Uwanja wa ndege Zanzibar waanza kutumia madaraja ya kupitia abiria

Muktasari:

  •  Baada ya miezi kadhaa tangu Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA) kutiliana saini na kampuni ya kimataifa ya Dnata kuendesha Uwanja wa Ndege wa Abeid Aman karume Terminal 3, sasa uwanja huo umeanza rasmi kutumia madaraja ya kupitia abiria (PBB).


Unguja. Baada ya miezi kadhaa tangu Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA) kutiliana saini na kampuni ya kimataifa ya Dnata kuendesha Uwanja wa Ndege wa Abeid Aman karume Terminal 3, sasa uwanja huo umeanza rasmi kutumia madaraja ya kupitia abiria (PBB).

Mbali na huduma hiyo ya PBB, uwanja huo pia umeanza kutumia mitambo ya inayomsaidia rubani kuegesha ndege (VEDS) bila kuwapo kwa muongoza ndege kama ilivyozoeleka.

Madaraja hayo ya kisasa yanatumiwa na abiria wakati wa kupanda na kushuka badala ya kutumia ngazi za kawaida hivyo kuwafanya abiria wawe katika hali ya usalama zaidi.

Novemba 24, 2021 Serikali ya Zanzibar ilisaini mkataba wa kuendesha uwanja huo kwa kushirikiana na kampuni za kimataifa katika kuboresha huduma za abiria na mizigo yao kuwa katika hali ya usalama tofauti na kutumia ngazi.

Mikataba hiyo iliyosainiwa na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Mawasilino na Uchukuzi Zanzibar, Rahma Kassim Ali na kampuni hiyo huku ikishuhudiwa na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi, alisema nia wanataka huduma zinazotolewa katika uwanja huo ziwe za kimataifa.


Akizungumza baada kuanza rasmi matumizi hayo leo Aprili Mosi, 2022, Ofisa Uhusiano wa ZAA, Mulhat Yussuf Said, alisema Shirika la ndege la Edelweiss la nchini Uswiss limekuwa la kwanza kutumia huduma hiyo.


“Huduma hii ni ya kimataifa, maana hata abiria anaposhuka na kupanda haonekani anapita ndani kwa ndani kwenye hizo PBB, kwanza yanaongeza hali ya usalama maana kuna wakati mwingine abiria akiwa anashuka kwa kutumia njia ile ya kawaida kama ndege kubwa anakuwa anaogopa akidhani anaweza kuanguka,” alisema


Mulhat alisema mbali na huduma hiyo ya PBB, uwanja huo pia umeanza kutumia mitambo ya inayomsaidia rubani kuegesha ndege (VEDS) bila kuwapo kwa muongoza ndege kama ilivyozoeleka.


Alisema miongoni mwa viapumbele vya ZAA, ni usalam wa raia na mizigo yao hivyo hata abiria atapita katika eneo mahususi bila kukosea njia ya kutoka uwanjani humo akipita eneo ambalo halihusiki kwasababu anapata mwongozo wa moja kwa moja kupitia madaraja hayo.


Baada ya kuzindua huduma hiyo, hivyo itakuwa miongoni mwa mapato ya uwanja wa ndege.


Serikali ya Zanzibar imewekeza dola za kimarekani 128 milioni (Sh297 bilioni) katika ujenzi wa uwanja huu uwanja huo wenye uwezo wa kuhudumia watu milioni 1.6 kwa mwaka, kwahiyo inalenga huduma hizo ziendane na uwekzaji uliofanywa.