Veta yaja kivingine kukabili changamoto ya ajira kwa vijana

Mkurugenzi wa Hakielimu, Dk John Kalage akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuwajengea uwezo walimu wa vyuo vya ufundi  kuendana na soko la ajira na matumizi ya teknolojia.

Muktasari:

  • Mradi waanzishwa kukuza uwezo wa walimu kusaidia wanafunzi kujiajiri.

Dar es Salaam. Katika kukabiliana na ombwe lililopo kati ya mahitaji ya soko la ajira na wataalamu katika Vyuo vya Elimu ya Mafunzo na Ufundi Stadi (Veta), vyuo hivyo vimeanza kutekeleza mradi utakaozalisha wahitimu wenye ujuzi na tija kwenye soko la ajira.

 Mradi huo wa ushirikiano na uendelezaji wa sekta ya elimu ya ufundi na mafunzo Tanzania (TVET), unafadhiliwa na Jumuia ya Umoja wa Ulaya (EU).

Mradi huo pia unalenga kuwanoa na kuwajengea uwezo wakufunzi katika kutumia teknolojia kufundisha na kusambaza maarifa, ili kutoa wahitimu wanaoendana na mahitaji ya soko la ajira katika karne hii ya sayansi na teknolojia.

Hatua hiyo imefikiwa katika kipindi ambacho Tanzania inaendelea kufanyia mageuzi sekta ya elimu kwa kuleta mitalaa inayolenga kuwajengea ujuzi wanafunzi badala ya maarifa pekee. 

Tayari taasisi za elimu ya juu nchini hasa vyuo vikuu vya Serikali vinatekeleza mradi kama huo wa kimkakati kwenye sekta ya elimu utakaowezesha mfumo wa elimu ya juu ujikite zaidi katika kutoa elimu ujuzi ambayo itawafanya wahitimu waweze kuzalisha ajira au kujiajiri.

Mradi huo kwa ngazi ya vyuo vya ufundi utatekelezwa kwa ushirikiano baina ya Shirikika la Hakielimu, Chuo Kikuu cha HAMK cha nchini Finland, Taasisi ya Mafunzo na Uendelezaji Tekinolojia ya 3DBear na SCV, Chuo cha Ualimu wa Mafunzo ya Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC) na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume Zanzibar.

Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano ya ushirikiano, jana Januari 27, 2024 Mkurugenzi wa Shirika la HakiElimu, Dk John Kalage amesema mradi huo utajikita kuimarisha ushirikiano kati ya TVET nchini na sekta binafsi, lengo likiwa kujenga uhusiano wenye nguvu baina ya taasisi hizo, wajasiriamali na mahitaji ya soko la ajira.

“Mradi unalenga kukuza uwezo wa walimu, ili wasaidie wanafunzi wao kujiajiri, hii pia inalenga kuwapa walimu maarifa na ujuzi wa kuwasaidia wanafunzi wao wajue fursa za ujasiriamali na jinsi ya kuanzisha biashara,” amesema Dk Kalage.

Meneja mradi, Carita Cruz amesema mradi huo pia utawajengea uwezo walimu wa vyuo vya ufundi na mafunzo wa kutumia teknolojia ya kidijitali katika kufundisha, ili kurahisisha uelewa wa wanafunzi na kuwafanya waweze kukabiliana na dunia ya ajira ya kisasa.

Amesema programu hiyo itatoa fursa kwa walimu na vyuo vinavyoshirikiana, kufanya ziara za mafunzo nchini Finland kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu.

“Hii itaruhusu taasisi zilizo chini ya Veta kuona jinsi nchi nyingine zinavyotekeleza dhana hii ya ushirikishaji walimu wa ufundi na mafunzo katika matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika ufundishaji.

“Lengo ni kuwawezesha walimu na taasisi za elimu ya ufundi kuboresha mafunzo wanayotoa, ili kuwafanya vijana wapate ajira kwa urahisi au kuanzisha biashara zao wenyewe,” amesema Carita.

Mradi huo wa miaka mitatu (2024-2026) utawanufaisha zaidi ya walimu-wanafunzi 660 wanaodahiliwa katika chuo cha MVTTC ambao wataongeza idadi ya walimu wanaofundisha katika vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi na vyuo vya ualimu wa mafunzo ya ufundi nchini.

Pia utanufaisha wanafunzi 66,459 wanaodahiliwa katika vyuo hivyo ambao watafundishwa na walimu waliojengewa uwezo.

Pamoja na hayo, mradi huo utanufaisha wajasiriamali katika sekta binafsi ambao wamekuwa na hitaji la kupata wafanyakazi na wasimamizi wa shughuli zao wenye ujuzi na stadi zinazokidhi mahitaji ya soko, ili kuzalisha faida zaidi.