Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utoaji silaha usivyofuata utaratibu

Dar/mikoani. Itakuhitaji kuwa na subira ya miaka kadhaa ili kupata kibali cha kumiliki silaha kwa njia halali nchini, tangu mwaka 2019.
Ugumu wa upatikanaji wa vibali hivyo, unatajwa kuchagizwa na uwepo wa mtandao wa watoaji wa vibali kwa mlango wa nyuma, uliogeuza suala hilo kuwa kitega uchumi kwa miaka kadhaa.

Mwananchi imedokezwa na vyanzo mbalimbali juu ya uwepo wa mtandao huo, unaosababisha umiliki wa silaha kwa watu wasio na sifa.

Kama hiyo haitoshi, Mwananchi imedokezwa Aprili mwaka huu kuwa maofisa wanane wa Jeshi la Polisi nchini katika mikoa ya Arusha, Mwanza na Dodoma waliwajibishwa baada ya kushtakiwa kijeshi kwa kosa la utoaji vibali hivyo kinyume na utaratibu.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, baadhi ya watu walitozwa kati ya Sh1.5 milioni na Sh2 milioni kumiliki bastola na Sh1 milioni na Sh1.5 milioni kumiliki bunduki, bila kujadiliwa na kikao chochote.
 

Utaratibu wa kuomba silaha

Hayo yanafanyika wakati utaratibu wa kisheria wa kumiliki silaha unahitaji, kujaza fomu ya maombi na kujadiliwa katika kata anayoishi, kisha maombi yatapelekwa kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), atakayewasilisha katika kamati ya usalama ya wilaya husika.

Baada ya kuwasilishwa huko, waombaji huitwa na kujadiliwa na kamati hiyo na baada ya kupitishwa yanarudishwa kwa OCD, ili ayawasilishe kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC).

RPC atayawasilisha kwa kamati ya usalama mkoa na muombaji ataitwa kwa ajili ya mahojiano.

Licha ya kuwepo kwa utaratibu huo, vyanzo mbalimbali vimelieleza gazeti hili kuwa baadhi ya watu wenye fedha huandaa mpango na watu kutoka ofisi mbalimbali za mchakato wa maombi na hatimaye humilikishwa silaha bila mahojiano.

Kulingana na vyanzo hivyo, uwepo wa mbinu hizo chafu ndiyo sababu ya maombi mengi ya umiliki wa silaha za moto kukwamia kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhan Kingai.

Kasoro hizo zinabainishwa kipindi ambacho Ripoti ya Tume ya Haki Jinai iliyoangalia jinsi ya kuboresha taasisi za haki jinai nchini ikibainisha dosari ndani ya Jeshi la Polisi na kupendekeza kufanyika kwa tathimini kubwa ya kulifumua kimuundo na kimfumo.
Ripoti hiyo ilikabidhiwa Julai 15, mwaka huu kwa Rais Samia Suluhu Hassan na wajumbe wa tume hiyo iliyoongozwa na mwenyekiti, Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Othuman Chande.
 

Mtandao Polisi ulivyonaswa

Vyanzo hivyo vinafafanua, mtandao huo uligundulika baada ya mfanyabiashara mmoja kubainika amenunua na anamiliki silaha haraka, huku akicha msongamano wa maombi lukuki.

“Katika uchunguzi ndio ikabainika wala hakuwahi kujadiliwa na kikao chochote na polisi aliyeshiriki akamtaja polisi ambaye ana cheo cha mkaguzi yuko makao makuu Dodoma ambaye naye akakamatwa,” kilidokeza chanzo hicho.

Uratibu wa kupata kwake silaha, ulibainika baada ya simu yake kuchunguzwa na hilo alilifanya katika mikoa ya Mwanza na Arusha.

“Kule Arusha kwa maelezo yalivyo ni kama yule dada (polisi) alionewa kwa sababu ukisikiliza hiyo hadithi hao jamaa walianzia kwa bosi wake ndio bosi akampa maelekezo huyo polisi naye akawasiliana na mhusika makao makuu.

“Huko ndio aliambiwa kiwango naye akarudisha jibu kwa bosi, bosi akawaambia wahusika. Unajua polisi hupokea amri na huwezi kukataa lakini sasa bosi kahamishwa, lakini yule dada kafukuzwa kazi,” kilidokeza chanzo hicho.

Chanzo hicho kinaeleza wafanyabiashara hao walimilikishwa bastola moja na bunduki moja na kwamba katika makao makuu Dodoma, mtandao huo ulihusisha maofisa wanne ambao ndio walitengeneza nyaraka na kumpelekea DCI aidhinishe.
 

Waombaji silaha walalama

Mmoja wa maofisa wastaafu wa Jeshi la Polisi aliyeomba silaha (jina linahifadhiwa), alisema tangu mwaka 2018 aliomba kibali hicho bila mafanikio, wakati wapo wanaopata kabla yake.

“Fikiria nilikuwa askari nimeomba silaha tangu 2018 na nimejadiliwa kuanzia kwenye kata, wilaya hadi mkoa, lakini leo hii ukifanya uchunguzi kuna vijana wadogo wala hawastahili kumiliki silaha kwa rekodi zao lakini wanamiliki,” amesema.
Mwombaji mwingine ambaye naye aliyeomba jina lake lihifadhiwe, alisema ni mwaka wa tatu sasa tangu afuate taratibu zote, lakini hajapewa kibali wala kuelezwa sababu ya kutopewa.

“Jeshi la Polisi liweke wazi ni wangapi wamebainika walipata vibali bila kufuata taratibu kwa sababu kuna maneno wapo wanaopita juu kwa juu na wana vitabu mitaani na silaha. Tuambiwe polisi wangapi na raia wangapi walihusika,” amesema.
Mwaka 2021 na 2022 baada ya kutokea mauaji ya kiholela na mengi yakihusisha vijana wanaotoka mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara, wananchi walipaza sauti wakitaka ukaguzi maalumu ufanyike wakidai wengine hawana sifa.

