Prime
Uteuzi wa Matinyi wawaibua wadau
Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi.
Dar es Salaam. Wiki moja baada Rais Samia Suluhu Hassan kumhamisha aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amemteua Mobhare Matinyi kuziba nafasi hiyo, huku wadau wa habari wakijitokeza kuusifu.
Katika mabadiliko hayo, Msigwa aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, kabla ya kuhamishiwa kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo.
Taarifa ya uteuzi wa Matinyi aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, ilitolewa juzi usiku na Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Zuhura Yunus.
Uteuzi huo umepokelewa kwa furaha na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), ambalo katika taarifa kwa vyombo vya habari ya jana, limesema lina matarajio, kuwa Matinyi atakuwa kiunganishi kati ya vyombo vya habari na Serikali.
“Kuna uundwaji wa vyombo vya habari vilivyoanzishwa kupitia Sheria za Huduma za Habari ya mwaka 2016 kama ilivyorekebishwa mwaka 2023, jukumu ambalo lilishindikana tangu mwaka 2016. Tunaamini sasa ni wakati mwafaka alisimamie suala hili, ili viundwe,” alisema.
TEF pia imegusia uchumi wa vyombo vya habari ikisema kuwa hali hiyo mbaya imesababisha kushusha ubora wa habari.
“Kutokana na ukweli huu, tunaamini ni wakati mwafaka wa Serikali kutenga bajeti ili kuhakikisha vyombo vya habari vinapata matangazo ya kutosha na kuwa na uwezo kiuchumi, hali itakayoongeza ubora wa maudhui,” alisema.
Nacho Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kupitia taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana, Katibu Mkuu, Alfred Lucas kilimpongeza Matinyi kwa kuaminiwa na kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali.
“TASWA tunamtakia kila la kheri katika nafasi hiyo aliyoaminiwa na Mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan, ambaye pia anastahili pongezi kwa uteuzi huu,” ilisema taarifa.
Mobhare Matinyi ni nani?
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, Matinyi ni mwandishi wa habari na mtaalamu wa sayansi ya siasa.
Alianza uandishi wa habari mwaka 1993 alipojiunga na Business Times Ltd akiwa mchora vibonzo. Mwaka 1995 alikwenda nchini India ambako alisomea shahada ya kwanza ya Sanaa katika sayansi ya siasa, uchumi na utawala katika Chuo Kikuu cha Osmania. Pia alisomea stashahada ya uandishi wa habari.
Aliporudi mwaka 1998 alijiunga tena na kampuni hiyo na kuwa mhariri wa gazeti la Spoti Starehe.
Mwaka 2000 aliteuliwa kuwa mhariri wa gazeti la Majira na wakati huo pia aliwahi kuwa mhariri wa gazeti la Dar Leo, kazi alizofanya hadi mwaka 2003.
Mwaka 2001 hadi 2002 alikuwa pia akifundisha Chuo cha Uandishi wa habari (TSJ) sasa Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mwaka 2003 alikwenda nchini Marekani kuendelea na masomo ambako alisoma shahada ya uzamili ya mawasiliano katika siasa katika Chuo Kikuu cha Johns Hopkins.
Baada ya hapo, alisoma shahada nyingine mbili za uzamili ikiwamo ya mikakati na nyingine ya uhusiano wa kimataifa na utatuzi wa migogoro.
Akiwa huko pia aliajiriwa katika taasisi ya Mambo ya Nje (Foreign Services) ya Washington DC akiwa mhadhiri kwa miaka mitano.
Katika kipindi hicho alikuwa mchambuzi wa masuala ya siasa na alikuwa akitoa maoni yake katika vyombo vya habari vya kimataifa kama Sauti ya America (VOA), Radio France International (RFI) na BBC na pia alikuwa na safu yake iitwayo With an Eagle Eye katika gazeti la The Citizen mwaka 2008 hadi 2013.
Aliporudi nchini mwaka 2013 aliajiriwa kuwa mtumishi wa umma katika Ofisi ya Rais.
Kati ya mwaka 2013 na 2014 alifundisha Chuo cha Diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa Kurasini Dar es Salaam, sasa kikijulikana kama chuo cha Dk Salim.
Baada ya hapo alikwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) akifanya kazi na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Africa (Sadc).
Aliporudi nchini alianza kusoma shahada ya uzamivu (PhD) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2021 anayoendelea nayo hadi sasa akisoma Sayansi ya siasa (usalama wa kimataifa).
Julai 3, 2023 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke hadi Oktoba 1 alipoteuliwa kuwa Msemaji mkuu wa Serikali.
Amekuwa pia akitoa mada katika Chuo cha Ulinzi cha Taifa kilichopo Kunduchi, Dar es Salaam.