Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utulivu watanda nchini, shughuli zikiendelea kwa tahadhari, ulinzi waimarishwa

Muktasari:

  • Idadi ya watu katika maeneo mbalimbali kwenye baadhi ya mikoa imeonekana kuwa ndogo huku maduka mengi yakifungwa na kufanya mdororo wa shughuli za kiuchumi.

Dar/mikoani. Hali ya utulivu na ukimya imetawala katika mitaa na maeneo mbalimbali nchi ikiwemo Dar es Salaam, jiji la kibiashara. Maduka yamefungwa. Daladala za kuhesabu. Hakuna pilikapilika.

Hata Mwenge, Kimara Mwisho, Kimara Suka na Ubungo, ambazo nyakati zote huwa na shughuli na pilika nyingi, nazo zimetulia. Ni askari wa Jeshi la Polisi na Bodaboda chache ndizo zilizoonekana.

Ile Sinza ya biashara na maduka ya nguo, viatu na urembo wa binadamu, imebadilika kuwa eneo tulivu, hakuna fremu ambayo geti lake liliachwa wazi. Zote zimefungwa hadi mchana wa  Julai 7, 2026. Mvua zinazoendelea kunyesha jijini humo zinawafanya watu kusalia majumbani.

Hali hiyo inatokana na taarifa za kufanyika kwa maandamano huku Serikali ikiyapinga marufuku na kuonya watakaoandamana wakakutana na mkono wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Pia Mwananchi limepita maeneo mbalimbali mikoani ukiwamo wa  Mbeya, Mwanza, Iringa, Dodoma, Shinyanga na Kilimanjaro kuona kinachoendelea huko.


Hali ilivyo Mbeya

Shughuli za uzalishaji kiuchumi zimeonekana kudorora kufuatia maduka mengi jijini Mbeya kufungwa huku ulinzi na usalama ukiimarishwa katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.

Magari ya Jeshi la Wananchi yakiwa yameimarisha ulinzi na usalama katika eneo la Kabwe jijini Mbeya

Mbali na maduka na masoko kufungwa, hali ya usafiri imeonekana kuwa adimu kwa daladala huku pikipiki na bajaji zikionekana kutawala zaidi jijini humo.

Jioni ya Leo Julai 7, 2026 wananchi mkoani Songwe katika maeneo tofauti tofauti wakiendelea na shughuli zao kama kawaida. Picha na Denis Sinkonde

Hadi saa 6:30 mchana leo Julai 7, 2026, Mwananchi imepita baadhi ya maeneo ikiwa ni soko la Soweto, Stendi ya daladala Kabwe, Sido, Soko la Mwanjelwa na kushuhudia kutokuwapo shughuli za kiuchumi kama inavyokuwa siku zote.

Hata hivyo, idadi ya watu barabarani ni ndogo huku zile hekaheka zilizozoeleka kwa siku za kawaida zikipotea na kufanya jiji kuwa tulivu.

Magari ya Jeshi la Polisi na Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ) yakiwa na askari zilionekana katika maeneo ya Kabwe na nyingine eneo la Mataa wakiimarisha ulinzi na usalama.

Bidhaa mbalimbali zikiwa zimepangwa  na wafanyabiashara kusubiri wateja katika Soko la Mabatini jijini hapa. Picha na Hawa Mathias

Pamoja na mabadiliko hayo ya kimazingira, hali ilionekana kutulia huku wachache waliokuwa wakifanya shughuli zao wakiendelea bila hofu.

Jana Julai 6 wakati wa jioni, ilishuhudiwa idadi kubwa ya wananchi katika masoko tofauti wakifanya manunuzi hasa katika eneo la Sido.

Jioni ya Leo Julai 7, 2026 wananchi mkoani Songwe katika maeneo tofauti tofauti wakiendelea na shughuli zao kama kawaida. Picha na Denis Sinkonde

Mmoja wa waendesha bajaji, Simon Tengwa amesema taarifa za maandamano mitandaoni huenda zimechangia kiasi fulani kusababisha mabadiliko hayo akieleza kuwa hali hiyo inawapunguzia utafutaji.

"Watu wanaogopa kutoka jana walipishana sana sokoni kununua vitu wakidhani huenda hali ikachafuka, kwetu sisi ni pigo kwa kuwa tunapaswa kurejesha pesa kwa bosi,”amesema Tengwa.


Kinachoendelea Iringa

Wakati hayo yakiendelea Mbeya, mkoani Iringa hali ya usalama katika Manispaa ya Iringa imeendelea kuwa tulivu huku wananchi wakiendelea na shughuli zao za kila siku katika maeneo mbalimbali ya mji bila kuripotiwa matukio ya uvunjifu wa amani.

Katika maeneo ya biashara, Mwananchi imeshuhudia baadhi ya wafanyabiashara wamefungua maduka yao na kuendelea kuwahudumia wateja.

Hata hivyo, harakati za wananchi zimeendelea kuonekana katika masoko, vituo vya usafiri na maeneo mengine ya biashara na mmoja wa wafanyabiashara wa eneo la Mlandege, John Mwabela, amesema alifungua biashara yake mapema na idadi ya wateja ilikuwa ya kawaida lakini ni ndogo ikilinganishwa na siku nyingine.

