezewa umuhimu kwenye matumizi yake.

Advertisement

Mkuu wa idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa halmashauri ya Meru mkoa wa Arusha, Grace Solomoni amesema pamoja na kuongezeka kwa kilimo cha mbogamboga wilayani Arumeru, upatikanaji wa mbogamboga za asili umekua hauhamasishwi kwa sababu wataalamu wa kilimo hawakufundishwa katika mitaala yao vyuoni.

Mratibu wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Agri ProFocus, Ernest Likoko amesema baada ya matokeo ya utafiti uliofanywa kwa pamoja watajikita kushirikiana na jamii kuhamasisha matumizi zaidi ya mbogamboga hizo ili kuimarisha lishe na uendelevu wake katika jamii.

Advertisement