Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utafiti wafichua ukatili kwa wavuvi wanawake

Wavuvi wa Mwalo wa Share jijini Tanga wakisafisha nyavu zao kwa ajili ya kurudi tana baharini kuvua samaki. Picha na Mbonea Herman

Muktasari:

  • Utafiti huo unaweka wazi umuhimu wa hatua za pamoja kutoka kwa Serikali, wadau wa maendeleo na jamii kwa ujumla katika kulinda haki za wanawake na kuhakikisha sekta ya uvuvi inakuwa jumuishi, salama na endelevu kwa wote.

Tanga. Wanawake wanaotegemea sekta ya uvuvi wa bahari kujipatia kipato, wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukatili wa kijinsia unaodhoofisha ustawi wao wa kijamii na kiuchumi, imebainika.

Hayo yamefichuliwa na utafiti uliofanywa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) katika mikoa ya Tanga, Lindi na Mtwara, ukichunguza athari za mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya uvuvi na haki za makundi yanayotegemea shughuli hiyo.

Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha baadhi ya wanawake, hususan wabebaji wa samaki maarufu ‘bodaboda wa samaki’ na wachuuzi, hulazimika kuingia katika mahusiano ya kimapenzi na wavuvi au manahodha ili kupata fursa ya kununua samaki kwa bei nafuu au kupata bidhaa kwa urahisi.

Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa matokeo ya utafiti huo kwa wavuvi wa wilayani Mkinga, mkoani Tanga leo Jumatano, Juni 17, 2026, Ofisa wa Haki za Binadamu na Biashara wa LHRC, Clay Mwaifani amesema kupungua kwa rasilimali za uvuvi kunakochangiwa na mabadiliko ya tabianchi kumeongeza ushindani katika sekta hiyo na kuchochea mazingira ya unyonyaji, pamoja na ukatili wa kijinsia.

Mmoja wa wachuuzi akiuza dagaa aina ya uono kwenye Mwalo wa Sahare jijini Tanga . Picha na Mbonea Herman

“Kadiri samaki wanavyopungua, ushindani unaongezeka na kusababisha wanawake kuwekwa katika mazingira hatarishi ya kunyanyaswa ili waweze kuendesha shughuli zao,” amesema.

Mbali na kubaini changamoto hizo, utafiti huo pia unapendekeza kuanzishwa kwa mifuko rafiki ya kifedha itakayowawezesha wavuvi kupata mikopo yenye riba nafuu kupitia vyama vya ushirika, ili waweze kumiliki au kukodisha boti za uvuvi na kufikia maeneo yenye rasilimali nyingi zaidi.

Pia, unapendekeza kuboreshwa kwa mifumo ya utoaji wa taarifa za hali ya hewa kwa wakati kupitia ushirikiano kati ya mamlaka husika, halmashauri na Vikundi vya Usimamizi wa Fukwe (BMU), hatua itakayosaidia wavuvi kufanya maamuzi sahihi na kuepuka hatari za baharini.

Kuhusu ushirikishwaji wa kijinsia, Mwaifani amesema licha ya kuwepo kwa sera na sheria zinazosisitiza uwakilishi wa wanawake katika vyombo vya maamuzi, bado sauti zao hazisikiki ipasavyo.

“Ni muhimu kutoka katika dhana ya ujumuishi na kuelekea kwenye ushirikishwaji halisi unaowapa wanawake nafasi ya kutoa maoni na kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayowahusu,” amesema.

Kwa upande wake, Ofisa Mkuu wa Uchunguzi wa LHRC, Chrisantus Ndibaiukao amesema utafiti huo pia umebaini kushuka kwa kipato cha wavuvi pamoja na ukosefu wa uwakilishi madhubuti katika ngazi za juu za maamuzi.

Wavuvi wa Moa katika wilaya ya Mkinga mkoani Tanga akisikiliza matokeo ya utafiti wa kuchunguza  athari za mabadiliko ya tabia nchi  katika sekta ya uvuvi. Picha na Mbonea Herman.

Amesema kuna haja ya kuimarisha vyombo vya uwakilishi wa wavuvi ili kuhakikisha sauti zao zinasikika katika utungaji wa sera na mipango ya maendeleo ya sekta hiyo.

Wakichangia matokeo ya utafiti huo, baadhi ya wanachama wa Umoja wa wanawake wavuvi wamesema ripoti hiyo inaakisi hali halisi wanazokutana nazo kila siku, ikiwamo ukosefu wa mitaji, mazingira magumu ya kazi na vitendo vya unyanyasaji.

Katibu wa BMU Zingibari, Mwanakombo Hassan amesema wanawake wengi hulazimika kuingia katika mahusiano yasiyo rasmi ili kupata samaki, hali inayowaweka katika mazingira magumu zaidi.

“Nguvu ya kupata bidhaa imekuwa ikihusishwa na mahusiano, jambo linalowalazimisha wanawake wengi kuingia katika uhusiano bila hiari,” amesema.

Naye mkazi wa Moa, Rehema Ally, amesema ukatili huo umekuwa kikwazo kikubwa kwa wanawake wanaojishughulisha na uvuvi na kuwataka wadau kuchukua hatua za haraka kuboresha mazingira ya kazi.

“Ukatili huu unatunyima fursa ya kufanya kazi kwa uhuru na usalama. Tunahitaji suluhisho la haraka ili wanawake waweze kufanya kazi bila shinikizo wala hofu,” amesema.