"Nimefungua biashara yangu kama kawaida tangu asubuhi. Hali ni tulivu, lakini wateja bado si wengi. Tunaendelea kusubiri kuona biashara itakavyokuwa hadi jioni," amesema.

Mkazi wa Iringa, Neema Mwasi, amesema ameamua kuendelea na shughuli zake za kawaida kwa kuwa mazingira ya mji yalikuwa ya amani.

"Nimetoka kwenda sokoni na kufanya manunuzi kama kawaida. Hali ninayoiona ni ya utulivu na watu wanaendelea na shughuli zao," amesema.

Naye dereva wa bodaboda, Juma Msile, amesema huduma za usafiri zimeendelea kutolewa bila changamoto kubwa, ingawa idadi ya abiria imeonekana kupungua katika baadhi ya maeneo.

"Tunaendelea kufanya kazi kama kawaida. Abiria si wengi sana asubuhi, lakini tuna matumaini shughuli zitaongezeka kadri siku inavyoendelea," amesema.

Aidha katika masoko na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu, wananchi wameendelea kufanya manunuzi huku baadhi ya biashara zikiendelea kufunguliwa hatua kwa hatua.


Shinyanga

Katika Manispaa ya Shinyanga imeonekana kuwa ya utulivu huku shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi zikiendelea kama kawaida katika maeneo mengi ya mji, wananchi wameonekana wakiendelea na shughuli zao za kila siku bila kuwepo kwa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyoripotiwa.

Baadhi ya wafanyabiashara wamefungua maduka yao na kuendelea kutoa huduma kwa wateja, huku wengine wakiamua kutofungua biashara zao, hali hiyo imeonekana katika maeneo mbalimbali ya biashara ndani ya manispaa, ambapo shughuli zimeendelea kwa viwango vinavyotofautiana kulingana na eneo husika.

Katika masoko na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu, wananchi wameendelea kufanya manunuzi na shughuli nyingine za kawaida, huku baadhi ya wafanyabiashara wakiwa wamefunga, harakati za watu zimeendelea kuonekana katika sehemu mbalimbali za mji.


Dodoma ulinzi ni fimbo

Wakati hali ya usalama ikionekana kuwa shwari katika jiji la Dodoma, imeshuhudiwa mtindo tofauti wa ulinzi ambao umetumiwa na Polisi walioonekana kwa baadhi ya maeneo ikiwemo waliozunguka jengo la Bunge.

Tofauti na ilivyozoeleka ambapo kwenye ulinzi kama huu bunduki huwa nyingi, Polisi katika Jiji la Dodoma, wengi wameonekana kuwa na fimbo mikononi wakati waliobeba silaha za moto ni wachache kwa kuhesabu.

Hadi saa 5:18 asubuhi ya leo Julai 7,2026, hakukuwa na tukio la aina yoyote lililoashiria uvunjifu wa amani ingawa polisi walionekana maeneo mengi wakitembea wawiliwawili na wote wakiwa wamebeba fimbo mikononi mwao.

Ulinzi mkali wa Polisi umeonekana katika jengo la Bunge ambako kila lilipo lango la kuingia walisimama polisi wawili na wote wakiwa na fimbo bila silaha isipokuwa lango Kuu maarufu (Lango la Waziri Mkuu) ndiko lilionekana gari la washawasha na polisi wenye silaha za moto wachache, huku baadhi wakikaa pembeni wakiwa na fimbo zao mikononi.

Maeneo mengine ambayo Polisi wameonekana, ni Nyerere Square, Four way, Chako ni chako na mzunguko wa uwanja wa ndege, pembeni mwa soko la majengo karibu na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, One way karibu na benki ya NMB na Barabara ya UDOM.

Hata hivyo, katika maeneo mengi kumeonekana kuwa na utulivu na idadi ndogo ya magari barabarani lakini huenda hali hiyo inatokana na kuwa leo ni siku ya mapumziko hivyo watu wengi wapo majumbani.

Kwenye vijiwe vya bodaboda shughuli zinaendelea kama kawaida na wafanyabiashara wamefungua biashara zao na kwa wale wanaopenda kutumia eneo la Nyerere Square kama sehemu ya mapumziko walikuwepo pia hasa vijana.


Biashara nyingi zafungwa

Jijini Arusha, hali imekuwa tofauti na ilivyozoeleka katika siku nyingine za mapumziko ya Sikukuu ya Sabasaba, ambapo hadi kufikia saa sita mchana biashara nyingi, ikiwemo maduka makubwa, zilikuwa zimefungwa.

Mwananchi imeshuhudia idadi ya watu katika barabara mbalimbali za katikati ya jiji ikiwa ndogo huku usafiri wa umma ukiwemo daladala, bodaboda na bajaji ukiwa na mwitikio mdogo kuliko ilivyo kawaida.

