Uzinzi unavyogharimu mipango ya familia nyingi

Muktasari:

Ninapata chai ya jioni na Injinia. Jamaa kafanikiwa. Maisha yake yanaongea na kuhamasisha wengi. Jamaa anaheshimika na kanipa heshima ya kikao. Simu zimeachwa yatima mezani kwa takribani saa mbili zilizopita.

Na Christian Bwaya

Ninapata chai ya jioni na Injinia. Jamaa kafanikiwa. Maisha yake yanaongea na kuhamasisha wengi. Jamaa anaheshimika na kanipa heshima ya kikao. Simu zimeachwa yatima mezani kwa takribani saa mbili zilizopita.

Injinia anaomba kutoka akateme mate kidogo. Namruhusu. Ninatafakari mambo aliyokwishaniambia mpaka sasa. Usimfiche jambo mkeo. Mke ndiye atabaki na wanao siku wewe haupo. Maneno mazito ambayo ukiyasema kwa wanaume wengi unaonekana hujitambui. Ishini na wake zenu kwa akili. “Hii ina maana gani?” ninatafuta uzani wa kuyatathmini maneno ya Injinia. Dakika zipatazo tano huyo Injinia karudi. Darasa linaendelea,

“Wanaume wengi hawafanikiwi kwa sababu wanaelekeza nguvu na muda mwingi kufanya vitu visivyochangia mafanikio yao. Tusiende mbali. Nguvu za wanaume wengi zinaishia kwenye uzinzi. Uzinzi ni gharama. Uzinzi ni umaskini.” Ninacheka kwa aibu. Injinia anacheka kwa kejeli na kupigilia msumari, “Wewe muda wote unawaza wanawake wa kuhonga mipango ya maana unapanga saa ngapi?”

Msumari wa moto unanikumbusha mazungumzo yangu na wanaume fulani nikiwa Babati wiki iliyopita. Wao walikuwa wanaamini michepuko ndio hamasa ya mafanikio. Nikalileta jambo hilo mezani, “Ujinga mtupu. Unajua kuna umri ukifika mwanaume hupaswi kuwa unahangaika na wanawake wa nje. Natamani wanaume wengi wangeelewa namna uzinzi unavyogharimu maisha yao. Ukiwa mzinzi unakausha nafsi yako na hatia zisizo na sababu. Unakuwa na vitu vingi vya kuficha, unaishi maisha ya kujistukia, una wasiwasi, hujui lini upumbavu unaouficha utafahamika. Sijui kwa nini watu huwa hawalioni hili?”

“Lakini chief si unafahamu wapo wazinzi wengi wenye fedha mjini hapa?” Namchokoza nione atasemaje. Uso wake unazizima, “Nani kakwambia kila mwenye fedha kafanikiwa? Huwezi kupata fedha kwa njia chafu ukaniambia umefanikiwa. Sisi hapa tunaongelea mafanikio yanayopatikana kwa kanuni. Mafanikio yanayoleta utulivu kwenye familia. Hatuongelei janja janja za kupiga dili halafu mtu anasema kafanikiwa.”

“Nikupe mtazamo mwingine kidogo. Unajua hii michepuko inayosumbua wanaume wengi ukiangalia vizuri ni biashara ya utafutaji tu na ombaomba wanaotumia wanaume wajinga kuendesha maisha yao. Mwanaume ukikosa akili utajikuta unatumia fedha nyingi kumtunza mwanamke asiye na akili kama wewe. Hana akili kwa sababu anafanya kitu ambacho yeye mwenyewe asingependa kufanyiwa.”

Hoja nzito hii. Namwona Injinia anagida kinywaji chake kidogo na kunitazama kwa kujiiba kidogo kama mtu anayepima namna ninavyopokea busara zake. Ninatingisha kichwa kuashiria kukubaliana naye. Ninagida na mimi. Injinia anaendelea,


“Ukijiuliza kwa nini mwanaume uhangaike na hayo yote unakuta ni kutokujitambua tu. Mwanaume mzima unachezewa na wanawake? Unaruhusuje mwanamke mwingine akuchezee kwa faida unayoweza kuipata kwa mke wako?” Natafakari hilo neno kuchezewa na wanawake. Tumezoea wanaume ndio wamekuwa wakiwachezea wanawake. Sasa Injinia anasema wanawake siku hizi ndio wanawachezea wanaume.

“Unajua tunapoteza ubunifu mwingi kwa mambo ya kipuuzi. Kwa mazingira yetu, ukishafika miaka arobaini, kwa tuliowengi, angalau unajua unataka nini kwenye maisha. Kama ni biashara unajua aina ya biashara inayoendana na uwezo wako. Kama ni kazi umeshatulia. Elekeza nguvu zako zote kupiga kazi. Umri huo una mke na watoto. Hao wote wanategemea heshima yako na kujituma kwako. Jielekeze kujenga familia achana na hawa wahuni wanaokutumia kuendesha maisha yako.”

Saa nne. Nimekutana na Injinia mshunuzi. Tunaagana. Nawaza mambo mengi kuhusu mafanikio na familia. Kuna ukweli mwingi katika maneno ya Injinia.