Uzinduzi wa Mbio za Mwenge kugharimu Sh1 bilioni

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako akisalimiana na viongozi wa Mkoa wa Mtwara mara baada ya kuwasili ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Ahmed Abas leo Machi 6, 2023. Picha na Mwanamkasi Jumbe.

Muktasari:

  • Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu wa 2023 zinatarajia kuzinduliwa rasmi kitaifa mkoani Mtwara Aprili 2 katika viwanja vya Nangwanda Sijaona.

Mtwara. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako ameutaka Mkoa wa Mtwara kuhakikisha unafanya vizuri katika eneo la hamasa siku ya uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru.

 Zaidi ya Sh1 bilioni zinahitajika kwa ajili ya shughuli za uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mkoani hapa.

"Kubwa ni kwenye hamasa, shughuli ni watu ninawaomba kwenye eneo hilo muendelee kufanya vizuri kikawaida mkoa tunaozindulia ndio unaoweka viwango. Mwaka jana tulizindua mkoani Njombe na walifanya vizuri sasa viwango huwa havishuki vinapanda, Mtwara kuchele tunategemea mtafanya vizuri," amesema Ndalichako.

Ndalichako amesema hayo leo Machi 6, 2023 wakati alipofika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kabla ya kuanza ziara ya kukagua maandalizi ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru.

Ameupongeza mkoa kwa utayari na maandalizi kwa ajili ya tukio hilo la Kitaifa na kuongeza kuwa Mwenge ni alama ya umoja kama Taifa ulioasisiwa na Hayati Julius Kambarage Nyerere.

Lengo la mbio za Mwenge wa Uhuru ni kuleta matumaini na unatumika kama chombo cha kumulika na kukemea maovu, kudumisha amani pia ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo na uwajibikaji miongoni mwa watendaji ndio sababu hupita kuzindua na kukagua miradi mbali mbali.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abas amesema kuwa ikiwa zimebaki siku 28 kuelekea siku ya uzinduzi wa mbio hizo maandalizi yanaendelea vizuri ikiwemo mafunzo ya halaiki kwa vijana 1,000 kwa kushirikiana na bendi ya Mgulani na vikundi mbali mbali vya uhamasishaji.

Mwenyekiti wa  Kamati ya Mapambo na Miundombinu, Mhandisi Ng'ondya Rejea amesema maandalizi katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona ambako ndiko tukio litafanyika yatakamilika ndani ya juma hili.