Veta, airtel kuwafuata wanaotaka kujifunza ufundi waliko

Afisa Matukio wa Airtel Dangio Kaniki (kulia) akimuonyesha application ya VSOMO Mkuu wa Usajili Veta Kipawa, Harold Mganga (katikati) pamoja na Mratibu wa Miradi na Kozi fupi Veta Kipaw Gosbert Kakiziba (kulia).

Muktasari:

Mfumo wa mafunzo ya ufundi kwa njia ya mtandao ulioanzishwa na Veta na Airtel unatoa fursa kwa vijana wengi kusoma kwa gharama ndogo.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi Tanzania (Veta) kupitia mfumo wa mafunzo kwa mtandao wa VSOMO unaodhaminiwa na kampuni ya simu za mkononi ya Airtel, imebainisha kuwa iko tayari kuhudumia vikundi au jamii ya wanaotaka kujifunza ufundi stadi kwa kupeleka timu yao ya mafunzo kwa vitendo popote walipo.

Veta imesena hatua hiyo inalenga kuhakikisha dhana ya uchumi wa viwanda inakamilika kwa kuwa na mafundi wazuri waliohitimu katika mafunzo mahiri.

Hayo yamebainishwa na Lucius Luteganya, Mkuu wa Chuo cha Veta Kipawa, ambae pia ni msimamizi wa mradi wa mafunzo kwa njia ya simu unaodhaminiwa na Airtel kwa lengo la kutoa fursa kwa vijana wengi maeneo ya mijini.

“Veta tuko tayari kuwafuata wanafunzi wetu endapo watajiandikisha na kuhamasihana kwa kuunda kikundi kwa ajili ya kusoma kwa njia ya mtandao wa VSOMO. Ikiwa watakuwa vijana kuanzia 15 hadi 20 na wakipenda kupata mafunzo basi sisi tutawafuata hukohuko waliko,” amesema.

Kupitia mtandao wa Vsomo, kuna kozi 12 na wanafunzi wanaweza kujisomea popote alipo mara baada ya kupakua application hiyo.

“Tunampango waongeza kozi zingine  15 hivi karibuni lakini kwa sasa zilizopo tayari kwenye mtandao,” ameongeza.

Alizitaja baadhi ya kozi hizo kuwa ni pamoja na chakula na mbinu za kuhudumia wateja, matengenezo ya kompyuta, umeme wa viwandani, ufundi bomba wa majumbani, umeme wa magari, ufundi umeme wa majumbani, ufundi pikipiki na ufundi wa simu za mkononi.