Mkesha wa mwaka mpya 2022 uligeuka shubiri huko mkoani Kilimanjaro, baada ya Jeshi la Polisi kueleza kuwatia mbaroni wamiliki wa silaha hususan bastola wanaodaiwa kufyatua risasi hovyo katika mazingira tofauti.
 

Waombaji wamepungua

Kutoka mkoani Manyara na Arusha, Mwananchi lilizungumza na baadhi ya viongozi waliosema idadi ya waombaji imepungua tofauti na miaka ya nyuma.

Kupungua kwa maombi hayo, kunatajwa kusababishwa na kupungua kwa matukio ya uhalifu hasa ujambazi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Vilimavitatu wilayani Babati, Abubakari Msuya alisema tangu mwaka 2019 alipochaguliwa hajawahi kupokea maombi ya umiliki wa silaha.

Kuimarika kwa ulinzi na usalama, alizitaja kuwa miongoni mwa sababu zilizochangia kupungua kwa maombi hayo. Maelezo ya Msuya, yanafanana na kile kilichoelezwa na ofisa mtendaji wa Kata ya Sakina mkoani Arusha, Kisarika Joackim amesema, “muda mrefu hatujapokea maombi, tofauti na zamani walikuwa wanakuja mmoja mmoja, lakini sasa hakuna kabisa.”

Akizungumzia hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), George Katabazi alisema, “huwa kuna muda maalumu ukifika kulingana na maombi vikao vinakaa kujadili na kupitisha walioomba kumiliki silaha, lakini ni lazima utaratibu ufuatwe kuanzia ngazi za chini.”

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Jastine Masejo alikiri kupungua kwa maombi ya watu binafsi kumiliki silaha, isipokuwa kwa sasa zinazoomba ni kampuni za ulinzi na wawindaji wa kitalii.

Julius Mallya, ofisa mstaafu wa jeshi la polisi, alisema uchche wa maombi hayo unasababishwa na kuimarika kwa ulinzi na usalama kuanzia maeneo ya kazi, nyumbani na maeneo ya biashara.

“Miaka ya nyuma kila mara watu walikuwa wakivamiwa na majambazi na kuporwa, lakini sasa ujambazi umepungua sana,” amesema.

Ofisa mtendaji wa moja ya kata mkoani Mwanza, aliyeomba hifadhi ya jina lake, alisema mwaka 2022 kamati ya ulinzi na usalama ya kata hiyo ilikaa vikao vitatu kujadili wananchi waliowasilisha fomu katika ofisi yake kuomba kibali cha kumiliki silaha.
Kati yao, alisema wawili walikidhi vigezo na maombi yao yalipelekwa hatua zinazofuata kwa ajili ya kuchakatwa.

“Huyo mmoja wajumbe wa kamati walikataa kumjazia fomu yake kwa sababu aliwahi kukumbwa na tuhuma za kutishia mtu maisha,” amesema.
Katika Mkoa wa Geita, ofisa mtendaji wa kata ya Kalangalala, Hamad Hussein alisema kwa miaka mitatu sasa hajapokea maombi hayo.

“Sijui kama ni mwamko wa kumiliki silaha hawana au vipi, lakini ofisi niliyoko hakuna mwananchi aliyefika kuomba kumiliki,” amesema.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Gideon Msuya alisema hana takwimu halisi za watu waliowasilisha maombi hayo.
Hata hivyo, mwaka 2021, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene aliahidi kutolewa kwa ripoti ya umiliki holela wa silaha, ambayo hadi sasa haijatolewa.
 

Kilichoelezwa na Polisi

Msemaji wa Jeshi Polisi, David Misime alisema maombi ya silaha huongozwa na sheria na yanahitaji umakini kwa kuwa kuna matumizi mbalimbali ikiwemo ulinzi na kujilinda.

“Sheria imeainisha taratibu za kufuata kwa anayeomba kumiliki silaha kwa ajili ya ulinzi binafsi na mali zake.

“Mtu anapoomba kumiliki silaha taratibu zinaelekeza apitie hatua mbalimbali ikiwepo katika kamati ya usalama ya wilaya na mkoa, lengo likiwa ni kuona na kujiridhisha kama mtu anayeomba ana sifa zilizoainishwa katika Sheria ya Udhibiti wa Silaha na Risasi ya 2015 na Kanuni zake za 2016 hasa kifungu cha 11,” amesema.

Hatua ya kuchukua muda mrefu kwa baadhi ya maombi, aliwataka waombaji wasubiri kwa kuwa uchunguzi wa vigezo vya kumiliki silaha hauhusishi vikao pekee.
Dhamira ya ufuatiliaji huo ni kile alichokieleza, baadhi waliwahi kumilikishwa na wakakiuka masharti.

“Tumeshuhudia wengine wakipiga risasi watu kwenye baa na kuua, kujeruhi, kutishia familia na wengine, kuibiwa na wakati mwingine wanashindwa kujitetea,” alisema.
Kwa sababu hizo, alisema si kila anayedhani ana uwezo wa kumiliki silaha kwa ana vigezo stahiki.

Kuhusu maofisa waliotimuliwa, kamanda huyo alikiri uwepo wa suala hilo baada ya uchunguzi na kuthibitika kwa tuhuma dhidi yao.

“Hizo ndizo taratibu zinazochukuliwa dhidi ya askari anayekiuka kiapo chake na kwenda kinyume na mwenendo mwema wa Jeshi la Polisi pamoja na sheria za nchi kwa sababu ushahidi unaonyesha,” alisema Misime.