UVCCM Arusha wamtimua mwenyekiti wao

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) mkoani humo, Lengai ole Sabaya

Muktasari:

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shaaban Mdoe alisema kamati hiyo pia imeagiza Sabaya asimame kuiwakilisha jumuiya hiyo katika vikao vyote.

Arusha. Kamati ya Siasa ya Halmashauri ya CCM Mkoa wa Arusha, imependekeza kuvuliwa uanachama na madaraka Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) mkoani humo, Lengai ole Sabaya ambaye anashtakiwa kwa kujifanya ofisa usalama wa Taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shaaban Mdoe alisema kamati hiyo pia imeagiza Sabaya asimame kuiwakilisha jumuiya hiyo katika vikao vyote.

“Kutokana na kuwa diwani wa CCM Kata ya Sambasha, vikao vya chama vya kata na wilaya yake vinapaswa kukaa na kumjadili kuhusiana na uadilifu wake ili hatua za kumfukuza uanachama ziweze kuchukuliwa,” alisema.

Mdoe alisema kamati hiyo imebaini Sabaya siyo mwadilifu, anatuhuma kwa makosa mbalimbali yaliyoripotiwa polisi na mengine yapo mahakamani.

Alisema wamepokea waraka kutoka kwa Kamanda wa Polisi mkoani humo, Charles Mkumbo wenye kumbukumbu namba ARR/C.5/4/VOL/57/59 wa Sept 21 ambao unaeleza tuhuma mbalimbali za Sabaya.

“Sabaya amekiuka kanuni za maadili na uongozi kifungu cha tatu (5) 1-2 na kifungu cha nne(4)1-III ambavyo adhabu zake ni kuvuliwa uanachama na kuachishwa uongozi,” alisema.

Alifafanua kuwa kamati hiyo ambayo ilimhoji Sabaya, pia imeridhia kufukuzwa kazi Katibu wa UVCCM mkoani humo, Ezekiel Mollel kwa kutotii mamlaka yake ya ajira na utovu wa nidhamu baada ya kugoma kuhamia makao makuu ya umoja huo.

Akizungumzia uamuzi wa kamati na ule wa kamati ya utekelezaji Taifa, Sabaya alisema tuhuma nyingi siyo za ukweli .

“Sijapata barua rasmi ya uamuzi wao, lakini sipendi kuongelea sana suala hili na nitazungumza baada ya kuipata kwa kuwa lipo mahakamani, kwani tuhuma nyingi siyo za kweli,” alisema.