Utafiti waeleza hatari wajawazito kula udongo

Fungasi na bakteria wakionekana baada ya udongo ambao wanawake hasa wajawazito wamekuwa wakila kutokana na utafiti uliofanywa na wasomi kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE).

Muktasari:

  • Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) umebaini kuwa udongo unaoliwa na wajawazito una madhara kiafya.

Iringa. Watafiti kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) wamesema udongo unaoliwa na wajawazito una madhara kiafya kwa kuwa umejaa fangasi na bakteria wenye magonjwa, hivyo kuhatarisha afya zao.

Pia, wamesema hata mazingira ya uandaaji wa udongo huo kutoka kwenye machimbo mpaka kwa mlaji hayako salama jambo ambalo pia ni hatari.

Madhara ya udongo kwa wajawazito yameelezwa katika moja ya utafiti miongoni mwa tafiti zaidi ya 60 zinazowasilishwa kwenye maonyesho ya Wiki ya Tafiti MUCE.

Akizungumza na Mwananchi leo Aprili 17, 2024, mmoja wa watafiti, Hellen Kassian amesema matokeo ya utafiti wao yanaonyesha kiwango cha bakteria na fangasi kwenye udongo ni kikubwa zaidi.

Watafiti wengine waliohusika kwenye utafiti huo ni Dk Fanuel Ligate, Amina Msonga na Moses Olotu.

Hellen amesema awali, walikwenda kwenye machimbo katika Mikoa ya Kigoma na Morogoro ambako udongo mwingi unazalishwa na kuchukua sampo za udongo ambao bado haujatengenezwa.

"Baadaye tulikwenda sokoni tukachukua udongo ulio tayari kuuzwa, huu wote tuliupeleka maabara. Tumefanya utafiti wa kisayansi kutumia mashine ya Lamina Floor, fangasi na bakteria tulio kutana nao ni wengi, wamezidi 500,000, hii ni hatari. Ulaji wa udongo sio salama kwa mama na mtoto aliye tumboni," amesema Hellen.

Amesema fangasi na bakteria waliokuwa kwenye udongo huo wanaweza kusababisha magonjwa kwa wajawazito na watoto ambao hawajazaliwa.

"Kuna mazingira mengine udongo unachimbwa ni eneo la makazi, yakishakuwa makazi huu sio salama," amesema Hellen.

Ameishauri Wizara ya Afya kuona namna ya kutoa elimu ili badala ya kula udongo, wanawake wajawazito wale chakula kingine chenye madini yanayopatikana ndani ya udongo.

"Kwanza wapewe elimu na kuambiwa madhara ya udongo lakini pia, waambie nini wanaweza kula mbadala wa udongo," amesema Hellen.

Baadhi ya wajawazito ambao hupenda udongo wamesema kinachowasukuma kula ni hamu ambayo hushindwa kuidhibiti.

"Binafsi nikila huwa napata choo ngumu sana lakini siwezi kujizuia. Watuambie tukipata hamu hiyo tule nini?" amesema Hilda Ngezi, mkazi wa Mtaa wa Mkwawa.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya, Mimea na Viuatiligu, Profesa Joseph Ndunguru amesema lengo la utafiti huo ni kuisaidia jamii kutatua changamoto zinazowakabili.

Amevishauri vyuo vikuu nchini kuendelea kufanya tafiti kama ndio msingi wa maendeleo.

"Maendeleo ya nchi yoyote duniani yanategemea tafiti. Tuendelee kufanya tafiti zenye kuleta matokeo chanya na kutatua changamoto za kijamii," amesema Profesa Ndunguru.

Wiki ya Tafiti MUCE imelenga kuonyesha kazi za watafiti na zile zitakazoonekana kuwa bora zitaenda kuwasilishwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.