UWEKEZAJI: Serikali, Airtel wavutana hisa za TTCL

“Ni kweli jana (Juni 24, 2014) kulikuwa na kikao cha majadiliano...Jambo hili linasimamiwa na Wizara ya Fedha na mpaka leo sijapata ripoti ya kikao hicho.”

Profesa Mbarawa

Muktasari:

  • Ni kuhusu  thamani ya hisa zao katika kampuni ya Simu ya TTCL

Dar es Salaam. Kumekuwa na mvutano mkali baina ya Serikali na Kampuni ya simu za mkononi ya Bharti Airtel kuhusu hatima ya asilimia 35 ya hisa ambazo kampuni hiyo inamiliki ndani ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).

Mvutano huo uliodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, unaiweka njiapanda Serikali ambayo kwa miaka kadhaa imeshindwa kutekeleza mpango wowote wa kibiashara, kutafuta mwekezaji mpya au mbia ili kuiwezesha TTCL ‘kufufuka’.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa mvutano katika mazungumzo hayo unatokana na Bharti Airtel kukataa malipo ya Sh5 bilioni yanayopendekezwa na Serikali ili kampuni hiyo iondoke TTCL, licha ya kwamba kiwango hicho ni kikubwa kuliko thamani ya hisa hizo, ambayo Sh3.8 bilioni.

Badala yake kampuni hiyo ya India ambayo ni Kampuni mama ya Airtel Tanzania, inataka ilipwe Sh21.5 bilioni, huku ikidaiwa kwamba haijawahi kuwekeza chochote ndani ya TTCL sawa na watangulizi wake; Celtel Tanzania, Celtel International na Zain.

Februari 21, 2001, TTCL ilisaini mkataba na Kampuni ya SMI/Detecon ambayo ilinunua asilimia 35 ya hisa kwa Dola za Marekani 120 milioni (Sh198 bilioni).

Hata hivyo, kiasi kilicholipwa ni Dola 65 milioni tu (Sh107.3 bilioni) kwa ahadi kwamba kiasi kilichosalia kingelipwa baada ya hesabu za TTCL kukaguliwa.

Baadaye MSI/Detecon ambao ulikuwa ushirika wa Kampuni ya Mobile Systems International ya Uholanzi na Detecon ya Ujerumani, ilitumia leseni ya biashara ya simu za mkononi iliyokuwa mali ya TTCL, kuanzisha Celtel Tanzania.

Baada ya kuundwa kwa Celtel Tanzania, TCCL walipewa umiliki wa asilimia 40 ya hisa, baada ya muda mfupi, hisa hizo zilihamishiwa Hazina, hivyo kuiacha TTCL bila hisa wala biashara ya simu za mkononi.

Katika mchakato huo, Celtel Tanzania iliuzwa kwa Celtel International ambayo baadaye iliuzwa kwa Zain. Juni 2010, Zain iliuzwa kwa Kampuni ya Bharti Airtel Limited ambayo ndiye mmiliki Airtel Tanzania.

Hata hivyo, taarifa zinaonyesha kuwa hadi MSI/Detecon walipoondoka nchini 2005, walikuwa wamelipa si zaidi ya Dola za Marekani 8 milioni kati Dola 55 milioni walizokuwa wakidaiwa.

Majadiliano

Habari zilizolifikia gazeti hili zinasema majadiliano kati ya Serikali na Airtel yalianza Aprili 19, 2013 na kikao cha mwisho kilifanyika Juni 24, mwaka huu mjini Dodoma lakini hakuna mwafaka uliofikiwa baada ya pande zote kuendelea kushikilia msimamo wake.

Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Patrick Makungu kwa nyakati tofauti walithibitisha kufanyika kwa vikao hivyo, lakini wakasema wenye uwezo wa kuzungumzia hatua iliyofikiwa ni Hazina.

Juni 25 mwaka huu, Profesa Mbarawa katika ujumbe wa maandishi kupitia simu yake ya mkononi alisema: “Ni kweli jana (Juni 24, 2014) kulikuwa na kikao cha majadiliano, kwa bahati mbaya mimi sikuwapo kwa sababu siyo mjumbe wa kamati hiyo. Jambo hili linasimamiwa na Wizara ya Fedha, wao ndiyo wanaosimamia mali za Serikali na mpaka leo sijapata ripoti ya kikao hicho.”

Kwa upande wake, Dk Makungu alisema: “Kwa maana ya usimamizi na uendeshaji, TCCL ipo chini ya wizara yetu, lakini yanapokuja masuala ya fedha na mali za kampuni hiyo, watu wanaoweza kuyazungumzia ni Wizara ya Fedha.”

Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba licha ya kukiri kuwapo kwa majadiliano hayo alisema hakuwa amepata taarifa rasmi kutoka kwa watendaji wa wizara yake kuhusu hatua iliyofikiwa, hivyo kutaka apewe muda wa kufuatilia.

Mara kadhaa kati ya Jumatano, Juni 25, 2014 na jana, mwandishi wetu alimtafuta Katibu Mkuu – Hazina, Dk Servacius Likwelile kupitia simu ya mkononi lakini kwa zaidi ya mara 10 alizopigiwa hakupokea na hata alipoandikiwa ujumbe mfupi (SMS) hakujibu.

Kwa upande wake, Kampuni ya Bharti Airtel ilisema mazungumzo yanaendelea lakini haikuwa tayari kuzungumzia hatua iliyofikiwa hadi sasa.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano – Mallya katika baruapepe aliyoituma kwa gazeti hili jana alisema: “Kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Kitengo cha Mawasiliano ya Airtel Afrika, Michael Okwiri, majadiliano yanaendelea na hivi sasa hatuko kwenye nafasi ya kuzungumzia suala hilo.”

Mabishano

Mvutano uliopo ulianzia katika taarifa ya Airtel kuhusu udhamini wa TTCL uliofanywa na mtaalamu mwelekezi wa Bhat Airtel; Kampuni ya Hesabu ya KPMG ambayo ilibainisha kuwa thamani ya hisa za Airtel (asilimia 35) ni kati ya Sh11.49 bilioni na Sh38.345 bilioni huku ikibainisha fursa za TTCL kukua hasa katika kutoa huduma za data.

, Airtel ilithibitisha nia yake ya kuondoka TTCL na kuibaki katika biashara ya simu za mkononi ambako imewekeza mtaji mkubwa.

Habari zinasema timu ya Serikali katika majadiliano hayo (GNT), ilikosoa taarifa ya KPMG na kutoa mfano kwamba hata matarajio ya ongezeko la wateja (projections on customer base growth) lililotajwa halina uhalisia kwani kwa mujibu wa taarifa za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wamekuwa wakipungua kila mwaka. Kadhalika, GNT ilisema mapendekezo mengi ya KPMG yanaonyesha kuwa mafanikio ya TTCL yanategemea uwekezaji wa kiwango kikubwa ambao hivi sasa unafikia Sh336 bilioni, fedha ambazo Bharti Airtel haiko tayari kuchangia.

“Kutokana na historia ya uanzishwaji wa Bharti Airtel, ambapo fedha pamoja na miundombinu ya TTCL ilitumika, kuna uwezekano wa Bharti Airtel kuharibu sifa yake mbele ya jamii ya Watanzania endapo itang’ang’ania kulipwa kiasi kikubwa cha fedha,” inasomeka sehemu ya taarifa ya GNT ambayo gazeti hili limeiona na kuongeza:

“TTCL ina madeni makubwa ambayo kama siyo Serikali kuendelea kutoa uthibitisho kwa wakaguzi wa kuendelea kuisimamia (letter of comfort/support), basi ingefilisiwa na Bharti wasingepata kitu.”

Kwa kuzingatia hoja hizo, Serikali ilipendekeza Bharti Airtel ilipwe Dola moja ya Marekani, wazo ambalo lilipingwa na kampuni hiyo, ambayo ilitaka malipo ya Sh25 bilioni ili iondoke TTCL.

Baada ya majadiliano, GNT walipendekeza malipo ya Sh5 bilioni kwa Bharti Aitel, lakini lilikataliwa wawakilishi wa kampuni hiyo, ambao walipunguza kiwango wanachotaka kulipwa kutoka Sh25 bilioni za awali, hadi Sh21.5 bilioni lakini Serikali haikuafiki.

Katika mazungumzo hayo, Serikali ilitoa hoja ya kutaka Juni 30, mwaka huu iwe tarehe ya mwisho ya Bharti kuwapo TTC, ili kutoa nafasi ya kuanza mkakati wa kuinusuru kampuni hiyo.

 Hoja hiyo pia ilikataliwa na Bharti ikisema lazima yawepo makubaliano ya masharti ya kuondoka, ikiwa ni pamoja na malipo.

Baada ya kushindwa kuafikiana, Bharti iliomba wiki mbili ili kushauriana na mamlaka ya juu ya kampuni hiyo, hivyo kikao kingine kimepangwa kifanyike Julai 18, mwaka huu.