Katika maeneo ya biashara, ikiwemo Soko Kuu la Arusha, mpaka saa 4:09 asubuhi kulikuwa na wafanyabiashara na wanunuzi wachache, hali iliyoashiria kupungua kwa shughuli za kiuchumi.

Katika Barabara ya Sokoine, kulipo na maduka makubwa ya biashara,hadi saa tano asubuhi maduka karibia yote yalikuwa hayajafunguliwa.

Hali ya Mkoa wa Tanga ulinzi ukiimarishwa wanachi wanaendelea na shughuli zao za kawaida.

Wakati huohuo, hali ya ulinzi imeendelea kuimarishwa katika maeneo mbalimbali ya jiji, ikiwemo Sanawari, Phillips na Mnara wa Saa, ambapo askari wa Jeshi la Polisi waliovalia sare wameendelea kuwepo kwa ajili ya kuimarisha usalama.


Mwanza kukoje?

Jijini Mwanza baadhi ya wananchi wameendelea na shughuli zao huku Jeshi la Polisi likiimarisha ulinzi katikati ya mji.

Mwananchi imeshuhudia, kama zilivyo siku za sikukuu za umma ikiwemo ya Sabasaba, idadi ya watu huwa ni ndogo maeneo kama ya mjini kati, na ndivyo hali ilivyo katikati ya mji.

Shughuli katika soko la samaki la Lamadi wilaya ya Busega mkoani Simiyu zikiendelea kama kawaida. Picha na Samwel Mwanga

Shughuli za usafirishaji nazo zinaendelea kama kawaida ukiwemo usafiri wa daladala, bodaboda na bajaji ambao ni usafiri unaotumika sana jijini Mwanza.

Maeneo ya kituo kikuu cha mabasi Tabora shughuli zikiendelea kama kawaida.

Baadhi ya maduka yamefungwa, huku masoko nayo yakiwa na mwitikio mdogo wa wafanyabiashara na wateja.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema ulinzi mkoani humo ni wajibu wa Jeshi la Polisi.

“Niendelee kuwashauri wananchi waendelee na shughuli zao wasipo kuwa na hofu ya aina yoyote kwa sababu ni wajibu wetu sisi kama Jeshi la Polisi kulinda wananchi na mali zao,” amesema Kamanda Mtafungwa mchana huu.

Aidha, Kamanda Mutafungwa ametoa wito kwa watu wenye nia ya kusababisha uvunjifu wa amani kuacha mara moja, kwani Jeshi la Polisi limejipanga imara na yeyote atakayejaribu atadhibitiwa kwa mujibu wa sheria.


‘Hakuna tishio la usalama Kilimanjaro’

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema hakuna tishio lolote la kiusalama mkoani humo na kuwataka wananchi kuendelea na shughuli zao bila hofu huku likisisitiza umuhimu wa kuendelea kutii sheria wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya Sabasaba.

Maigwa amesema Mkoa wa Kilimanjaro umeendelea kuwa na utulivu, huku wananchi wakiendelea na shughuli zao za kila siku na vyombo vya ulinzi na usalama vikiendelea kutekeleza majukumu yake ya kawaida.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu (wa tatu kushoto) akiwa na wajumbe wa kamati ya usalama, wakiteta jambo na baadhi ya wananchi huku wakiburudika kwa kahawa kwenye kijiwe cha kahawa eneo la Manyema mjini Moshi baada ya kuzunguka maeneo mbalimbali ya mji huo kuangalia hali ya usalama leo Julai 7, 2026. (Picha na Mpiga Picha Wetu)

"Mkoa wa Kilimanjaro ni shwari sana. Maeneo yote yako salama na wananchi wanaendelea na majukumu yao. Kama unavyojua Kilimanjaro, kipindi cha sikukuu watu wengi huenda milimani kuwasalimia ndugu na marafiki. Mkoa wetu uko salama na hakuna woga wowote," amesema Maigwa.

Wakati huohuo, Mwananchi lilipotembelea maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Moshi kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 6:45 mchana, lilibaini shughuli za biashara, usafirishaji na huduma nyingine za kijamii zikiendelea kama kawaida, huku maduka, masoko na taasisi mbalimbali zikiendelea kutoa huduma.

Vyombo vya usafiri wa umma, vikiwemo mabasi ya mikoani, daladala, teksi na bodaboda, vimeendelea kutoa huduma kama kawaida, huku hadi kufikia mchana harakati za wananchi zikiendelea kwa utulivu.


Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi wamesema wameendelea na shughuli zao kama kawaida huku wakieleza kuwa doria za askari katika maeneo mbalimbali zimewaongezea utulivu.

"Sisi tunaendelea na kazi zetu kama unavyoona, hakuna vurugu wala dalili yoyote ya maandamano. Maisha lazima yaendelee," amesema Oscar Madirisha, dereva wa bodaboda katika Stendi Kuu ya Moshi.


Imeandikwa na Juma Issihaka, Bakari Kiango (Dar) Habel Chidawali na Rachel Chibwete (Dodoma), Janeth Mushi (Arusha), Saada Amir, PraiseGod Mgumba (Mwanza) na Yese Tunuka (Kilimanjaro